Habari

Mihimili ya nchi inavyotia kichef-chefu

Mwandishi Maalum

Jumapili, Julai 30, 2017

MWISHONI MWA WIKI ILIYOPITA kuanzia Jumatatu, tarehe 24/7/2017 hadi juzi Alhamisi, tarehe 27/7/2017 tumeshuhudia vioja na vituko vya hali ya juu vya Bunge la Tanzania na Tume ya Uchaguzi (NEC). Hizo ni taasisi kubwa na muhimu za umma.

Bunge katika nchi nyingine za dunia na hasa kwa nchi zilizoendelea ndiyo moyo wa taifa. Bunge ndiyo lenye maamuzi yanayoweza kutekelezwa na serikali. Maamuzi mengi ya bunge ni yale yanayo zingatia maslahi ya wananchi wake.

Bunge, linafanyakazi kuisimamia serikali ili utendaji wake uendane na matakwa ya wananchi na mahitaji yao, uendane katika kusimamia haki na maslahi ya wananchi wake kwa ufanisi.

Bunge si chombo kinachopaswa kujiingiza katika itikadi za kisiasa na kukuza migogoro katika jamii. Bunge linapaswa kuitwa bunge, bunge halipaswi kufanana na chama cha siasa. Bunge ni la wananchi wote.

Bunge linaloingilia migogoro ya taasisi za kiraia na kuwa kiini cha migogoro hiyo, hilo ni bunge lililokosa maadili, lilikosa nidhamu na halipaswi kuheshimiwa na wananchi kwa sababu limejivunjia heshima na kukosa hadhi ya kuitwa bunge.

Kama nilivyosema, kuwa bunge kwa baadhi ya nchi na hasa nchi zilizoendelea ndiyo muhimili mkuu unaotegemewa na wananchi wake katika kutoa maamuzi sahihi, yasiyokuwa kuwa na doa au kasoro ndani ya jamii.

Bunge limepewa ridhaa na wananchi kuwa chombo pekee cha kutunga sheria za nchi. Mahakama, muhimili mwingine wa nchi kazi yake kubwa ni kutafsiri sheria na kutoa haki kwa wananchi.

Bunge, kama chombo kikuu cha uwakilishi wa wananchi kinapokuwa na mambo ya ovyo ovyo, na kuanza kusikiliza na kutekeleza amri za muhimili mwingine kwa hofu ya spika kuogopa KUTUMBULIWA au kwa utashi wa kisiasa, ni hatari sana kwa jamii.

Spika wa ovyo, anaendesha bunge atakavyo, anabariki maamuzi ya ovyo ovyo bila kuangalia athari zake kwa jamii na analivunjia bunge heshima yake.

Bunge likiwa madhubuti, makini na imara, mihimili mingine ya nchi haiweze kufanyakazi kwa upendeleo na uonevu au kuyumbisha taasisi nyingine za wananchi kwa sababu taasisi hizo zimeundwa kutokana na sheria zilizotungwa na bunge.

Ili Bunge liheshimiwe na kuaminiwa na wananchi, lazima mfumo wa utendaji wa bunge uwe makini, hasa katika maamuzi yanayogusa maslahi ya wananchi. Spika wake anatakiwa kuwa ‘neutral’.

Bunge likianza kuhofia/kuogopa muhimili mwingine wa nchi na kuanza kupokea amri kutoka muhimili huo, bunge hilo ni hatari ya kuipeleka nchi mrama. Inawezekana hata kuitumbukiza nchi katika machafuko ya raia wenyewe kwa wenyewe.

Siku chache zilizopita nilimsikia Edward Lowassa, akiishangaa Tanzania, kuwa nchi ambayo imekuwa huru kwa miaka zaidi ya 50, lakini bado watawala wanakasumba za kuwaonea/kuwatesa raia, kana kwamba nchi imepata uhuru jana.

Lowassa (waziri mkuu wa zamani) aligusia hoja hiyo ya unyanyasaji na uonevu wa raia unaofanywa na serikali kutokana suala la Masheikh wa Jumuiya ya Uamsho, ambao wamekuwa mahabusi kwa muda mrefu.

Lowassa, anashangaa kwamba miaka 50 tangu nchi kupata uhuru, lakini bado unatokea utawala unasimamia mateso ya wananchi wake. Ni dhambi kubwa iliyopitiliza kiwango katika utawala wa sheria.

Naandika kwa uhakika kabisa, kwamba kwa asilimia kubwa sana ya watanzania hawana imani na mfumo wa bunge jinsi linavyoendesha shghuli zake.

Kadhalika, naamini kuwa wananchi, kwa asilimia kubwa hawana imani kabisa na Rais John Magufuli na utendaji wa serikali. Kama alivyosema Tundu Lissu: “Tanzania ina rais wa ajabu haijapata kutokea.”

John Pombe Magufuli (mtumbua majipu – hapa kazi tu), anatushangaza sana kuhusu utendaji wake, anaonekana kama ni kiongozi wa nchi aliyekosa dira. Haeleweki anafanya nini na anataka nini!.

Juzi, kama wiki moja iliyopita akiwa Kigoma, alimmwagia sifa nyingi David Kafulila (CHADEMA), kutokana na kuibua ufisadi wa serikali (escrow) katika bunge na serikali ya awamu ya 4.

Magufuli, kwa jinsi alivyopoteza mwelekeo wa uongozi na kwa jinsi alivyokuwa hana hekma/hana busara katika kauli yake kadamnasi alifikia hatua ya kumwita Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani, Jaji Stephen Warema, kuwa ni tumbili.

Hoja hapa, Jaji Warema alikuwa anaitetea serikali ya wakati huo, ambayo yeye (Magufuli), alikuwa pia ni kiongozi katika serikali hiyo hiyo, tena waziri. Hapa ndipo tunapomuona Magufuli, haeleweki anataka nini!.

Magufuli, kama kweli alikuwa hapendi ufisadi, ni kwanini hakulisema hilo ndani ya bunge la wakati huo, ilhali yeye akiwa pia ni kiongozi wa juu wa serikali. Alibaki hadi mwisho wa serikali ya awamu ya 4, ilipomaliza muda wake, bila kupaza sauti yake kuhusu ‘escrow’.

Magufuli, eti leo anajitokeza katika hadhara ya wananchi wa Kigoma, na watanzania anamsifia Kafulila kwa kuibua ufisadi, kama si unafiki ni kitu gani?.

Hivyo, Magufuli kwa kumsifu Kafulila, anadhani kwa akili yake tunaweza kumuamini, hatumuamini ng’oo tunajuwa anatafuta kiki kwa wananchi aonekana hapendelei (neutral). Anataka kuwaaminisha wananchi kwamba hayumo kwa yaliyotokea bungeni akiwa waziri awamu ya 4.

Kwa ufupi, Magufuli si mtetezi wa haki za wanyonge, ni kiongozi hatari ambaye anaweza kuisababishi nchi nakama na majanga, iwapo hatua za mapema za kumdhibiti hazitachukuliwa.

Benjamin Mkapa kwa viongozi wa Tanzania, peke yake ndiye aliyesababisha  maafa makubwa ya raia kule Zanzibar, kwa utashi na chuki za kisiasa. Mwenyewe (Mkapa) alikiri hilo, akiwa nchini Marekani, siku chache kabla ya kuwacha madaraka.

Lakini, Magufuli kajaa ‘undumi-wa-kuili’. Matatizo yote yanayo kikumba CUF hivi sasa yana mkono wake. Si Msajili wa vyama, si RITA, si Ofisi ya Spika wala si hao Polisi na Usalama wa Taifa.

Iweje, asifie ushujaa wa David Kafulila, lakini anabariki dhulma na ufisadi unaofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa, RITA, Spika wa Bunge na Tume ya Uchaguzi, kuhusu Lipumba kuwafukuza wabunge wanane wa CUF. Lipumba si mwanacham, wala si kiongozi wa CUF.

Mimi nasema bila kiwewe kuwa mgogoro wa CUF umetengenezwa na Magufuli na wenzake, hata mtoto aliyezaliwa leo anajuwa. Lipumba ni mtatago tu, kuwa ni sababu ya kuifanya CUF, kutumbukia kwenye janga.

Tangu bunge lionekane kuwa na sura ya mfumo wa vyama vingi, haijawahi kutokea vituko na vioja vinavyo fanywa mwaka huu na taasisi muhimu za umma ndani ya wiki mmoja, kama Magufuli hahusiki.

Wabunge wamekuwa wakifukuzwa na vyama vyao na bunge hupuuza kuzingatia uamuzi wa kuwavua ubunge. Maalim Seif, kasema juzi, kuwa haijapata kutokea ni “super sonic speed.”

Jumatatu, wiki iliyopita, tarehe 24/7/2017 Lipumba na Sakaya walimuandikia Spika wa Bunge kumjulisha kuwa “Baraza Kuu la CUF” (baraza feki) limewafukuza uanachama wabunge wanane wa CUF, Viti Maalum.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alimuandikia Spika wa Bunge, Job Ndugai kumjuilisha kuwa Baraza Kuu la CUF (Baraza Halali) lilichaguliwa mwaka 2014 na muda wake utamalizika mwaka 2019 na baraza hilo halali ndilo lililomfukuza Lipumba.

Siku iliyofuata Jumanne, tarehe 25/7/2017 Ofisi ya Bunge ilitoa taarifa kwa umma kwamba imepokea maelekezo kutoka kwa Sakaya na Lipumba kuwa wabunge hao wanane si wanachama wa CUF, na ofisi hiyo inatafakari hatua za kuchukua.

Jumatano, tarehe 26/7/2017 Ofisi ya Bunge ilitoa uamuzi wake, kwamba imekubaliana na maelekezo ya Lipumba na Sakaya na kuwa imewavua wabunge hao, ubunge wa viti maalumu.

Pia, Ofisi ya Bunge ilisema kuwa tayari imeiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuijuilisha kuchukua hatua kujaza nafasi hizo zilizo wachwa wazi.

Jumatano, hiyo hiyo jioni, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nayo, ikaridhia na kutoa agizo kuandaliwa kwa uteuzi wa wabunge wapya kwa kushirikiana na Lipumba.

Aidha, Alhamisi, tarehe 27/7/2017 mapema asubuhi Tume ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza wabunge wapya wa Lipumba. Kitu ambacho hakijawahi kutokea. ‘super sonic speed’

Magufuli atambue, kuwa ubaya unapofanywa na kiongozi wa nchi matokeo yake ni mabaya na dhambi yake haifutiki hata kwa kutumia raba ya moto. Hilo Magufuli, atambue.

Magufuli, akitaka kujifunza nadharia ya ubaya kuwa inamuondolea muhusika ubinadamu na unyenyekevu kwa wenzake, na hatimaye kuwa na tabia kama ya mnyama, asome kutoka kwa Benjamin Mkapa.

Mkapa, ambaye hadi leo hadiriki kuwa na kauli nzuri za kistaarabu na kiungwana kila anapopanda jukwaani, kauli zake ni zile zile za matusi dhidi ya wananchi. Hiyo ni ishara ya mtu aliye-laanika.

Mwenyezi Mungu, keshampiga chapa ya laana, hatamzindua na kumtanabahisha, mpaka ataondoka duniani, kauli zake zitabaki kuwa za matusi, kuwaita watu malofa na wapumbavu.

Imekatazwa sana katika uislamu, kumtukana mtu asiyekutukana, kumsengenya mtu, kudhulumu haki za watu za aina yoyote, iwe mali, kazi, madaraka na kadhalika.

Watu wa kawaida hapaswi kudhulumiana seuze kiongozi wa nchi anapo wadhulumu raia haki zao na anafanya hivyo katika hali ya jeuri na kejeli kwa sababu analindwa na vikose vya ulinzi.

Wanasahau kuwa vikosi vya ulinzi ni mtihani wa dunia. Allah, akiamrisha MALAIKA wake kwenda kuchukua amana yake ya uhai, mauti hayana kikosi cha ulinzi.

Tunawaomba WATAWALA wetu kwa unyenyekevu mkubwa wajirekebishe. Tunawanasihi na kuwasihi kuwa waache jeuri, kiburi na dhulma. Tunawakumbusha kuwa kuna akhera, kuna hesabu na malipo. Vile vile kuna Pepo na MOTO..

 

 

Tagsslider
Share: