Habari

Mkurugenzi wa CUF (Mh.Suleiman) afarika dunia baada ya kuvamiwa na Mazombi

Mkurugenzi huyo alifariki dunia juzi wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, baada ya kupigwa na kujeruhiwa maeneo mbalimbali ya mwili na watu hao.

Ilielezwa kuwa usiku wa kuamkia Jumatano ya wiki hii, majira ya saa sita usiku, watu wasiojulikana walimvamia na kumteka kiongozi huyo nyumbani kwake kisha wakamchukua na kwenda naye sehemu isiyojulikana.

Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa watu hao waliokuwa na silaha za jadi, walimjeruhi kisha kumtupa kwenye msitu wa Masingini Mwera katika wilaya hiyo.

Mazishi ya mkurugenzi huyo yalifanyika jana katika makaburi ya Mwanakwerekwe na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CUF, wakiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Wafuasi wa chama hicho na wananchi mbalimbali walibeba jeneza la mwili wa marehemu kutoka Mtoni hadi Mwanakwarekwe kwa miguu tofauti na ilivyozoeleka kutokana na umbali wa eneo hilo.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, alisema kuwa tukio hilo ni la kusikitisha huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi zake ili kuwabaini wahusika.

Aliishutumu serikali kwa kusema: “Jukumu la serikali ni kuwalinda raia wake lakini kwa kiasi kikubwa serikali imeshindwa kulisimamia hilo.”

Aidha, aliwataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake wafuate maeekezo kutoka kwa viongozi wao.

Mazrui alisema Suleiman alikuwa mstari wa mbele katika harakati za chama na kabla mauti hayajamfika, aliacha usia kuwa wananchi wakatae uonevu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib, Hassan Nasir Ali, alisema hawezi kuzungumzia chochote kuhusu tukio hilo hadi pale askari wake wa upelelezi watakaporudi msibani na kumpa taarifa.

nipashe

Tagsslider
Share: