Habari

Micheweni kukosa maji ya ZAWA kwa muda usiojulikana

IMEANDIKWA NA MASANJA MABULA (na hisani ya mitandao),

WANANCHI zaidi ya 120,000 wa shehia za Maziwang’ombe, Shanake na Kiuyu Mbuyuni wilaya ya Micheweni Pemba, huwenda wakakosa huduma ya maji safi na salama kwa muda usiojulikana, baada ya bomba na nchi nne linalopeleka maji katika shehia hizo kukatika.

Aidha taasisi za Serikali na Binafsi ikiwemo chuo cha uwalimu Micheweni-CCK- pamoja na kituo cha Redio Jamii Michweni ni miongoni mwa taasisi ambazo zitakumbwa na kadhia hiyo.

Bomba hilo linalotoa maji kutoka kwenye kisima cha Kironjwe kilichopo Kilindini, limekatika huku sababu ni wachimbaji wa mawe ambao waliochmba hadi chini ya bomba hilo.

Akizungumza katika eneo la tukio, Afisa wa Mamlaka ya Maji –ZAWA -Wilaya hiyo Ali Rajab amesema Mamlaka kwa kushirkiana na vyombo vya ulinzi, wanaendelea kumtafuta kijana aliekuwa akichimba mawe katika eneo hilo.

Alisema kutokana na athari hiyo, wananchi wa shehia hizo wanapaswa kuwa wastahamilivu wakati Mamlaka inaendelea na utaratibu wa kuirejesha huduma hiyo.

“Kutokana na tatizo hili, wakaazi wa shehia hizi tatu watakosa huduma ya maji safi na salama, kwa muda usiojulikana, lakini ZAWA tunawaomba wawe wavumilivu,”alisema.

Aidha aliongeza kuwa kijana aliyehusika na uchimbaji wa mawe karibu na bomba , akipatikana atawajibika kulipia gharama zote za matengenezo,’alifahamisha.

Mmoja wa wananchi amesema kwamba wachimbaji wa mawe wanapaswa kuheshimu njia zinazopitiwa na miundombinu ikiwemo maji ,umeme na barabara, ili kuepuka athari ambazo zinaweza kujitokeza.

Amesema iwapo wachimbaji wa mawe watazingatia uwepo wa miundo mbinu itasaidia kuifanya idumu kwa muda mrefu.

Naye Meneja wa Kituo ch Redio Jamii Ali Massoud Kombo ambacho nacho kitakumbwa na tatizo hilo, ameiomba Mamlaka ya Maji –ZAWA- kutoa elimu kwa wananchi hususani wachimbaji wa mawe juu ya kuilinda miundo mbinu.

‘ZAWA wanalojukumu la kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuilinda miundo mbinu ya maji , kwani hii itasababisha hasara kubwa kwa Mamlaka wakati wangetumia gharama kidogo utoa elimu’alisisitiza.

Aisha Hassan Haji na Patima Makame Kombo wa Michweni walisema sasa wanaelekea kutumia maji ya kuokota, hadi hapo ZAWA itakapotengeneza baomba hilo.

Nae Saumu Hassan Haji alisema, kwanza ZAWA ishughulikie matengenezo ya bomba hilo, na kasha ndio wamtafute alieharibu miundo mbinu ya maji.

“Mimi hofu yangu, sasa sisi wananchi wa shehia tatu tutanyemelewa na matumbo ya kuharisha, maana maji ya ZAWA yalikuwa yameshatibiwa, lakini maji tunayoelekea kutumia sio salama,’’alieleza.

Hata hivyo mtaalamu mmoja wa afya ambae alisema sio msemaji wa wilaya hiyo, aliwataka wananchi kuendelea kuchemsha maji hasa katika kipindi hichi.

“Kukatika kwa bomba ni sababu, lakini suala la kuchemsha maji na kunawa kwa sabuni kila unapotoka chooni, liwe endelevu ili kujikiga na magonjwa,”alieleza.

Disemba 11, mwaka 2017 Mkuu wa wilaya ya Micheweni Salama Mbarouk Khatib, aliwataka wananchi wa wilaya hiyo, kuendelea kujikinga na maradhi ya mripuko ikiwemo kipindu pindu, kwa kufanya usafi katika maeneo yao.

Bomba hiyo imekatika baada ya wananchi kuchimba mawe karibu na njia yake na hivyo kusababisha athari kwa wakaazi wa shehiya hizo.

Mwisho.

PembaToday

Share: