Habari

Mradi wa umeme Zanzibar wazinduliwa lakini ghafla wazimika tena

Salma Said

Poste on 

IMG_0131

Saa chache baada ya sherehe kubwa za uzinduzi wa mradi mpya wa umeme Zanzibar ambao una lengo la kuondoa mgao wa umeme, nishati hiyo muhimu imekatika Zanzibar yote.

Sherehe kubwa zilifanyika Uwanja wa Amaan mjini hapa jana na kuhutubiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein katika uzinduzi huo wa nyaya mpya za umeme kutoka Bara hadi hapa.

Wakati sherehe hiyo ilimalizika wakati wa adhuhuri umeme katika kisiwa cha Zanzibar ulikatika kwenye saa 9 mchana na hali hiyo ilidumu kwa zaidi ya nusu saa.

Meneja wa Shirka la Umeme Zanzibar (ZECO), Mbarouk Hassan alisema kwamba umeme umekatika Zanzibar yote lakini ni tatizo kutoka Tanzania Bara.

“Umeme uliondoa laini kabisa, ni tatizo kutoka Bara, limemalizika,” alisema Meneja huyo kwa njia ya simu.

Akizindua mradi huo uliogharimu dola za Marekani 64.4 milioni ikiwa ni msaada kutoka Marekani, Rais Shein aliwataka wananchi kuilinda miondumbinu ya umeme kwani imetengenezwa kwa gharama kubwa.

Pia aliita ZECO kufuatilia madeni yake na kuwataka wananchi kulipia bili zao za umeme kwani ‘haki na wajibu ni watoto pacha’.

Alisema kwamba hali hiyo sasa inatoa fursa nzuri kwa wawekezaji kuwekeza Zanzibar kwani watakuwa na umeme wa uhakika.

Mradi huo wa umeme umeanza Ras Kiromoni hadi Mtoni Zanzibar  ili kuondosha  tatizo la kukosekana kwa umeme  lililokuwa likiwasumbua wananchi kwa muda mrefu .

Matarajio ya Serikali ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuwa wawekezaji wengi wa ndani na nje wataweza kuwekeza na kupanua sekta za uwekezaji nchini kwani changamoto kubwa iliyokuwa inawakabili kwa ukosefu wa umeme wa uhakika tayari imepatiwa ufumbuzi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo leo huko katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar uzinduzi wa mradi mpya wa uwekaji wa laini ya pili ya umeme kutoka Ubungo, Dar-es-Salaam hadi Mtoni Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein aliwasihi wananchi kutumia fursa hiyo ya umeme wa uhakika kuongeza uzalishaji zaidi na vile vile kuanzisha shughuli mbali mbali za kujiajiri wenyewe na kuzalisha bidhaa kwa matumizi na kuuza nje ya nchi.
Alisema kuwa umeme ni kwa ajili ya maendeleo hivyo, ni vyema watu wote wakafaidika na fursa hii kwa kuimarisha maendeleo kuanzia ngazi ya Kaya, Shehia, Wilaya, Mkoa hadi nchi nzima.
Kutokanan na umuhimu wa huduma hiyo, Dk. Shein alilitaka Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO), lizidi kutilia mkazo utaratibu wa kuwapatia mkopo wa kuungiwa umeme wananchi wa kipato cha chini hasa wanaoishi vijijini ili na wao waweze kunufaika na huduma hiyo muhimu.
“Kukamilika kwa mradi huo na ule wa kukiunganisha Kisiwa cha Pemba na Gridi ya Taifa kunaifanya Zanzibar nzima kuwa na umeme wa uhakika tena bila ya mgao”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa mradi huo unatoa mchango mkubwa katika kutimiza malengo ya maendeleo kama yalivyoelezwa katika Dira ya Maendeleo ya 2020, Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA), Mpango Mkuu wa Kimataifa wa Malengo ya Milenia na vile vile kutekeleza Ilani ya Uchaguzi wa CCM.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo ni kielelezo cha urafiki baina ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa Zanzibar.
Alisema kuwa urafiki wa waru wa Zanzibar na Marekani hauishiitu kwenye umeme bali Shirika la MCC la Marekani lililosaiodia mradi huo, linasaidia pia, katika ujenzi wa kilomita 35 za barabara huko kisiwani Pemba katika kiwango cha lami.
Aidha, Serikali ya Marekani inasaidiana na Marekani katika sekta ya afya katika kupambana na Malaria, kifua kikuu na ukimwi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Shein sherehe hizo ni kukamilisha mchakato wa muda mrefu tangu mwezi wa Februari mwaka 2008 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete na aliyekuwa Rais wa Marekani Mhe. George W. Bush walipotia saini mkataba wa Millenium Challenge Compact wenye thamani ya dola milioni 698.1.
Aidha, Dk. Shein aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kuitunza miundombinu ya umeme hasa nguzo za umeme kutokana na baadhi ya wananchi kuchimba mchanga pembezoni mwa nguzo za umeme na kuwataka wananchi kuwa walinzi.
Nae, Balozi wa Marekani nchi Tanzania Mhe. Alfonso Lenhardt alieleza kuwa nchi yake itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha miradi yake mbali mbali ya maendeleo.
Balozi Lenhardt alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo mpya wa umeme wa wamu ya pili itakuwa ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kiuchumi na kijamii huku akipongeza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na mashirikiano mazuri kati ya Marekani na Zanzibar chini ya Serikali yake ya Mapinduzi Zanzibar iliyo chini ya Umoja wa Kitaifa.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Bwana Ali Halil Mirza alisema kuwa kazi ya uwekaji wa njia ya pili ya umeme kutoka Ubungo Tanzania Bara hadi Mtoni Zanzibar imegharimu jumla ya dola za Kimarekani milioni 64.4 kati ya Dola milioni 206.5 zilizotengwa kwa sekta ya nishati Tanzania.
Alisema kuwa kutokana na kukua kwa teknolojia waya huo mpya hautumii teknolojia ya upozaji kwa mafuta, hivyo changamoto zake za matunzo na matengenezo ni ndogo kulinganisha na waya wa awali ambao unatumia teknolojia ya mafuta ambayo inahitaji huduma mara kwa mara.
Kazi za ujenzi kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo zilianza rasmi tarehe 12 Septemba 2010 na kukamilika mwezi Machi mwaka huu.
Mapema Dk. Shein alizindua kituo kipya cha kisasa cha mtandao wa udhibiti na mawasiliano ya SCADA.
Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Balozi Seif Idd na viongozi wengine wa MCC kutoka Tanzania na Marekani.

 

Zanzibar Yetu

Share: