Habari

Moto wa Mswada wa Katiba wamuakia Balozi Seif Idd

Chama cha Wananchi (CUF) kimemtaka Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, kujiuzulu wadhifa huo kwa kushindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar. Kauli hiyo ilitolewa mjini Zanzibar jana na Mjumbe wa Baraza Kuu la CUF, Ismail Chusa Razu, wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kibanda Maiti.

Alisema Balozi Seif amegeuka dalali wa kuiuza Zanzibar baada ya kukiri kuwa Zanzibar ilishirikishwa katika Mswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Muungano katika kipengele kinachohusu Zanzibar, jambo ambalo sio kweli. Aliongeza kuwa, Balozi Seif akiwa kiongozi alistahili kuzungumza na Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na Mwanasheria Mkuu ndipo apate cha kuzungumza.

“Namtaka Balozi Seif ajiuzulu nafasi yake kwa kushindwa kusimamia maslahi ya Zanzibar, ikiwa ana uchungu wa Zanzibar hakustahili kusema hivyo,” alisema na kuongeza kuwa kuanzia sasa watakuwa wakimuita Balozi Mkazi wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa upande wa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru,kusema anashangaa wazee wenzake kuleta rasimu ya Serikali tatu wakati Serikali mbili zilizopo kila moja ina mipaka yake na Zanzibar na bara zilikufa mwaka 1964 wakati nchi mbili zilipoungana,Chusa alisema Zanzibar bado ipo hai na itaendelea kuwa hai hadi kiama.

Alisema iliyokufa ni Tanganyika hivyo kama lengo ni kuizika Zanzibar bado hawajafanikiwa kwani Wazanzibari wapo macho.

“Zanzibar ipo hai na itaendelea kuwa hai hadi kiama, nchi hii haijazikwa,” alisisitiza. Kwa upande wake Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, alimtaka Rais Jakaya Kikwete, asisaini mswada huo, kwani ana nia nzuri, lakini wenzake wanataka kumpeleka kubaya.

“Rais Kikwete ana nia nzuri lakini wenzako wanakupotosha, usisaini mswada huu tunajua una nia nzuri,”alisema Maalim Seif na kuongeza kuwa iwapo atakubali kusaini mswada huo atazuia wajumbe wa chama hicho wasishiriki Bunge la Katiba. Alishauri mswada huo urejeshwe Zanzibar ili kupata Katiba Bora. Kuhusu Balozi Seif, Maalim Seif alisema anamuonea huruma makamu mwenzake huyo kwa sababu hakujua ni mswada upi aliuona.

Alisema Mei 6, mwaka huu aliitwa Dodoma na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kuambiwa kuwa wanataka kufanya marekebisho kwenye vipengele sita ambapo walifanya marekebisho, lakini waliporudi Tanzania Bara walifanya marekebisho kwenye vipengele nane. Alisema makamu wake hakujua hilo na anashangaa ni kwa nini wana-CCM wenzake wamemtosa. Alisema bila shaka walikuwa wamepanga jambo hilo.

Alisema Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Mwanasheria Mkuu, Rais wa Zanzibar na yeye mwenyewe hawakubaliani na hilo.

Share: