Habari

Msajili msaidizi wa vyama vya siasa alivyopotosha katika ‘mada moto’

14519778_1710126665978688_8271811003025116466_n
Mwenyekiti wa CUF kwa Idhini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba akisalimiana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi: Picha kutoka kwenye mitandao

Imeandikwa na Elbattawi
Jumamosi, Oktoba 8, 2016

NIMESIKILIZA clip ya ‘channel ten’ kuhusu kipindi cha mazungumzo cha “mada moto” mzungumzaji alikuwa Msajili Msaidizi wa vyama vya siasa, Six Nyahonza.

Alionekana kuzungumza kwa sura ya u-CCM, zaidi alijielekeze katika mazungumzo yake kumtetea msalijili wa vyama na ofisi yake tangu mwanzo hadi mwisho wa kipindi huku, akilinda maslahi ya CCM.

Nyahonza anasema: “Pofesa Lipumba alijiuzulu, lakini mchakato wa kukubalika kujiuzu kwake haukumpa jibu au niseme ulishindwa kuthibitisha uamuzi wake.”

Anasema: “Mamlaka iliyotakiwa kukubali au kukataa kujiuzulu kwa Lipumba ni mamlaka iliyomuweka madarakani ambayo ni Mkutano Mkuu wa Chama…mkutano huo haukufanyika na kutoa uamuzi.”

Nyahonza, anasema: “Baada ya muda kupita Lipumba, alibadilisha mawazo na kutengua uamuzi wake kwa kuwa bado alikuwa Mwenyekiti wa CUF.” Nyahonza, hapa alionekana kumaanisha kuwa nafasi ya mwenyekiti bado ilikuwa wazi.

Anasema: “Hadi Lipumba, alipotengua uamuzi wake mamlaka ya kuthibitisha kujiuzulu kwake haikufanya hivyo, ndiyo maana mkutano mkuu wa chama hicho, uliyofanyika Agusti 21 ulikumbwa na vurugu.”

Nyahonza, alipoulizwa na msikilizaji mmoja kwa njia ya simu kutoka Liwale, alijibu kwa kutoa mfono anasema: “Kujiuzulu ni sawa na mtu (mfanyakazi) aliyekwenda likizo na baadaye kurejea na kuendelea na kazi.”

Hapa napenda kumuuliza Msajili Msaidizi, Nyahonza: Hivyo, kweli hajui tofauti ya kujiuzulu na kuchukuwa likizo?.  Kama kweli Nyahonza, hajui maana ya kujiuzulu na likizo, hafai kuwa msajili wa vyama vya siasa. Nyahonza, anatupotosha anatuminisha kitu ambacho sicho.

Hata kwa mtu ambaye hakusoma kabisa, anajuwa kuwa kujiuzulu ni kuacha kazi kwa ustaarabu wa hali ya juu. Utaratibu huo ndiyo unaofanya muhusika kuheshimika ndani ya jamii.

Umri wangu wote, sijawahi kusikia ndani na nje ya Tanzania, kwamba kuna mtu amejiuzulu cheo chake na baadaye akatengua uamuzi wake. Profesa Lipumba, ndiye wa kwanza. Nyahonza, lazima ajue kuwa likizo ni mapumziko ya kazi kwa wingi ni siku 21 au siku 25 na kurejea kazini.

Profesa Lipumba, alijiuzulu kwa ridhaa yake, baada ya kukerwa na ujio wa Lowassa ndani ya UKAWA. Hii ni kwa mujibu wa kauli yake, aliposema “nafsi imenisuta naachia ngazi.”

Akiwa na maana kwamba, nafsi yake imemsuta kutokana na kutetea ufisadi, hawezi kumpokea fisadi akiwa mwenyekiti wa chama mshiriki wa Ukawa. Nyahonza, afahamu kuwa Profesa Lipumba, hakufukuzwa.

Profesa Lipumba, hakustahiki tena hata kuulizwa au kuitwa katika mkutano mkuu wa CUF, kuthibitisha uamuzi wake kwa kuwa barua ilishatosha. Barua ni maandishi na maandishi yanashinda kauli.

CUF, haikuwa na sababu kuharakisha kukamilisha mchakato wa kuthibitisha kujiuzulu kwa mwenyekiti wake. Kwa sababu mbili muhimu:

Muda haukuruhusu kwa wakati ule, mazingira ya kujiuzulu na kila mtu aliamini kutokana na Profesa Lipumba kuwa ni msomi aliyebobea. Kwa hivyo, hakukuwa na hofu wala shaka kwamba, baadaye atageuka kinyonga, atageuza kauli na imani yake.

Hapa nafafanua zaidi. 

(1) Kipindi alipojiuzulu Lipumba, hakukuwa na muda wa kuitisha mkutono mkuu wa chama kuthibitisha au kukataa uamuzi wa Profesa Lipumba kujiuzulu na kujaza nafasi hiyo. Kamati ya muda iliyoundwa na Baraza Kuu, iliridhiwa na ilipata baraka zote za Ofisi ya Msajili.

(2) Kadhalika, haijawahi kutokea kiongozi wa taasisi yoyote iwe ya chama au serikali kuchukuwa uamuzi wa kujiuzulu baadaye kusitisha/kutengua uamuzi wake, Lipumba ni wa kwanza.

(3) Halafu, sababu nyingine ambayo imewashangaza watu wengi, wasomi wa fani zote, wakiwemo wahadhiri wa Vyuo Vikuu, wanasheria na wanasiasa ni kumuona Profesa Lipumba, mtu anaye heshimika kudhalilika na kudharaulika kwa mambo aliyoyatolea uamuzi kwa kipindi cha mwaka mzima.

Lazima hapa watu waache midomo wazi…washangae, wajiulize maswali mengi, kimezidi nini kwa msomi huyu nguli na kuonekana msomi mjinga. Kuna nini kilichojificha nyuma yake.

Watu wengi wanajiuliza Profesa Lipumba, ana shida gani…ana njaa gani…ana matatizo gani, amesibiwa na nini na ana nia gani?. Jibu, analo mwenyewe (Profesa Lipumba), Msajili wa Vyama vya Siasa na wengine waliyoko nyuma ya jambo hili kwa nia ya uovu.

Hivyo kweli, anahitaji Uenyekiti wa CUF, alioususa mwenyewe kwa hiari yake tena katika wakati ambao alikuwa anahitajika kuwepo ndani ya chama?. Liko jambo si bure. Hapa baadhi ya watu wana wasiwasi na mashaka na Profesa Lipumba.

Hata hivyo, kuna baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa, wanatilia shaka na namna ambavyo Profesa Lipumba alivyoibuka haraka kwa kishindo kudai kuwa bado ni Mwenyekiti wa CUF halali.

Wanasema: “Profesa Lipumba, kwa nini kasubiri hadi Katibu Mkuu wa CUF, kapeleka masuala ya Zanzibar, kwenye Jumuiya za Kimaifa na kuna uwezakano mkubwa wa kushughulikiwa?” Hapa pana kitandawili, panatia shaka…wanasema: “Si bure pana na mkono wa mtu.”

Kwa maoni yangu, napenda kumwambia, Nyahonza na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kwamba, wajue kukifuta CUF, hakutaweza kusaidia kukubalika kwa CCM katika mioyo na nafsi za Watanzania, hasa Wazanzibari.

Nampa mfano Msajili wa Vyama, Francis Mutungi na ofisi yake yote: Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, mwaka 1995 Pemba Majimbo yote 21, CCM haikuambulia kitu. Hivyo hivyo na chaguzi zote zilizofuata kila uchaguzi mkuu.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana wa Oktoba 25, Pemba majimbo yote 18 na viti vyote vya madiwani CCM, hawakuambulia kitu. Unguja, jumla ya viti 9 vilichukuliwa na CUF.

Majimbo yote ya Zanzibar (Unguja na Pemba) ni 54 ambapo 27 yalikwenda CUF. Ndiyo sababu serikali ilitia mpira kwapani.

Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ilikuwa tayari imeshawakabidhi shahada zao za ushindi wawakilishi na madiwani wote wa CUF, Unguja na Pemba.

Kwa hivyo, CCM na serikali zao, Ofisi ya Msajili wa vyama, Mutungi/Nyahonza na wenzao wengine wote, wanapaswa wafahamu kuzibadilisha imani za Watanzania na Wazanzibari, ni vigumu, si kazi rahisi wala haiwezekana kwa wakati huu tulionao.     

Kwa kumaliza: CCM kimechoka, kimeshazeeka, watu wamechoka kukisikia isipokuwa hawana budi, hawana hamu nacho, ndiyo maana serikali ya CCM inabana kwa kuzuia shughuli za kisiasa hasa mikiutano ya hadhara.

CCM na serikali zake hasa kwa upande wa Zanzibar, havina msaada kwa wananchi, maneno yamekua yale yale miaka nenda miaka rudi zaidi ya kauli za vitisho, matusi na dharau kutoka kwa viongozi.

Wananchi waliyo wengi bado wanateseka, hakuna unafuu wowote wa maisha yao, siyo maji wala umeme, siyo matibabu na afya, siyo miundombinu mjini na vijijini, elimu ni duni na maisha kwa jumla hali ni ngumu. Watu wanahangaika kutokana na kuongozwa na watu wasiyokubalika.

Wafanyakazi wa serikali, wafanyabiashar na wananchi wa kawaida wanalia na ugumu wa maisha hakuna siku ambayo imekuwa na nafuu chini ya CCM. Wananchi wameshajikatia tamaa kabisa mpaka watu wanaonesha huruma.

Watanzania sasa wanataka mawazo mapya yanayoendana na hali ya duniani. Wanataka chama kiingine na siyo CCM. Kinatumia nguvu nyingi kubaki madarakani kwa sababu eti kimeleta ukombozi.

Vingapi vimeleta ukombozi Afrika, havipo tena vimeshasahaulika na nchi zimepiga hatua na kuwa na maendeleo makubwa ya kupigiwa mfano na kuigwa.

Chama kimeshachoka hakina tena mvuto, yaani ingekuwa ni nguo ingekuwa ni viraka vitupu au imejaa viraka. CCM basi watu wametubu. CCM, wakubali fikra na mawazo mapya.. 

Tagsslider
Share: