Habari

MKUTANO WA CUF

Na Peter Mwenda
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba  amesema inawezekana kabisa kwa kila mtanzania kulipwa sh. 450,000 kwa mwaka zinazotokana na rasilimali za asili.

Akizungumza na wanachama na wafuasi wa chama hicho kwenye viwanja vya Mwembeyanga Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema watanzania watalipwa fedha hizo kama watakiingiza kwenye katiba mpya kipengele hicho.

“Tanzania kuna rasilimali za asili nyingi, bahari, gesi, madini ya dhahabu, tanzanite, mbuga za wanyama na nyingine nyingi ambazo zinaweza kuingia sh. bil. 2 kwa mwaka ambazo zinatosha watanzania kukagawana sh. 450,000 kwa mwaka” alisema.

Alisema wafuasi wa CUF wasitishike na helkopta zinazoranda kwenye chaguzi kuwa vyama hivyo havina uwezo wa kuleta mabadiliko kwa watanzania ambao wamekata tamaa kutokana na kukosa ajira.

“CCM na vyama vingine vinavyoongozwa na wapiga disko haviwezi kuwakombioa watanzania akimaanisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho Mwenyekiti wake anamiliki ukumbi wa Billicanas.

Alisema uchumi wa Tanzania unazidi kuwa taabani kwa sababu gharama za kuyingia tani 100 kutoka China ni nafuu kuliko kusafirisha tani moja kupeleka mkoa wa Kigoma na kuongeza kuwa rasilimali ambazo Tanzania inazo zinakosa viongozi wa kuzisimamia na badala yake zibnaingia kwenye mikono ya mafisadi.

Profesa Lipumba hata hivyo alimsifu Rais Jakaya Kikwete kukubali kuruhusu uundaji mchakato wa kuanzisha Katiba Mpya na kuongeza kuwa napaswa kuungwa mkono.

Alisema ili mipango hiyo itimie watanzania wote wakubali kujiandikisha kupewa vitambulisho na kuchangia kuundwa kwa Katiba mpya ambayo itasema kila mtanzania alipwe rasilimali za nchi.

Awali Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema wanaopiga kelele kuwa CUF imekufa wanajidanganya kwa sababu mapokezi wa Profesa Lipumba Machi 11 mwaka huu ni ushahidi tosha kuwa chama hicho hakitakufa kamwe.

“Mimi nilitoa machozi baada ya kuona umati mkubwa ulijitokeza kumpokea Mwenyekiti wetu, hiyo ni salamu kwamba tumeanza mikakati ya kuingia Ikulu, tumeingia mguu mmoja Zanzibar, mwaka 2015 tunaingia miguu yote je, Ikulu ya magogoni mnasemaje?aliuliza Maalim Seif na kuitikiwa na sauti kuwa CUF inachukua dola.

Katika mkutano huo CUF imetoa namba 15338 kwa njia ya mtandao wa zantel ambayo mwanachama wake atachangia kwa ajili ya kujiandaa na uchaguzi wa 2015 ambako pia aliywahi kuwa kiongozi wa chama hicho na baadaye kuhamia CCM, Bw. Hamisi Kituga amerejea katika chama hicho na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti Profesa Lipumba.

Pia Mjumbe wa baraza Kuu la Taifa la chama hicho kutoka mkoa wa Mbeya, Bw. Yassin Mrotwa ambaye alikuwa mmoja wa wanachama walioshtaki mahakamani amejitoa na kurudi CUF.

Share: