Habari

Mfumo wa vyama vingi ni uamuzi wa watanzania

Picha ni viongozi wa CCM waasisi wa mfumo wa siasa wa chama kimoja na baadaye vyama vingi; kutoka kushoto ni Mzee Mwinyi, Kikwete, Mangula na Mkapa. Matatizo mengi ya kisiasa yanayoikumba Tanzania kwa sasa wanayaona na wanayashuhudia, hatujasikia sauti zao!. Picha kutoka mitandao ya kijamii

by Selemani Rehani – Raia Mwema
Wednesday, March 21, 2018

“JAMHURI ya Muungano ni nchi ya kidemokrasia na ya kijamaa, isiyokuwa na dini, yenye kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.” (Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, sura ya kwanza, ukurasa wa 19).

Nimeona nianze na nukuu hiyo, ili tuweze kukumbushana kuwa, pamoja na kasoro zilizopo katika katiba yetu ya mwaka 1977, ni vyema tukaelewa kuwa tuliamua kama watanzania kufuata mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa katiba na kwa mujibu wa sheria za nchi yetu. Walioko katika vyama vingi, wanatekeleza haki yao na wajibu wao wa kikatiba, na kama raia. Kama vile ambavyo wana haki kwa mujibu wa katiba na sheria za vyama vingi vya siasa, pia wanao wajibu.

Nukuu hiyo hapo juu inaeleza wazi kabisa nchi hii inafuata mfumo wa vyama vingi. Hilo halina mjadala. Kuna tatizo kidogo katika kipengele hicho cha katiba, pale inaposema ni nchi ya ‘kidemokrasia’ na ya ‘kijamaa’. Maneno haya mawili yananipa taabu kidogo. ‘kidemokrasia’ na ‘Kijamaa’.

Nadhani bado hatujafika huko kuwa ni nchi ya demokrasia na pia sina hakika sana kama kweli tunafuata siasa ya ujamaa.

Nadhani ujamaa tulikwisha uweka kando. Labda, demokrasia kwa maana ya dhamira yetu ni kujenga nchi ya kidemokrasia.

Tufanye rejea kidogo. Mijadala na vuguvugu la kudai si tu mfumo wa vyama vingi bali kurudisha haki zote za uraia zilizoanza miaka ya 80 na 90. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alikuwa mstari wa mbele katika mjadala huu.

Mwanzoni mwa mwezi wa Februari 1990, aliitisha mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani na kusema kuwa “si dhambi kujadili mfumo wa vyama vingi”.

Baba wa Taifa katika juhudi zake za kutoa elimu na kubadilisha fikra za watanzania na hasa wana CCM wenzake, mwezi Mei mwaka 1990 akihutubia vijana wa CCM mjini Mwanza, Mwalimu Nyerere aliwausia vijana wa CCM kwenda na wakati.

Mwalimu alitumia fursa hiyo, kukosoa tabia ya kubweteka iliyopo CCM na kusema kuwa CCM imekuwa ni taasisi ya mashindano kati ya wanachama wake na kukosekana kwa upinzani kunakifanya chama hicho kubweteka na kujisahau katika kushughulika na malengo yake ya msingi.

Mwalimu aliwaasa vijana kuingia katika ushindani kwani wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa urasimu na kubweteka.

Maneno haya yalisemwa na hayati Baba wa Taifa mwaka 1990 nadhani maneno haya yana ujumbe mzuri sana katika kipindi hiki cha sasa na miaka mingi ijayo. Kwa sasa, CCM kimekuwa mzigo mzito kwa Jeshi la Polisi ili kuweza kuonekana na wananchi kuwa kinakubalika.

Katika kujibu shinikizo la kudai vyama vingi, serikali ya CCM, mwaka 1991 iliunda Tume iliyoitwa Tume ya mfumo wa chama kimoja au vyama vingi, wakati mwingine iliitwa Tume ya Nyalali.

Tume hii ilipewa hadidu za rejea. Moja ya hadidu za rejea ilikuwa ni kupendekeza mabadiliko muhimu na ya lazima ya katiba, sheria za nchi na mabadiliko ya kisiasa kwa dhumuni la kulinda taifa na muungano.

Tarehe 17 Februari 1992, tume ilikabidhi ripoti kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na mapendekezo mengine, tume ilipendekeza Tanzania iingie katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Ilitoa sababu tatu.

Kwanza, pamoja na kuwa waliopendelea tuingie katika mfumo wa vyama vingi ni wachache, bado idadi hiyo ni muhimu na kubwa na haiwezi kupuuzwa (substantial minority); Hivyo tukiingia katika mfumo wa vyama vingi, itasaidia kulinda na kutunza amani na umoja.

Pili, wengi ambao walipendekeza tubakie katika mfumo wa chama kimoja pia walitaka mabadiliko makubwa (fundamental reforms) yafanyike ndani ya mfumo wa chama kimoja.

Mapendekezo hayo hayawezi kufanyika bila kuingia katika mfumo wa vyama vingi. Na mwisho mapendekezo hayo yalifanyika kwa kuzingatia uzito wa mawazo na uzoefu wa siasa za vyama vingi nchini Tanzania.

Mwenyekiti wa CCM aliitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa mwaka huo huo wa 1992 ili kujadili ripoti ya Tume ya Nyalali na walikubaliana na mapendekezo ya tume ya kuingia katika mfumo wa vyama vingi.

Mwaka huo huo Halmashauri Kuu ya CCM ilipitisha azimio la kuitisha mkutano mkuu wa taifa kupitisha pendekezo la kuingia katika mfumo wa vyama vingi.

Mkutano Mkuu na wa kihistoria wa CCM uliitishwa na Mwenyekiti wa CCM wa wakati huo Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Mkutano huo ulifanyika kuanzia tarehe 18 – 20 Februari pamoja na mambo mengine uliitwa kujadili pendekezo la Halmashauri Kuu ya Taifa na kupitisha uamuzi wa kuingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mkutano Mkuu wa CCM ulipitisha uamuzi wa Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi. Akihutubia katika moja ya maandamano, Mwenyekiti wa CCM Ali Hassani Mwinyi alitaja sababu zifuatazo za CCM kukubali mfumo wa vyama vingi.

Alisema uamuzi huo una sababu za kisiasa, kiusalama, kidemokrasia na mikakati mizuri. Akasema kuwa kisiasa uamuzi huu unathibitisha kuwa CCM haiogopi upinzani. CCM inajiamini ni chama kinachokubalika na wengi.

Pia, chama kilikuwa hakitaki kuwapa nafasi wachache ambao wanaweza kuharibu amani ya nchi kwa kisingizio cha kudai mfumo wa vyama vingi.

Akaendelea kwa kusema kuwa CCM imeamua kurasimisha mfumo rasmi wa vyama vingi ili kuzuia wale ambao wanaweza kuanzisha vyama nje ya mfumo rasmi na kuleta machafuko. Akasema kuwa ni busara kwa Tanzania kujifunza kutokana na makosa ya nchi nyingine.

Ninayaeleza haya yote nikijaribu kusema tu kuwa mfumo wa vyama vingi tuliukubali sisi wenyewe, tuliupitisha sisi wenyewe na tuliamua kuufuta sisi wenywewe. Hivyo tuna kila sababu ya kuulinda, kuudumisha na kuuendeleza ili tuwe na vyama vya siasa vingi vyenye tija kwa Watanzania.

Kazi hii ni ya watanzania wote. Hakuna tija yoyote kubomoa upinzani wala kudhoofisha upinzani wala wote kujazana katika chama tawala.

Ndipo hapo yatupasa kurejea maneno ya Mwalimu Nyerere kwa vijana wa CCM na wakati mwingine aliwahi kusema kuwa CCM ni kokoro. CCM imara itapatikana kwa kuwa na upinzani imara.

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi yalifanya kikao kuanzia April hadi Mei 1992, kujadili mabadiliko muhimu ya kikatiba na sheria ili kuweza kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mei 7, Bunge lilipitisha muswada wa kuingia katika mfumo wa vyama vingi na kufuta vifungu vyote vya katiba ambavyo vilikuwa vinaipa CCM mamlaka ya kuwa chama pekee cha siasa nchini (monopoly). Kwa ujumla angalau vifungu 32 vilifanyiwa mabadiliko. Vifungu hivyo vilifutwa au vilifanyiwa marekebisho kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Nyalali.

Hatua iliyofuata ilikuwa ni ya kutunga, kujadili na kupitisha sheria ya vyama vingi vya siasa. Mwezi wa Mei 1992 serikali iliwasilisha muswada wa utaratibu wa kuendesha shughuli za siasa katika mfumo wa vyama vingi.

Katika Makala yake iliyotoka katika Gazeti la ‘The Daily News’ la tarehe 22 Februari mwaka 2018, Spika Mstaafu na Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Pius Msekwa ameeleza upande wa pili wa uamuzi wa kupiga marufuku mikutano ya siasa kwa vyama vya upinzani.

Amejaribu kutoa sababu nzuri za uamuzi huo, akasema kuwa uamuzi huo sio mpya hata wakati wa utawala wa Mkapa serikali iliwahi kupiga marufuku mikutano ya siasa.

Pamoja na sababu alizozitoa Msekwa, tungependa pia kueleza upande mwingine au wa tatu wa shilingi. Shughuli za siasa katika mfumo wa vyama vingi haziendeshwi na utashi au akili ya mtu, bali shughuli hizi zinaendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria ya vyama vingi vya siasa.

Mathalan, sheria ya vyama vingi vya siasa katika suala la vyama kufanya mikutano yake ya kisiasa inasemaje?. Naomba Msekwa anisaidie katika hili. Pia nasema kuwa hatajikita katika katiba wakati anajadili suala hili! Ila tu ataeleza upande mwingine wa shilingi wa suala hili.

Je utaweza vipi kujadili masuala ya mfumo wa vyama vingi vya siasa bila kugusia vifungu vya katiba na sheria ambavyo ndivyo vinaeleza namna ya kufanya shughuli za siasa, haki na wajibu wa vyama vya siasa nchini!?. Katiba inasema wazi kuwa:

“Mambo yote yahusuyo uandikishaji na uendeshaji wa vyama vya siasa nchini yatasimamiwa kwa mujibu wa masharti ya katiba hii na ya sheria iliyotungwa na bunge kwa ajili hiyo.”

Sheria ya vyama vingi nayo inasema: “Chama chochote chenye usajili wa kudumu kitafanya mikutano yake ya kitaifa, kimkoa na kiwilaya na katikia ngazi za chini kwa mujibu wa katiba.”

“Endapo chama kinakusudia kufanya mkutano au maandamano katika sehemu yoyote ya umma, chama kitatoa taarifa chini ya saa 48 kabla ya mkutano kwa Ofisa wa Polisi ambaye ni kiongozi wa eneo hilo amablo mkutano utafanyika.”

Iwapo shughuli za mfumo wa vyama vingi zinaendeshwa kwa mujibu wa katiba na kwa mujibu wa sheria ya vyama vingi vya siasa, si sahihi kuzuia mikutano ya vyama vya siasa kwa sababu yoyote ile.

Tunao wajibu wa kuheshimu, kuilinda na kutekeleza katiba na sheria za nchi. Iwapo tunaona sheria hii haiendani na wakati basi, ni muhimu kwa mamlaka inayohusika kupeleka muswada bungeni ili sheria hii ifanyiwe marekebisho na iseme wazi kuwa mikutano ya kisiasa itafanyika wakati wa uchaguzi tu na iseme wazi kuwa baada ya uchaguzi, siasa za vyama zinahamia bungeni.

Kwa nini hatubadilishi katiba na sheria ili kuweza kukidhi mtazamo huo mpya, ambao unazua maswali mengi sana?. Hivyo, kuna ugumu gani wa kufanya hilo na linawezekana.

Nadhani iwapo mikutano ya hadhara na maandamano vitazuiwa kupitia utaratibu wa sheria ni jambo jema na kuondoa mivutano iliyopo sasa.

Kuweka amri kwa kutumia Jeshi la Polisi kuzuia mikutano na maandamano kwa vyama vya siasa vya upinzani ni uvunjifu wa sheria na katiba ya nchi, ilhali CCM kinafanya shughuli zote za kisiasa bila kubugudhiwa.

Tuache tabia ya kuamini kuwa Jeshi la Polisi litaibeba CCM milele na kuvigandamiza vyama vya upinzani na viongozi wake. Tusijidanganye, itafika siku Jeshi la Polisi litachoka kufanyakazi za kisiasa.

Chama cha siasa kinaponyimwa fursa ya kunadi sera zake, kinanyimwa haki yake ya kikatiba na uraia. Wakati wote chama kikuu cha upinzani na vyama vingine vina wajibu wa kuwasilisha sera mbadala na mawazo mbadala na kuikosoa serikali, ndani ya bunge na nje ya bunge.

Katiba yetu na sheria ya vyama vingi vya siasa haisemi kuwa mikutano itafanyika wakati wa uchaguzi tu, la hasha haisemi hivyo, pia haisemi kuwa uchaguzi ukiisha basi eti siasa zitahamia bungeni, la hasha haisemi hivyo.

Yapo masuala ambayo ni muafaka kuyajadili bungeni na yapo masuala ambayo ni muafaka kuyaeleza katika mikutano ya kisiasa na maandamano.

Pia, sote tufahamu namna bunge letu linavyoendeshwa. Sidhani kama kuna mtu anayeweza kukataa ukweli kuwa wabunge kutoka vyama vya upinzani hawapewi fursa sawa na mara nyingi uchache wao unatumika kama fimbo ya kwachapia na kupitisha mambo na wakati mwingine wanayimwa nafasi au wanaamriwa kufuta na kurekebisha baadhi ya michango yao au hotuba zao. Hivyo, bunge pia halitoi uwanja sawia katika kufanya siasa.

Hivyo, nakubaliana na kauli ya Maaskofu Katoliki kuwa kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni kwenda kinyume cha katiba ya nchi. Hili ni kweli na halipingiki kwa sababu zozote zile zitakazotolewa.

Kama kuna upungufu katika katiba yetu, basi ni wakati muafaka sasa kufanya mabadiliko. Asasi za kiraia takribani 105 pamoja na masuala mengi, asasi hizi zilitoa tamko na kusema:

“Serikali itazame upya suala la upatikanaji wa katiba mpaya kwani ndiyo suluhisho la matatizo mbalimbali katika jamii kwa sasa, kwani suala la katiba mpya kimekuwa ni kilio kikubwa na hitajio la watanzania ili kutibu hali hii inayojitokeza sasa.”

“Tunashauri mchakato wa katiba ufanyike mwaka huu kwa kuwa mwaka 2019 na 2020 taifa litakuwa na shughuli nyingi na mambo ya uchaguzi.”

Kwa wale viongozi na wananchi wenye mtazamo hasi kuhusiana na vyama vya upinzani, tukumbushane kuwa tuliamua wenyewe kuingia katika mfumo wa vyama vingi na vyama hivi vipo kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi kama ilivyoelezwa hapo juu.

Vyama hivi vina haki na wajibu ambao umeleezwa bayana na katiba na sheri inayoshugulika na vyama vya siasa. Kama tulikubali kuingia katika mfumo wa vyama vingi, ni wazi kuwa tutakuwa na vyama mbalimbali, vyenye mipango na sera tofauti.

Na vyama hivi ipo siku moja vinaweza kushika dola. Basi ni muhimu sote tufanye juhudi za kuwa na vyama bora na makini vyenye sera mbadala na program nzuri na organizeshini nzuri, ili siku vikija kushika dola nchi yetu iendelee kuwa salama, amani na ipate maendeleo na ustawi.

Sisi wote ni Watanzania na tunajenga nyumba moja ila tunatofautiana mikakati na mipango. Adui yetu sote ni umaskini, maradhi, ujinga, rushwa, ufisadi, uwongo na unafiki.

Imeandikwa na Selemani Rehani – 0756 20 96 66, srehani@hotmail.com

Tagsslider
Share: