Habari

Mgelema waikumbusha serikali ujenzi wa barabara yao

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

WANANCHI wa shehia ya Mgelema wilaya ya Chakechake kisiwani Pemba, wameikumbusha serikali ahadi ya kuwajengea barabara yao kwa kiwango cha lami, kama ilivyoahidi hivi karibuni.

Walisema wanaendelea kutesema na barabara hiyo hasa kipindi hichi cha mvua za masika zikiendelea kunyesha, kwa vile hulazima kwenda kwa mguu na mizigo yao kichwani.

Walisema wanaona choyo ya kimaendeleo kwa kijiji jirani cha shehia hiyo eneo la Ngomeni, kwamba sasa wameshasahu machungu kwa kujengewa barabara kwa kiwango cha lami, ingawa wao bado wanateseka.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kijijini hapo, wananchi hao walisema, wanaelewa kuwa serikali imeshaahidi kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, lakini sio vibaya kuikumbusha kutokana na matatizo wanayokumbana nayo.

Mmoja kati ya wananchi hao Ali Kheir Makame, alisema kwa kipindi chote cha mvua, lazima watembea kwa miguu kutoka kijijni kwao Mgelema hadi barabara kuu eneo la Kipapo kusubiri usafiri wa umma.

“Tumekuwa tukipata tabu na usumbufu mkubwa, maana siku kama hizi mvua, barabara inachimbuka na kutokeza mashimo ambayo hairusu gari kupita,”alieleza.

Nae Hadia Hassan Chumu na Asha Khalfan Amour walisema, tabu na mashaka zaidi huyapata wanapotaka kwenda hospitali kuu ya Chakechake kwa ajili ya uchunguzi.

“Mvua kama hizi gari hata vile vikeri ambavyo huwa tunapeana msaada wa dharura kwa ugonjwa na mama mjanzito, imekuwa ni shida, sasa serikali iharakishe kutujengea kwa kiwango cha lami,”alishauri Hadia.

Hata hivyo Asha Khalfan, alisema hata usafiri wa kupitia bahari kwa kipindi kama hichi cha mvua, ni kujiongezea matatizo, maana mito imechimbuka ni hatari tupu,”alieleza.

Sheha wa shehia ya Mgelema Omar Iddi Zaina akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, alisema ni kweli serikali imeshaahidi kuijenga kama ilivyofaya kijiji cha Ngomeni shehiani humo.

“Mimi naamini serikali inaelewa kilio na tabu tunayoipata wananchi wa shehia ya Mgelema kwa barabara yetu kuwa mbaya kwa siku za mvua, illa nawataka wananchi wawe wastahamilivu,”alifafanua.

Mkuu wa wilaya ya Chakechake Rashid Hadid Rashid, alisema muda mfupi ujao serikali itatimiza azma yake ya kuijenga barabara hiyo kama ilivyo ahidi.

Alisema serikali haijawasahau wananchi hao, bali inakwenda kwa mipango na bajeti, lakini ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.

“Serikali hii inayoongozwa na dk: Ali Mohamed Shein, inapoahidi inatekeleza, kwa mfano iliahidi huduma zote za kijamii Ngomeni, na sasa hayo tayari,”alieleza.

Afisa Mdhamini wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Pemba Hamad Ahmed Baucha, alisema awali wizara ilikuwa na upungufu wa zana za ujenzi, lakini kwa sasa vimeshanunuliwa.

Alisema wakati ujenzi wa barabara ya Ole –Kengeja ukiendelea, na kwa vile zana za ujenzi sio tatizo, sasa nao ujenzi wa barabara ya Kipapo- Mgelema unaweza kuanza.

Alisema bado azma na ahadi ya serikali ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami, ipo pale pale, na kwa sasa wananchi waendelee kustahamili kidogo.

“Sisi wizara inayoshughulikia ujenzi wa barabara, sasa serikali imeshatununulia zana za kisasa za ujenzi, hivyo hakuna sababu kwa kutoendelea na ujenzi barabara kadhaa kisiwani Pemba ikiwemo ya Kipapo- Mgelema.

Wakati akiifungua barabara ya Kuyuni- Ngomeni yenye urefu wa kilomita 3.2 iliojengwa kwa kiwango cha lami, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi dk: Ali Mohamed Shein aliwaahidi wananchi wa Mgelema kuijenga barabara yao.

Alisema barabara hiyo itaanza kujengwa kuanzia mwaka huu, ambapo pia itaunganishwa na vijiji vya Wambaa na Chumbageni wilaya ya Mkoani ikiwa na kiwango cha lami.

Kwa wakati huo, dk Shein alisema tayari shilingi milioni 700 zimeshatenga na serikali kwa ajili ya kazi hiyo ya ujenzi wa barabara hiyo ya Kipapo- Mgelema.

Barabara ya Kipapo – Mgelema yenye urefu wa kilomita 6, awali iliasisiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania TASAF, kwa ujenzi wa kiwango cha kifusi baina ya mwaka 2001 na mwaka 2003, na sasa Serikali imeahidi kuijenga kwa kiwango cha lami.

Mfuko huo ambao wa kwanza kugharamiwa na Benki ya dunia ulianza mwaka 1987 nchini Bolivia, ingawa kwa Tanzania ulianza mwaka 2000 na kwa Zanzibar utekelezaji wake ulianza mwaka 2001.

Mwisho

PembaToday

Share: