Habari

Mitandao ya kijamii yamkomsesha usingizi Mtawala

Na Mzee Kondo

Mitandao ya kijamii inamkosesha usingizi mtawala/mkoloni wa visiwa vya Zanzibar, ambae pia ni rais wa ajabu wa Tanganyika. Bwana Magufuli ameonyesha wazi kuyathibiti magazeti ya Tanganyika ambayo hayamsifii anavyotaka, huyu hakuanza leo kutafuta sifa magazetini. Kumbukeni uchapa kazi wake ulionekana pale tu, alipokuwa hafanyi kazi yake bila kuwaita waandishi wa habari, kila alipokuwa akifungua barabara, akijenga madaraja, akiendesha matrekta, vichwa vya treni nk.

Aliwatumia waandishi na vyombo vyao kiasi cha kutosha, kwa msaada huo ndio hii leo akaweza kuitwa RAIS na kuikalia ikulu huku akitoa jeuri, kuwa yeye peke yake ndie aliyechukua fomu ya kugombea hakuna aliyemsaidia, sijui wale aliokuwa akigombea nao urais kwa tiketi ya ccm, walisaidiwa na wake zao laa. Rais huyu kasahau kuwa alipewa kura na wanachi, uchukuaji wake kura ilikuwa ni jukumu lake peke yake sasa anataka kumlaumu nani? Mbona alipopiga zile “push-ups” alizipiga peke yake na hakutumwa na mtu?

Mimi leo nimeikumbuka riwaya fupi niliwahi kutolewa na mzee mmoja wa kiarabu hapa kwetu, alinihadithia wakati nikiwa kijana mbichi, aliniambia kuwa yeye alipata misukosuko mingi kama walivyopata jamii ya watu wenye asili kama yake hapa kwetu baada ya mapinduzi, aliniambia kuna siku aliitwa kwa Mzee Karume kujibu mashitaka ya uongo, kwa bahati nzuri Mzee Karume aliuona ukweli na anamjua kwa jina.

Karume aliamrisha mheshimiwa aliyeleta mashtaka aje ikulu haraka, na aliwasili kama alivyoamriwa, baada ya kusikiliza pande zote mbili, ndio akatoa maamuzi ya haki na akamwambia aendelee na kazi yake na asihofu kitu. Kabla hajaaga, alimwambia Karume kuwa huyu mheshimiwa aliyekuja kunishtaki, na yeye yupo hapa leo, mnatuonea sisi, sisi mkitumaliza, mtageukiana wenyewe kwa wenyewe, na mtamalizana, akamaliza na akaaga kwa heshima zote na akaenda zake.

Nape Nauye, yamemkuta yale aliyosema mzee wa kiarabu. Sio siri tena sasa na wala tusingeshangaa kama Nape angelikuwa mbunge wa chama chochote cha upinzani, hao siku hizi wanalala jela kama nyumba ndogo, wameshazowea kuonewa na kufunguliwa kesi/mashtaka ya kusingiziwa, ili muradi waende jela, Wabunge wa chama cha mapinduzi walikaa kimya wakidhani wao wako salama, sasa rais na serekali yake wameanza kuwageukia na wao. Kwa nini sisi tuwaonee huruma wakati wao ndio waliotayarisha huu mfumo mzima wa kuwathibiti wenzao.

Rais wa Tanganyika leo ametoa kauli ya kukasirishwa na magazeti ya huko kuweka picha hadharani ya tukio la kutolewa bastola Nape,alichokuwa anataka yeye hili tukio iwe SIRI nadhani,na ameahidi kuwachukulia hatua wana habari hao na vyombo vyao ikiwa wataedelea na utoaji habari wa namna hii,huyu Rais hajui wala hajasomea taaluma ya habari,kwa maana hiyo anajiropokea tu, kama ilivyo desturi yake, kwa sababu hajui sheria wala miiko ya fani yenyewe.

Huwezi kuwakataza kuliweka kurasa yoyote mkasa huu uliomtokea Nape, au kuweka picha ya aliyemshikia bastola Nape, polisi na wizara ya mambo ya ndani wametoa matamko kuwa wanaanza na uchunguzi wa kumbaini huyu kijana ni nani aliyetoa bastola? Wanazidanganya nafsi zao kuwa sasa hawamtambui tena, na hawajamtuma, wananchi tunatakiwa tufikirie kuwa huyu ni jambazi tu, kama ni hivyo, mbona aliletwa na gari la polisi,siku hizi majambazi hukodisha au kuazima madefender ya polisi kwa kazi zao?

Kwa nini rais anataka suala hili lisiripotiwe kwa undani? Yeye anaiogopa aibu hii kiasi cha kutaka isitiriwe? Kama ni hivyo sina budi kuamini kuwa yeye ndie aliyemtuma kijana huyu, sasa kama alimtuma asiwaonee waandishi wa habari kwa KOSA LAKE.

Rais ni lazima aibebe misalaba yake hii, na kutaka kuvidhibiti vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii ni kujidanganya mweyewe tu. Hii ni dunia ya digital haturudi kwenda kwenye kuhesabu vidole. Tanzania haina amani hili tunalijua, sio Zanzibar na wala sio Tanganyika. Niliwahi kuonya kuwa, Zanzibar mnaitawala na mnaipenda, lakini visiwa hivi vina matatizo yake na gharama zake, ni lazima mzikubali kama lazima mtutawale,moja ya gharama tunayo waleteeni ni kuboresha upinzani Tanganyika. Hili tumefanikiwa kiasi kikubwa, ndio maana hivi sasa mnahangaika kuwadhibiti waandishi na vyama vya upinzani kama tulivyozowea huku Zanzibar.

Onyo kwa wabunge wote wa ccm katika bunge la jamhuri ya muungano wa Tanganyika. Rais wenu ana mpango wa kuwashughulikia nyote msio taka kufuata amri zake. Ndio maana bunge lenu halina thamani tena mpaka mkuu wa mkoa wa DSM bwana Makonda aka Bashite akathubutu kusema kazi yenu kulala na wengine kusinzia tu, bunge lina uwezo wa kumfungulia mashtaka mkuu wa mkoa huyu bila kupitia mahakama. Pengine wengi ya wabunge hata hawajui kama bunge lina nguvu kiasi hiki, lakini woga na tamaa ya kukosa ajira ya ubunge, wenye mshahara mnene, imewaziba midomo, pua na masikio kwa kuganga njaa.

Rais wenu amepiga marufuku bunge lenu lisionyeshwe moja kwa moja ”live” kwa kuhofia kumkosoa na nyinyi kupata umaarufu asioupenda au kuutaka, Nape ndie aliyeusimamia muswada huu mpaka ukapita kuwa sheria, nina uhakika leo anajuta.

Haya ilikuwa ayajuwe mapema, mchimba kisima huingia mwenyewe, kisingizio alichotoa rais wakati wa kukataza bunge live, kuwa watu wakafanye kazi badala ya kukaa kitako wakiangalia televisheni saa za kazi, aliyemwambia duniani watu wote hawatizami tv saa za kazi nani? Mbona leo serikali nzima imeacha kazi kwenda ikulu kuangalia mawaziri wawili wakiapishwa. Mbona huko ulimwenguni mabunge wanaonyesha moja kwa moja, au hakuna marais huko? Marais wa huko wote hawaijui hii kauli mbiu ya hapa kazi tu, huyu ni dikteta uchwara tu, naiba maneno ya rais mwingine wa Tanganyika, wa chama cha wana sheria bwana Tundu Kissu sio Lissu.

Watanganyika msiogope kama alivyosema mheshimiwa Nape, hasa vijana, nchi hii sio mali ya Msukuma mmoja au wawili, ni mali yenu nyote, hakuna alie juu ya sheria, sio rais sio mlala hoi, nyote mna haki sawa katika sheria, mna makabila mengi na tofauti hata waarabu mnao tele na nyie, msituonee choyo sie na waarabu wetu adhimu.

Aluta kontinua comrades.

Share: