Habari

Miaka 26 ya Chama cha Wananchi – CUF (2)

Julius Mtatiro – Gazeti la Mwananchi
Sunday, June 10, 2018

Jumapili iliyopita tuliona jinsi Chama Cha Wananchi (CUF) kilivyokuwa chachu ye demokrasia Tanzania tangu kinaanzishwa mwaka 1992 hadi kilipofanikiwa kushiriki kwenye harakati za kusaka kuongoza dola kupitia uchaguzi wa mwaka 1995, 2000 na 2005, upande wa Tanzania na Bara.

Jumapili ya leo tutamalizia na kuona ushiriki wa CUF kwenye chaguzi za mwaka 2010 na 2015, viongozi wakuu wa CUF tangu kuanzishwa kwake na itikadi yake.

Mwaka 2010 (Bara)
Katika uchaguzi wa urais wa Tanzania wa mwaka 2010, mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 695,667 (asilimia 8.28), akizidiwa na mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete aliyepata kura 5,276,827 (asilimia 62.83) na mgombea wa Chadema, Dk Willibrod Slaa aliyekuwa na kura 2,271,491 (asilimia 27.05).

Kwa hiyo CUF iliondolewa kwenye nafasi yake ya kushindana na CCM katika kura za urais wa Tanzania.

Mwaka huo 2010 kwenye ubunge, CUF ilipata wabunge 34 ambapo 24 walitokana na majimbo (22 Zanzibar na mawili ya Bara) na wabunge 10 walikuwa viti maalumu.

Kwa wingi wa kura za ubunge CUF ikapigiwa kura 818,122 (asilimia 10.61) ikizidiwa na Chadema iliyopata wabunge 23 wa majimbo na 25 wa Viti maalumu na kura za ubunge 1,839.569 (asilimia 23.86).

CCM ilipata wabunge 186 na viti maalumu 67 pamoja na kura za ubunge 4,641,830 (asilimia 60.20), huku NCCR ikipata wabunge wanne wa kuchaguliwa na kura za ubunge 193,738 (asilimia 2.1), na UDP ikapata mbunge mmoja na kura za ubunge 113,148 (asilimia 1.47).

Mwaka 2010 (Zanzibar)
Uchaguzi wa urais wa Zanzibar wa mwaka 2010 ulikuwa kipimo tosha cha nguvu za CUF kwa upande wa Zanzibar, matokeo yalipotangazwa mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alipata kura 176,338 (asilimia 49.14) na mgombea wa CCM akatangazwa kuwa mshindi kwa kuwa na kura 179,809 (asilimia 50.11).

Pamoja na kutoridhishwa na matokeo hayo, CUF iliamua kuyakubali kwa ajili ya kuheshimu utaratibu mpya wa kikatiba ambao unaruhusu vyama vyote viwili kuwamo serikalini kwa wakati mmoja, kwa hiyo, Maalim Seif Sharif Hamad akateuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Lengo la CUF kukubali hali ya mwaka 2010 ilikuwa kuisaidia Zanzibar kujijengea taratibu mpya za haki katika kushiriki kwenye chaguzi zinazofuatia.

Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, CCM ilipata viti 28 vya uwakilishi (wawakilishi 28 + 8 wa viti maalumu) na CUF viti 22 vya uwakilishi na tisa vya viti maalumu.

Mwaka 2015 (Tanzania)
Katika uchaguzi wa urais wa Tanzania wa mwaka 2015, CUF iliungana na vyama vingine vitatu katika ushirikiano ulioitwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kusimamisha mgombea urais mmoja ambaye alitumia tiketi ya Chadema.

Mgombea huyo, Edward Lowassa alipata kura 6,072,848 (asilimia 39.97) akipitwa na mgombea wa CCM, John Magufuli aliyepata kura 8,882,935 (asilimia 58.46).

Kwa upande wa ubunge, utitiri wa vyama 22 ulisimamisha wagombea nchi nzima. Vyama vilivyoambulia wabunge ni vitano. CUF ilipata wabunge 32 wa kuchaguliwa na 10 wa viti maalumu. Kati ya wabunge wa kuchaguliwa (24 walitoka Zanzibar na kwa mara ya kwanza 10 wakatoka Bara).

Pia, CUF ikapata kura za ubunge 1,257,765 (asilimia 8.63), ikipitwa na Chadema iliyopata wabunge 34 wa kuchaguliwa na 36 wa Viti Maalumu na kura za ubunge 4,627,923 (asilimia 31.75) na CCM iliyopata wabunge 188 wa kuchaguliwa 64 viti maalumu pamoja na kura za ubunge 8,021,427 (asilimia 55.04).

Chama cha ACT Wazalendo kilipata mbunge 1 na kura za wabunge 323,112 (asilimia 2.22) na NCCR Mageuzi ikapata mbunge mmoja na kura za ubunge 218, 2019 (asilimia 1.50).

Mwaka 2015 (Zanzibar)
Uchaguzi wa urais wa Zanzibar wa mwaka 2015 ulifanyika katika mazingira tulivu sana ya kisiasa katika upande huo wa nchi yetu. Washindani wakubwa walikuwa Dk Ali Mohamed Shein wa CCM na Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad wa CUF.

Kura zote za vituoni zilipohesabiwa, mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alieleza kuwa kwa mujibu wa matokeo yaliyokusanywa vituo vyote na kwa mujibu wa fomu ambazo CUF ilikuwa nazo mkononi, yeye (Seif Sharif na CUF) walikuwa wamempita mgombea wa CCM, Dk Shein kwa kura zaidi ya 20,000.

Wakati huo huo kwa upande wa viti vya wawakilishi, CUF ilikuwa imeongoza kwa viti 27 na CCM viti 27. Maalim Seif Sharif akatoa wito kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kumtangaza mshindi halali wa uchaguzi huo na kuacha mbinu za kukwepa kuendelea na utangazaji wa matokeo.

Ghafla, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha akasitisha kumalizia kazi ya kutangaza matokeo na badala yake akatangaza kufuta uchaguzi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, Sheria za Uchaguzi za Zanzibar, Mwenyekiti wa ZEC au Tume nzima ya ZEC haina mamlaka ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa jimbo au ya urais. NEC ikatangaza uchaguzi mpya Machi 20, 2016.

Licha ya wadau wa masuala ya demokrasia ndani na nje ya nchi kutaka kuwe na mazungumzo ya haraka na mabadiliko kuhusu namna ya kusimamia uchaguzi huo CCM ikasisitiza ufanyike chini ya tume ileile na mwenyekiti yuleyule.

CUF ikatangaza kutoshiriki kwenye uchaguzi huo wa marudio ikisema inalenga kulinda misingi ya katiba na haki ya Wazanzibari iliyotokana na maamuzi yao kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.

Viongozi wa Kitaifa
Kikatiba, CUF inao viongozi wakuu wa kitaifa wanaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa Taifa kila baada ya miaka mitano.
Viongozi hao ni Mwenyekiti Taifa, Makamu Mwenyekiti Taifa na Katibu Mkuu.

Katika Ofisi ya Mwenyekiti Taifa, viongozi wa CUF waliowahi kuhudumu humo ni; James Mapalala (1992 – 1994), Marehemu Musobi Mageni (1994 1999), Ibrahim Lipumba (1999 – Agosti 2015) na wenyeviti wa kamati ya uongozi Twaha Taslima (Agosti 2015 – Juni 2016) na Julius Mtatiro (Agosti 2016 na kuendelea).

Japokuwa, Profesa Lipumba ameendelea kutambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa kama mwenyekiti, CUF pamoja na vikao vyake havimtambui mwenyekiti huyo kutokana na kujiuzulu kwake, hali iliyopelekea kuwepo kwa kesi kadhaa mahakamani.

Kwa upande wa Ofisi ya Makamu Mwenyekiti wa Taifa, waliowahi kuhudumu kwenye ofisi hiyo ni wafuatao, Maalim Seif Sharif Hamad (1992 – 1999), Shaabani Khamis Mloo (1999 – 2004), Machano Khamis Ali (2004 – 2014) na Juma Duni Haji (2014 – Agosti 2015). Kwa sasa ofisi ya makamu mwenyekiti haina kiongozi.

Tangu Chama cha Wananchi CUF kianzishwe kimewahi kuhudumiwa na Makatibu Wakuu wawili, Marehemu Shaabani Khamis Mloo (1992 – 1999) na Maalim Seif Sharif Hamad (1999 – hadi leo).

Pia, wapo viongozi waandamizi wa kitaifa ambao wanachaguliwa/kuteuliwa na viongozi wakuu wa kitaifa na kuthibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambao ni naibu makatibu wakuu wawili, wakurugenzi wa kitaifa na wengineo.

Itikadi ya Chama
Chama Cha Wananchi (CUF) kinafuata itikadi, misingi na imani ya uliberali ambao umefafanuliwa kwenye tamko la pamoja la Ilani ya Uliberali wa Kiafrika (African Liberal Manifesto) lililoazimiwa, kuungwa mkono na kuthibitishwa mjini Addis Ababa Ethiopia (mwaka 2012) na vyama vya Kiliberali vya Kiafrika vilivyomo kwenye Mtandao wa Uliberali Barani Afrika.

Katika misingi ya Uliberali wa Kiafrika, CUF inaamini na inasimamia uhuru wa mtu binafsi, uhuru wa taasisi huru za kisiasa, kiraia na kidini na kwamba utendaji na uhuru wa taasisi hizo haupaswi kuingiliwa na serikali huku suala la demokrasia shirikishi likiwa msingi wa ufanyaji maamuzi katika jamii.

CUF inaamini na kusimamia falsafa na misingi ya usawa wa watu wote na haki zote za kiraia. Salamu na “motto” wa CUF ni “Haki sawa kwa wote” ikiwa na maana ya kupigania haki zote za raia kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

CUF inasimamia sera ya uchumi huria kama unavyofafanuliwa na tunu za uliberali, uchumi ambao unamwezesha kila mwananchi kujibidiisha na kutoa mchango wake mkubwa kwenye uzalishaji na ukuzaji wa uchumi wa nchi bila kuwekewa vikwazo na serikali au mifumo iliyopo.

Katika uliberali, CUF inaamini katika uwepo wa serikali ya kidemokrasia na yenye mamlaka ya kadri yalivyofungamanishwa na kudhitibiwa na Katiba ya nchi, utawala wa sheria na mgawanyo wa madaraka kati ya Serikali, Bunge na Mahakama.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa mfuatiliaji wa utendaji wa Serikali barani Afrika; ni mtafiti, mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF. Simu; +255787536759 (WhatApp, Meseji na Kupiga)/ Barua Pepe; juliusmtatiro@yahoo.com)

Share: