Habari

Mpango wa kuvuruga GNU wafichuliwa

Salma Said, Zanzibar

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad jana amedai kuwepo kwa mpango maalumu unaofanywa na baadhi ya watu wenye lengo la kuvuruga serikali ya umoja wa kitaifa (GNU) visiwani Zanzibar.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Kibanda Maiti na kuhudhuriwa na maelefu ya watu Maalim Seif amesema mbinu za watu hao zimeshatambuliwa na kamwe wazanzibari hawatakubali kurejeshwa walipotoka kwa kuvurugiwa kwa serikali yao.

Akiwahutubia wafuasi wa chama hicho alisema mpango huo hauwezi kuwa na mafanikio kwa kuwa serikali ya umoja wa kitaifa imepewa baraza zote na wazanzibari wenyewe kwa kuichagua kwa kura nyingi za maoni na pia serikali hiyo ipo kikatiba hivyo haiwezi kuvunjika.

“GNU is there to stay,….na mimi ndio makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, mpango wao hautafanikiwa tumeshawagundua” alisema Maalim Seif huku akishangiriwa na wafuasi wake. Na kuongeza kwamba.

“Wale wenye ndoto kuwa serikali ya umoja wa kitaifa itavunjika yagujuuu hatutoki hatutoki na ili serikali ya umoja wa kitaifa itoke basi kuitishwe kura ya maoni” alisema Maalim ambaye ni makamo wa kwanza wa rais Zanzibar.

Maalim Seif alisema vitendo vinavyofanywa hivi sasa na jeshi la polisi kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ dhidi ya raia wasio na hatia ni miongoni mwa mipango ya kuwavunja moyo wananchi ili wachukie serikali yao.

Maalim Seif alisema kwa kuwa yeye ni kiongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa hangependa kumsema rais wake hadharani lakini kwa kuwa amefanya jitihada za kuwasiliana na kiongozi wake na kumueleza juu ya vitendo wanavyofanyiwa raia lakini jambo la kusikitisha Dk Shein hajachukua hatua yoyote dhidi ya kusimamisha vitendo hivyo vinavyoendelea ambapo hadi sasa wananchi wanaendelea kupigwa na kufuatwa majumbani kwa kisingizio cha kutafutwa wahalifu.

“Leo naongea kwa masikitiko makubwaaaa nina huzuni kubwa kwa mambo yanayofanyika hapa nchini kwetu na niseme ni mambo ya kishenzi kabisa wanaofanyiwa raia” alisema Maalim Seif.

Katibu Mkuu huyo alisema hapendi kuisema serikali na Rais wa Zanzibar hadharani, lakini analazimika kusema”Rais wangu Dk Shein unatungusha kwa kuwa wewe ndiye mwenye jukumu kubwa zaidi la kulinda amani ya Zanzibar.”

Hata hivyo katika kumkumbusha Dk Shein ahadi yake aliyoitoa siku ambayo anatangazwa mshindi na tume ya uchaguzi miaka miwili iliyopita Maalim Seif alisema “Dk Shein alichukua ahadi kwa wazanzibari wote kwamba atawalinda rai wote bila ya ubaguzi na akachukua hadi kwa Mwenyeenzi Mungu kwamba atailinda Zanzibar basi namuomba Rais wangu mpenzi akumbuke ahadi yeke”.

Katibu Mkuu huyo alimshutumu Rais Kikwete na Dk Shein na watendaji wake huku akieleza masikitiko yake ya kufanya kikao kikubwa Dodoma kinachohusu masuala ya nchi bila ya kumshirikisha yeye kwa kisingizio cha kipengele cha katiba kutomtambua.

“Inasikitisha kuona masuala mazito yanazungumzwa katika kikao ambacho kimewashirikisha viongozi wote isipokuwa mimi eti kisingizio katiba inamtambua waziri kiongozi … haikutaja makamo wa kwanza”

Alisema lengo la kikao hicho ni kuzungumzia vurugu zimetokea Zanzibar katika kipindi cha miezi miwili iliyopita ambapo polisi walilaumiwa kuwa hawakuchukua hatua za kukabiliana na vurugu zilizotokea.

“Viongozi wa ngazi ya juu wa serikali ya umoja wa kitaifa wote walikuwepo kasoro mimi, walishirikishwa kuandaa mpango huo, lakini kila likuepukalo lina kheri nalo na mimi bora nilipokuwa sikuwepo kwa sababu hata siku moja nisingebariki suala hilo.” alisisitiza Maalim Seif.

“Sasa haya yanayofanyika ndio matokeo ya kikao hicho kwa sababu polisi wanalaumiwa hawajachukua hatua sasa hivi ndio hao wanachukua hatua lakini wanafanya udhalilishaji mkubwa sana wa ukiukwaji wa haki za binaadamu, wanawapiga watu ndani ya majumba yao, watu wanahama majumba yao kutokana na unyama wanaofanyiwa mtu anapigwa mbele ya watoto wake mbele ya mkewe na kudhalilishwa jee rais haya hayaoni?” alihoji Maalim Seif.

Akivitaja vikundi ambavyo vinafakazi na polisi, na kutekeleza mpango wa kuvuruga serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuwadhalilisha wananchi ni pamoja na kikosi cha Janjaweed ambacho ni tawi la CCM, Ubayaubaya, kimyakimya, na mbwa mwitu na mbwa mkali ambao wote ni vikundi vilivyopewa mafunzo na sasa kuwafunza watoto wadogo kufanya uharamia.

Akizungumzia athari zilizopatikana baada ya jeshi la polisi kuzima vurugu zilizotokea Oktoba 17 Zanzibar, mwaka huu alisema kumetokea madhara ya kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa Zanzibar kutokana na vyombo vya dola kutumia nguvu ya ziada kudhibiti vurugu hizo.

Aidha alisema hatua za kurejesha amani wakati wa vurugu hizo hazikuwa muafaka, kutokana na nguvu iliyotumika ilikuwa kubwa kupita kiasi na hatua hizo ziliwadhalilisha wananchi wasiokuwa na hatia na mali zao kuhujumiwa, huku wengine wakipoteza maisha.

“Tunalaani mauaji yaloofanywa kwa polisi lakini pia tunalaani udhalilishaji unaofanywa na jeshi la polisi dhidi ya raia na hatuungi mkono kabisa unyanyasaji wanaofanyiwa wananchi hasa katika maeneo maalumu ambao ynajulikana ni maeneo ya wafuasi wa CUF kwa nini iwe hivi” alihoji Maalim Seif.

Maalim Seif alisema serikali na vyombo vya dola vitekeleze jukumu la kulinda haki za raia kwa kuwasaka waliohusika na tukio hilo bila kuwadhalilisha wananchi wasiokuwa na hatia.

Alisema hakutarajia vitendo vya aina hiyo kutendeka wakati huu ambapo mfumo wa serikali ya Zanzibar unaendeshwa kwa kuzingatia maridhiano ya kisiasa baina ya CUF na CCM ambayo lengo lake ni kumaliza uhasama na chuki na kujenga amani pamoja na kuheshimu utawala wa demokrasia.

Katika mkutano huo, Maalim Seif pia alisema mbali ya lengo la kuivuruga serikali ya umoja wa kitaifa lakini wahafidhina wanafanya juu shini ili kuuharibu mshikamano wa wazanzibari ambao kwa kiasi fulani ulikuwa umeonesha nia njema.

Akizungumzia lengo la tatu la wahafidhina hao alisema ni kuogopa mchakato wa katiba ambao unaonesha dhahiri kwamba wazanzibari wanapigania mamlaka kamili ya Zanzibar na kutaka Muungano wa Mkataba jambo ambalo ni mwiba kwa baadhi wana CCM na wahafidhina.

Katika hatua nyengine Maalim Seif aliitupia lawama Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kushindwa kuheshimu mawazo ya wananchi juu ya aina ya Muungano wanaotaka na kusema kwamba tume hiyo imekuwa ikiwalazimisha wananchi waseme kile ambacho wao wanakiamini.

Maalim Seif alimshauri Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Joseph Warioba ahakikishe tume yake inaheshimu mawazo tofauti ya makundi yote, yakiwemo yanayotaka mabadiliko katika mfumo wa sasa wa Muungano kwa kuwa tayari tume imeanza kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya makundi fulani.

Awali kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho. Salim Bimani alisema wazanzibari wamechoshwa na vitendo wanavyofanyiwa kwa kudhalilishwa na kupigwa bila ya hatia huku wneye kufanyiwa vitendo hivyo ni kutoka CUF.

Bimani alisema ni jambo la kusikitisha kuona hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya vitendo hivyo kuripotiwa na kuonekana hadharani na kuwataka wananchi wasikubali kurejeshwa walipotoka huku akiwasisitiza kujitokeza kwa wingi katika tume ya mabadiliko ya katiba ili kutoa maoni yao ili kubadili mfumo wa serikali.

“Wananchi msikubali kuchokozeka, nendeni mkatoe maoni kwani hii ni fursa pekee ya kupata katiba tuitakayo” alisisitiza Bimani.

Akisoma risala ya mikoa mitano ya Zanzibar, Khalifa Abdallah Ali alisema imani waliokuwa nayo wazanzibari kwa rais wao Dk Shein imeanza kuondoka na hivyo kumuomba kuchukua hatua ya kusitisha zoezi linaloendelea la vikosi vyake kupita majumbani na kuwapiga wafuasi wa CUF kwa kisingizio cha kuwatafuta wahalifu.

‘Tunamuomba rais wetu Dk Shein imani tuliompa alipokuwa anaingia madarakani ni kubwa na sasa tunamwambia imani hiyo imeanza kutoweka miongoni mwetu na tunamuomba ahadi aliyochukua ya kuhakikisha usalama wa raia wote anautekeleza bila ya ubaguzi kwani hilo ni jukumu lake kama kiongozi wa nchi’ alisema Khalifa.

Tagsslider
Share: