Habari

Mfumo wa kodi ZRB kufanyiwa mageuzi

NOVEMBER 14, 2017 BY ZANZIBARIYETU

Na Mwandishi wetu

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed, amesema Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ina dhamira ya kufanya mageuzi katika mfumo mzima wa kodi ili uendane na wakati uliopo.

Aliyasema hayo katika sherehe ya kuwaaga wajumbe wa bodi ya sita ya ZRB, katika hafla iliyofanyika ofisi za bodi hiyo Mazizini Unguja.

Alisema, katika mwaka huu wa fedha, ZRB itafanya mapitio ya mfumo wote na vyanzo vyote, sambamba na kuibua vyanzo vyengine vya mapato, ili kupanua wigo wa ukusanyaji kodi na kuhakikisha wale wote wanaopaswa kulipa kodi wanalipa.

Alisema mafanikio ya ZRB yana historia yake kupitia bodi zilizopita, hivyo hawawezi kusahau historia hiyo ambayo imeleta mafanikio kwa chombo hicho.

“Bodi hizi ikiwemo hii iliyopita ni kisima cha hazina, ambacho kinatakiwa kuenziwa ili kuendelea kupata mafanikio zaidi,” alisema.

Aidha alisema kutokana na ushirikiano huo, mapato yanaongezeka siku hadi siku kwani bila ya kukilea chombo hicho na bila ya kuwa na kazi nzuri, mafanikio hayo yasingepatikana.

Akitaja ongezeko la mapato kwa mwaka 2011/2012 alisema mapato kwa ujumla yanayojumuisha ZRB na TRA yalikuwa shilingi bilioni 204.91 na huku shilingi bilioni 258.77 zilikusanywa kwa kipindi cha 2012/2013.

Kwa mwaka 2013/2014 alisema vyombo hivyo vilikusanya shilingi bilioni 318.42, 2014/2015 shilingi bilioni 345.42, mwaka 2015/2016 shilingi bilioni 408.99 na 2016/2017 walikusanya bilioni 521.88 ambapo ni ongezeko la asilimia 27.

Alibainisha kuwa kutokana na mafanikio hayo, serikali imeweka lengo la kukusanya mapato ya shilingi bilioni 675.81 kwa mwaka 2017/2018.

Mbali na hayo, alisema serikali pia imepunguza utegemezi katika bajeti kutoka asilimia 15.5 mwaka 2011/2012 hadi asilimia 7.1.

Aliahidi kuwa, serikali itaendelea kuimarisha uwekezaji wa ndani na nje, ili kukuza fursa za ajira kwa vijana kwa lengo la kukuza mapato na kujikwamua na ukali wa maisha unaowakabili.

Mbali na hayo, alisema kuna changamoto zinazoikabili bodi hiyo ikiwemo magendo ya mafuta, makusanyo madogo hasa mapato yasiyo ya kodi na uelewa mdogo kwa baadhi ya wananchi na wafanyabiashara, juu ya umuhimu wa kutoa na wananchi kudai risiti.

Hivyo aliiomba ZRB, kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji katika kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi, ili kuhakikisha kodi ya serikali inakusanywa kama ilivyokusudiwa.

Kamishna wa ZRB, Amour Hamil Bakar, alisema bodi hiyo imeleta mafanikio makubwa na hawana budi kuyaendeleza ili kuendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.

Nae, Mwenyekiti mstaafu wa bodi hiyo, Abrahman Rashid, aliipongeza bodi mpya iliyoteuliwa na kuomba kufanya kazi kwa ushirikiano kwa kujenga misingi ya uongozi ili kufikia lengo la ukusanyaji mapato.

Zanzibar Yetu

Share: