Habari

MIAKA 50 YA MAPINDUZI NA NYUFA ZA NUSU KARNE.

Tokea kuanza kwa mwaka huu 2013 hapa Zanzibar hazipiti dakika kumi katika vyombo vya habari utasikia kila aina ya misherehesho kwa kutimiza miaka 50 ya mapinduzi. Kwa hakika si jambo baya hata kidogo kufanya hivyo kwa kukumbuka tukio hili kutokea na kutimiza nusu karne sasa.

Kumekuwa na utiwaji chumvi nyingi kupita kiasi na watu kuaminishwa kwamba mapinduzi yamekombowa Wazanzibari kwa hali ya juu kabisa. Mara zote sherehe za mapinduzi hutumiwa kisiasa kwa watu kujikweza na kufanya kila aina ya vitisho hasa katika kipindi hiki cha vyama vingi.Kusherehekea ni jambo zuri ikiwa tutatathmini mambo kwa kila upande wa shilingi na kila kitu kukipa haki yake. Kuanzia hapo mimi naona sherehe za miaka hamsini tunaangalia upande mmoja tu ama kwa makusudi kwa kusifu na tumeacha kujadili hasa malengo ya mapinduzi.

Ukweli wa mambo ni kwamba mapinduzi kwa ujumla yameleta maendeleo kwa kiasi na kuwapa fursa wale ambao hawakupata fursa hio hapo kabla ukilinganisha na wakati huo. Hapa kwangu mimi situmii neno WENGI ambao walinyimwa kwa sababu hadi leo hii bado wanaopata fursa ni wachache kwa kujuwana na kupendeleana kama ilivyokuwa kabla ya mapinduzi kilichobadilika ni rangi za watu tu na miaka, huko tuwache .

Hapa tuangalie hii miaka 50 na nyufa za nusu karne ambazo watu wengi hawaziangalii ama hawataki kwa makusudi kuzitaja na kuzipangia mikakati ya kuziziba. Si viongozi wa serikali yenyewe ya mapinduzi, si wana zuoni na wanataaluma na jamii. Zimesahaulika kabisa.

Kwanza kuna ufa mkuu wa utengamano wa kijamii- jamii ya kizanzibari bado imegubikwa na wingu zito la utengano uliojificha. Tatizo hili limesababishwa na historia yenyewe ya Mapinduzi kutokana na ukweli kwamba watu na mali nyingi zilipotea wakati wa mapinduzi na baada ya mapinduzi. Kadhia hii iliwagusa wanafamilia mbali mbali wa kizanzibari ambao leo hii wajukuu wao inakuwa ni miongoni mwa kizazi cha Zanzibar ya leo na wanashiriki kuchangia maendeleo ya zanzibar. Mapinduzi yalilindwa kwa kuwatenga baadhi ya watu na kuwaona kuwa ni maadui wa mapinduzi licha ya ukweli kuwa ni wazanzibari.Si hao tu bali hata wale walioonekana kuwa karibu na watu wanaohisiwa wanapinga mapinduzi. Mapinduzi kwa miaka 50 yameshindwa kuziba ufa huu ambao KINADHARIA unaonekana haupo lakini kivitendo umedumu kwa nusu karne sasa.Kuna watu hubisha kwamba vyovyote iwavyo mapinduzi yalipinduwa serikali halali ya wananchi wa Zanzibar.Mitafaruku ya siasa ndiyo iliyazaa fikra za kuunga mkono mapinduzi ambapo kwa wengine yalikuwa ni muhimu kutokea na kwa wengine hayakufaa kutokea na pangetafutwa namna nyengine ya uhalali wa mambo.Ikumbukwe kwamba HAWA WOTE NI WAZANZIBARI AMA WA KUZALIWA au wa KUANDIKISHWA.
Katika jamii kuna makundi makubwa mawili na watawala hukataa kutambuwa ukweli huu.
Kuna wale wanaoungamkono na wanaopinga kwa sababu yalipoteza roho za wazanzibari wenzao. Ufa huu haujapatiwa dawa na badala yake unaendelezwa. Hakuna SULUHU YA KITAIFA na imelazimisha WATU kukataa hata uhuru wao wa KIMATAIFA wa Disemba1963. Si lengine ni huu ufa tu.

Ingukuwa viongozi wangu watanisikia ningewaambia SASA WAKATI UMEFIKA KUWE NA MJADALA WA KITAIFA na MARIDHIANO baada ya miaka 50 ya MAPINDUZI KUHUSU DHANA YA ZANZIBAR MPYA YA MAELEWANO- hili suala la Mapinduzi liwe mjadala.

Vile vile kuna ufa wa kutengenezwa wa kimaeneo hasa kutokana na mitaji ya kisiasa kwa maslahi ya ubinafsi na uhafidhina uliochupa mipaka.Kuna watu hawaridhiki ila waone Unguja na Pemba zinatengana. hapa wanahisiwa ni watu wa nje ya Zanzibar na wasaliti wachache. Ubaya wa mambo SMZ yenyewe imo katika mkakati huo kwa zaidi ya awamu 6 za uongozi. Hawakuona umuhimu wa kuweka sera za kitaifa za utengamano na kuziba kila aina ya nyufa. Hatima yake wale wabaya ndio hutumia mwanya huo kuendeleza mabaya. Na mpaka sasa kuna watu wanafanya haya na wala hawaulizwi lolote na mamlaka.

Kukosekana kwa uzalendo wa dhati nalo ni pigo lengine wakati huu wa miaka 50. Mitaala yetu imekuwa dhaifu na tumekosa ile spirit hasa ya uzalendo kama nchi. Hakuna dira ya Uzalendo kwa maslahi ya Zanzibar. viongozi wanaogelea katika uzalendo wa kivyama na kuacha uzalendo wa nchi. jambo hili limeiodhoofisha Zanzibar kwa nusu karne. Tazama kila aliye pambana kuinasuwa Zanzibar alidhibitiwa kwa visingizio kadhaa na mifano ipo.Fikiria Zanzibar kukosa kutoa nafasi ya umakamo wa Rais kama ilivyokuwa hapo awali na ukawaona wabunge wanaunga mkono hili basi ni ishara tosha ya kukosa UZALENDO WA NCHI. Yote haya yanaendelea kufanyika mpaka sasa katika hii miaka 50 ya Mapinduzi watu bado wamelala ndio kwanza DAIMA.

Zanzibar imekosa nguvu za kujiamulia mambo yake na imepoteza mamlaka yake. Ikumbukwe jambo hili lilikuwa kilio hapo kabla ya mapinduzi na waasisi wa mapinduzi hawakusita kulisemea lakini leo wapi?. Hakuna mtawala anaejali na huandamwa yule anyehoji na kutafutiwa namna ya kupotezwa.

Aidha kuna suala la umasikini, ufisadi na kukosekana HAKI MIONGONI MWA JAMII.Mikakati imefeli.

Kwa kumalizia NASHAURI kwa wahusika.
.Wakati tunasherehekea miaka 50,tufikirie kuja na ajenda ya Zanzibar mpya yenye utengamano halisi na kuja zama mpya za mshikamano TUSIOGOPE MIJADALA YA KITAIFA kwa mambo yenye sintofahamu iwe ya kisiasa, kijamii na kidini au yoyote ile.

. Turejeshe masomo ya kizalendo kwa kutengeneza mitaala na kuwafinyanga vijana upya katika muktadha wa kizalendo na kuziba nyufa zote za usaliti, ufisadi na mitengano.

TUNAHITAJI ZANZIBAR MPYA.

Share: