Habari

MKAPA ATOA MAONI TUME YA KATIBA

WATU maarufu na Taasisi za jamii, wanaendelea kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, miongoni mwa waliyopata fursa hiyo jana ni Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.

Mbali na Mkapa, pia Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya naye alitoa maoni yake ambayo hata hivyo kama ilivyo kwa Mkapa, hayakuwekwa hadharani na wahusika.

Ofisi ya Tume ya Katiba ilituma picha kwa vyombo vya habari, kuonyesha viongozi hao wakitoa maoni yao mbele ya viongozi waandamizi wa Tume.

Mkapa alitoa maoni yake mbele ya Jaji Mkuu Mstaafu na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Agustino Ramadhani na Waziri Mkuu Mstaafu ambaye pia ni Kamishina wa Tume hiyo, Dk Salim Ahamed Salim.

Mazingira ya picha ya mazunguzo baina ya Mkapa na viongozi wa Tume hiyo, yanaonyesha kuwa na mandhari ya nyumbani katika jengo la ghorofa.

Ingawa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Tume katika utoaji maoni hayo. Rais Mkapa wakati wa utawala wake anakumbukwa kutafuta maoni ya wananchi juu ya marekebisho ya katiba kupita njia ya ‘white paper’.

Mfumo ambao Serikali inaeleza inachotaka na kuwataka wananchi nao kueleza wanachotaka. Tume hiyo ya Mkapa, ilikuwa inaongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Robert Kisanga.

Tume ya Jaji Kisanga, ilichukuwa jukumu hilo kwa kupita karibu maeneo yote ya Tanzania na wananchi walitoa maoni hayo, na kutoa mapendekezo kadhaa yakiwamo ya mfumo wa Muungano wa Serikali tatu.

Ripoti ya Tume ya Jaji Kisanga, haikumpendeza Mkapa na alihutubia wananchi kupitia wazee wa Dar es Salaam, na kumtolea maneno makali na ya kejeli Jaji Kisanga ambaye alipoulizwa juu ya hisia zake kwa kauli ya Mkapa, alisema “nimefedheheshwa”.

Mkapa alionekana kuwa mkali sana juu ya mapendelezo ya kuwako kwa muundo wa Muungano wa Serikali tatu. Kuwapo kwa mabadiliko ya lazima kwa mfumo wa Muungano ni suala lililovawaliwa njuga kwa sasa na Wazanzibari.

Mkapa pia anakumbukwa kwa jinsi utawala wake ulivyoshughulikia malalamiko ya kisaisa, hususan yale ya kupinga matokeo ya uchaguzi ya urais wa Zanzibar mwaka 2000.

Malalamiko ambayo yalisababisha watu kuingia mitaani kwa maandamano, lakini yakakutana na nguvu kubwa ya Dola ambayo ilisababisha mauaji ya watu zaidi ya 33.

Rais huyo mstaafu pia alikuwa na msimamo mkali juu kile kilichokuja kubatizwa kuwa “mpasuko wa kisiasa Zanzibar” ukihusisha vyama viwili vikuu vya siasa Zanzibar, CCM na CUF..

Share: