Habari

Mkurugenzi mpya manispaa mjini aomba ushirikiano

October 9, 2018

NA LAYLAT KHALFAN

MKURUGENZI mpya wa baraza la manispaa mjini, Said Juma Ahmada, amewaomba wafanyakazi wa baraza hilo, kumpa ushirikiano ili aweze kutekeleza makujumu yake kwa ufanisi.

Aliyasema hayo ofisini kwake Malindi wakati akizungumza na gazeti hili, baada ya kumaliza kuzungumza na wafanyakazi.

Alisema kuna baadhi ya wafanyakazi wana tabia ya kujigawa makundi na kusababisha kazi za baraza kutofanyika vizuri, hivyo aliwaomba kuacha tabia hiyo.

Alisema kama wafanyakazi watafanya kazi kwa ushirikiano ana imani kubwa taasisi hiyo itapata mafanikio ikiwemo kukusanya kodi kwa ajili ya serikali.

Aliwaomba wafanyakazi wanaokusanya mapato kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa weledi bila kumuonea mtu yeyote.

Kuhusu usafi wa mji, alisema hali ya mji bado hairidhishi, hivyo aliwasisitiza wafanyakazi wenye jukumu hilo, kusimamia vyema majukumu yao ili kuuweka mji katika hali ya usafi.

Nao wafanyakazi wabaraza hilo, walimshukuru Mkurugenzi huyo, na kuahidi kumpa ushirikiano ili kuifanya manispaa hiyo kuongoza katika ukusanyaji wa mapato na usafi wa mji.

Zanzibarleo

Share: