Habari

Miaka 46 Zanzibar bila Sh Karume: Mema, mazuri yake yaendelezwa

Miaka 46 Zanzibar bila Karume
Mema, mazuri yake yaendelezwa

NA MWANDISHI WETU

WANANCHI wa Zanzibar na watanzania, leo wanaadhimisha miaka 46 tangu kipenzi chao, Rais wa Chama cha Afro Shirazi Party (A.S.P) na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume alipouawa.

Sheikh Abeid Amani Karume, ni kiongozi wa kipekee aliyewahi kutokea visiwani Zanzibar na anakumbukwa kutokana na ujasiri wake wa kuongoza mapinduzi matukufu ya Januari 12, mwaka 1964.

Akiwa na ndoto za kustawisha uchumi wa na maisha ya wazanzibari, ghafla bila ya hata kutegemea Aprili 7 mwaka 1972, wapinga maendeleo kwa chuki zao binafsi walikamilisha njama za mauaji ndani ya Ofisi za CCM hapo Kisiwandui.

Hivi karibuni akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein alisema kuwa mzee Karume ana heshima ya kipekee.

“Marehemu mzee Abeid Amani Karume ana heshima ya pekee kwa Zanzibar na kwa Tanzania nzima kwa jumla”,alisema Dk. Shein wakati akizungumza na Mwenyekiti huyo, Prof. Mark Mwandosya.

Dk. Shein aliongeza kuwa katika uhai wake mzee Karume alikuwa na dira na ndio maana aliweza kufanya mambo mengi makubwa ambayo yataendelea kukumbukwa kutokana na umuhimu wake.

Alisema kuwa aliweza kusimamia Mapinduzi matukufu ya Januari 12, 1964 ambayo yamewakomboa wazanzibari na kuwatoa katika unyonge na hatimae kuondosha ubaguzi wa aina zote baada ya kuingia madarakani.

Alisema kufanyika kwa Mapinduzi ni jitihada za mzee Karume na viongozi wenzake ambapo jitihada hizo zinafaa kuenziwa pamoja na kutunzwa na kudumishwa ili na vizazi vijavyo viweze kuzifahamu.

Dk. Shein alisema marehemu Mzee Karume na marehemu Julius Kambarage Nyerere waliziunganisha Tanganyika na Zanzibar mnamo Aprili 26 mwaka 1964 na hadi hivi sasa muungano huo umeweza kujijengea sifa kubwa.

Kwa upande wake mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na waziri asiye na wizara maalum, Said Soud Said akizungumza na gazeti, hili alisema mzee Karume si wa kuenziwa kila mwaka, bali ni shujaa wa kukumbukwa na kuenziwa kila siku.

Said Soud kutoka chama cha siasa cha wakulima AFP, alisema moja ya faida kubwa za mapinduzi yaliyoongozwa na mzee Karume ni kuwawezesha Wazanzibari kupata uhuru wao unaowawezesha kujiamulia mambo yao.

“Falsafa ya Mapinduzi ya mwaka 1964, ilikuwa kujikomboa kutoka kwa wakoloni, kutakakowawezesha wananchi wa Zanzibar kujiamulia mustakbali wao bila ya kuingiliwa kwa njia yoyote”,alisema Soud.

Aidha alisema dhamira za mapinduzi zimekuwa zikiendelezwa kwa kila awamu ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hasa ikizingatiwa kuwa huduma muhimu za kijamii kama vile elimu, afya zimekuwa ikitolewa bure kwa wananchi.

“Wanaobeza hatuwashangai kwa sababu hawaelewi maana ya kujitawala, lakini pia wanapaswa wajiulize kama wangekuwa mpaka leo wako kwenye ukoloni wangeweza kujiamulia mambo yao?”,alihoji waziri huyo.

Naye mjane wa mzee Karume, mama Fatma Karume, akizungumza na gazeti hili hivi karibuni huko nyumbani kwake Kilimani mjini Zanzibar, aliomba jitihada zaidi zichukuliwe ili kuanzishwe kumbukumbu maalum ya mzee Karume.

Alisema kwa kufanya hivyo kutatoa nafasi kwa kizazi cha sasa na kijacho kufahamu na kupata elimu maalum ya mambo mengi kuhusu mzee Karume hali ambayo itawaepushia kudanganywa na kuutambua ukweli.

Alisema familia yake ina vitu vingi ilivyovihifadhi ambavyo itakuwa vyema kama kutakuwa na jengo maalum ili vitu hivyo vikawekwe hali ambayo itakuwa kielelezo cha kukumbukwa na kuenziwa kwa vitendo kiongozi huyo.

“Wanangu hapa nna vitu vingi vinaweza kuwekwa kwenye eneo litakalotengwa kuwa kumbusho la mzee Karume, hivi sasa baadhi ya vitu hivyo vinaanza kuharibika”, alisema mama Fatma.

Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili, walisema kuwa ndoto za kiongozi huyo katika kustawisha maisha ya wananchi wa Zanzibar hazikutimia kwani alikuwa na mambo makubwa ambayo kama angeweza kuyatekeleza yote Zanzibar leo ingekuwa kama nchi nyengine yoyote barani Ulaya.

Mmoja wa wananchi hao Haji Mcha Mlenge (78), mkaazi wa Marumbi wilaya ya Kati Unguja, anasema alimfahamu vyema mzee Karume kwani mara kwa mara alikuwa akitembelea vijiji vya wilaya hiyo.

Mlenge anasema kuwa anamfahamu mzee Karume sio kwa kuhadithiwa, bali amemuona kwa macho yake siku ambayo aliitisha mkutano ambapo alieleza dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wa vijijini wanaishi kwenye nyumba za kisasa.

Aidha mzee huyo alisema Sheikh Karume katika mkutano huo alielezea ndoto zake nyingi za kustawisha maisha ya wananchi wa Zanzibar ikiwemo kuwasaidia wavuvi wa wilaya ya Kati.

Naye Khamis Zahor Ali mkaazi wa Mikunguni mjini Zanzibar, alisema wakati wa mzee Karume jamii ilikuwa ikiitkia wito wa kujitolea lakini hivi sasa wito huo haupo na umepotea kabisa.

Kuhusu siasa alisema alikataza vyama ili awaunganishe wananchi wa Zanzibar na kuepuka migawanyo na mifarakano kama iliyokuwepo wakati Zanzibar ikiongozwa na Sultani.

Zanzibarleo

Share: