Habari

Msemo: ‘lakuvunda halina ubani’

Al Nofli
Jumamosi, Machi 9, 2019

Kinachojiri sasa ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) kwa pande zote mbili, upande wa Profesa Lipumba na upande wa ‘CUF Taasisi’ (Maalim Seif), ni kutokana na mahakama kuu kushindwa kubainisha wajumbe halali wa Bodi ya CUF.

Itakumbukwa Ally Saleh wa CUF upande wa Maalim Seif, alifungua mahakama kuu kesi dhidi ya Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) akiomba mahakama kubainisha wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kati ya makundi mawili ya wajumbe yanayovutana.

Takriban wiki tatu sasa tangu Mahakama Kuu ilipotengua uteuzi wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka upande wa Mwenyekiti wake anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Ingawa uamuzi huo ulitarajiwa kumaliza mvutano wa uhalali wa wajumbe wa bodi ya chama hicho, kati ya pande mbili zinazovutana, lakini ni dhahiri pande hizo zitarudi tena mahakamani kuomba iingilie kati kw kuwa mvutano huo umeanza upya.

Uamuzi huo uliotokana na kesi namba 13 ya mwaka 2017, iliyofunguliwa na Mbunge wa Malindi, Ally Saleh, kutoka kambi ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, dhidi ya Wakala wa Usajli, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Ally Saleh alikuwa akipinga wajumbe wa bodi walioidhinishwa na Rita kutoka kambi ya Profesa Lipumba kwa madai hawakuwa halali kwa kuwa hawakupatikana kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Hivyo alikuwa akiiomba mahakama hiyo itamke kuwa wajumbe waliokuwa wamependekezwa na kambi ya Maalim Seif ndio halali.

Katika uamuzi wake Jaji Benhajj Masoud, Februari 18 mwaka huu, alitengua utezi wa wajumbe hao kutoka kambi ya Profesa Lipumba, akisema kuwa haukuzingatia Sheria ya Muunganiko wa Wadhamini.

Pia, alisema kwamba hata wale waliokuwa wamependekezwa na upande wa Maalim Seif hawakuwa na sifa ya kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi kwani nao hakuwa wamekidhi matakwa ya Sheria ya Muungano wa Wadhamini, kifungu cha 17.

Narudia: Februari 18, Mahakama hiyo ilitangaza kutengua uteuzi wa wajumbe wa bodi hiyo na kutowatambua wajumbe wa upande wa Maalim Seif.

Matakwa hayo ni kuwapo muhtasari wa kikao halali kilichopendekeza majina husika na kwamba kikao hicho ni lazima kiwe kimesimamiwa na mamlaka halali ya kiserikali.

Jaji Benhajj alisema kuwa katika ushahidi wa pande zote hakuona muhtasari wa kikao cha kupendekeza majina hayo, ambao ungemwezesha kubaini kuwepo kwa kikao na uhalali wake na kwamba majina yaliyopendekezwa na makundi yote hayakustahili kuteuliwa.

Huenda, kauli na hatua zilizochukuliwa na viongozi wanaoongoza kambi hizo baada ya uamuzi huo, zinaonesha kuendelea kwa mvutano huo na kurudishana tena mahakamani kwa jambo hilo.

Kambi ya Maalim Seif iliuona uamuzi huo kama ushindi kwake na kuwa na matumaini ya kupata usajili wa wajumbe wapya wa bodi, hatua ambayo awali walikataliwa na Rita.

Maalim Seif aliwaeleza wanahabari kufurahishwa na uamuzi huo kwamba umekata mzizi wa fitina kuhusu madai yao dhidi ya Rita kuhusu bodi hiyo.

“Kwa ufupi Mahakama Kuu imetamka kuifuta rasmi bodi ‘feki’ ya Lipumba na kikundi chake na kuitanabaisha Rita kwamba ifanye kazi zake kwa kuzingatia sheria,” alisema Maalim Seif.

Kwa upande wake kambi ya Profesa Lipumba nayo iliutafsiri uamuzi huo wa mahakama kuwa iwapo wakirekebisha kasoro zilizoainishwa na mahakama ni dhahiri wajumbe wake watasajiliwa.

Siku hiyo hiyo ilianza harakati za uteuzi tena kwa kuzingatia uamuzi huo, ambapo ilipeleka barua ofisi ya Msajili ikimjulisha na kumwalika kuhudhuria kikao cha Baraza Kuu la Taifa kesho yake kwa ajili ya uteuzi wa wajumbe wapya.

Hivyo kesho yake, Februari 19, siku moja baada ya uamuzi wa mahakama, kambi ya Profesa Lipumba ilifanya uteuzi wa wajumbe walewale waliotenguliwa lakini mara hii kikao cha utezi kikihudhuriwa na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza.

Februari 20, kambi ya Maalim Seif nayo iliitisha kikao cha Baraza Kuu lake la Taifa na kufanya uteuzi.

Katika kutimiza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama, walimwalika Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob na Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia (TCD), James Mbatia.

Huu pia unaweza kuwa utata mwingine kuhusu mamlaka ya kiserikali inayotajwa na sheria hiyo kama ni viongozi wa kisiasa au ofisa wa taasisi ya kiserikali, yenye dhamana na vyama vya siasa au usajili wa bodi.

Siku hiyo hiyo kambi ya Maalim ilitangaza uteuzi huo kwa vyombo vya habari, huku ikieleza inaamini mara hii Rita itawasajili kwa kuwa wametimiza matakwa ya kisheria.

Profesa Lipumba licha ya kutangulia kufanya uteuzi lakini aliutangaza kwa vyombo vya habari siku mbili baadaye akitanguliwa na Maalim kwa siku moja.

Kambi zote tayari zilishawasilisha Rita fomu zikiwa na majina ya walioteuliwa kuwa wajumbe wapya wa bodi, ili waweze kuidhinishwa.

Ingawa kila upande ulitamba kuwa majina iliyoyateua ndio yanayostahili kusajiliwa na Rita kuwa wajumbe wapya wa bodi ya chama hicho, huku wote wakirejea uamuzi wa Mahakama Kuu, lakini uamuzi huo, ukisomwa ndani ya mstari unaonyesha kuisafishia njia kambi ya Profesa Lipumba.

Kwanza, Jaji Benhajj katika uamuzi wake hakusema amekubaliana na ushahidi kwamba wajumbe wa bodi waliokuwapo muda wao ulikuwa haujaisha na kwamba unaisha mwaka huu kama Maalim alivyowaeleza waandishi wa habari.

Ushahidi wa upande wa mwombaji (Ally Saleh) ulikuwa na mkanganyiko ambao hauwezi kufumbiwa macho, akibainisha kuwa katika hati yake ya madai alidai muda wa wajumbe wa awali uliimalizika mwaka 2017.

Wakati akitoa ushidi wake mahakamani alidai kuwa muda wa wajumbe hao unakwisha mwaka 2019 na kwamba majina yaliyopendekezwa yalikuwa ni kujaza baadhi ya nafasi zilizokuwa wazi.

Hata hivyo, akirejea vielelezo mbalimbali hususan fomu za maombi ya usajili kutoka kambi ya Maalim Seif, barua ya Rita kwenda kwa Maalim Seif na nyinginezo zinaonesha kuwa muda wa wajumbe wa awali ulikuwa umekwisha.

Akihitimisha hoja hiyo, Jaji Benhajj alisisitiza kuwa kwa maana hiyo chama hicho kitakuwa hakina wajumbe wa bodi ya wadhamini lakini akasema hilo si lake bali linaihusu mamlaka husika.

Jaji Benhajj alisema kuwa kwa mujibu wa barua ya Rita kwenda kwa Katibu Mkuu, Maalim Seif inatambua kuwepo kwa kambi hizo mbili na kwamba kambi moja ndio inayotambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Rita katika barua yake ya Juni 12, 2017 kwenda kwa Maalim Seif, inamjulisha kupokea majina kutoka makundi mawili ya chama kimoja (aliyoyawasilisha yeye Maalim na aliyoyawasilisha Kaimu Katibu Mkuu, Mgdalena Sakaya).

Ilieleza kuwa baada ya kupokea majina ya makundi mawili ilifanya mawasiliano na Ofisi ya Msajili wa Vyama ili kupata ufafanuzi, kwani kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, Msajili ndiye anatambua viongozi halali wa vyama vya siasa.

Jaji Benhajj alisema kuwa mawasiliano baina ya Rita na Ofisi ya Msajili (kupata ufafanuzi wa viongozi halali wa chama hicho waliostahili kuwasilisha mapendekezo ya wajumbe wapya) ndicho kilikuwa kigezo cha usajili wajumbe wa kambi hiyo.

Alisema hana tatizo na mawasiliano hayo na kwamba kwa mtazamo wake makusudio ya sheria katika kubaini wanaostahili kuwa wajumbe halali yanalenga wale waliyoko katika kitabu cha msajili na si walioko nje.

Kwa hukumu na kauli yake Jaji Benhajj ndiyo nilipokumbuka msemo huu wa wahenga kwamba ‘lakuvunda halina ubani’

Sasa, Bodi ya wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Ibrahim Lipumba imesajiliwa rasmi na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya akizungumza Dar es Salaam siku Ijumaa Machi 8, 2019 alisema Rita imewaandikia barua inayoonyesha maombi yao ya kusajiliwa yamekubaliwa na bodi hiyo imesajiliwa.

Sakaya amesema hatua hiyo imekuja kufuatia kurekebisha dosari walizoelezwa na Mahakama Kuu na hatimaye kukidhi vigezo vya kuwa na bodi inayotakiwa.

“Machi 6 nimepokea barua kutoka Rita ikionyesha maombi yetu ya kusajili bodi yamekubaliwa. Bodi yetu imesajiliwa na wajumbe wake wote wanane,” alisema Sakaya.

Aliongeza: “Kinachofuata sasa tunasubiri bodi ikae ichague mwenyekiti wake na kuanza kufanya kazi ya kukiendesha chama ikiwemo kushughulikia kesi zilizopo mahakamani.”

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa 2015, CUF imekuwa katika mgogoro uliokigawa chama hicho pande mbili ya Profesa Lipumba na Maalim Seif na mgawanyiko huo umefika mpaka kwa wanachama, wabunge, madiwani na viongozi wengine.

Nini chanzo cha mgogoro wa CUF, hapa hakuna jambo la kulificha kuwa mgogoro huu umeratibiwa na serikali zote mbili za CCM kwa lengo maalumu, hasa kuhusu Zanzibar, baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu uliyopita na CUF kuibuka kidedea.

Kwa hivyo, CUF upande wa Maalim Seif ina hali ngumu na hata ikijaribu kupapatua si rahisi kuweza kufanikiwa Bodi yake ya Wadhamini kusajiliwa na Rita, halafu kuungwa mkono na Msajili wa Vyama vya Siasa na hata mahakama nayo haijakaa vizuri katika mgogoro huu.

Mahakama za Tanzania, zinategemea na msimamo wa Jaji au Hakimu anaendesha kesi husika na ushawishi wa CCM na serikali zake.

Mfano ni Hakimu, Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Kisutu na kesi inayowakabili akina Mbowe alivyowafutia dhamana na kuwasababishi kukaa rumande miezi mitatu.

Uamuzi wa kuwafutia dhamana akina Mbowe ni dhahiri ulikuwa na shinikizo na maagizo kutoka juu kwamba: ‘wewe fanya hivi mimi nitakulipa cheo’ Baada ya uamuzi ule Wilbard Mashuri alipandishwa cheo kutoka Hakimu hadi Jaji wa Mahakama Kuu.

Narudia kidogo. Wakati mawakili wa kambi ya Maalim Seif wakionyesha kufurahia uamuzi huo, wakili wa kambi ya Profesa Lipumba, Mashaka Ngole alisema watakachofanya ni kuitisha kikao ili kufanya uteuzi mpya kwa kuzingatia matakwa hayo ya kisheria.

“Kwa sasa nimeitwa kwenye kikao, lakini tulishakubaliana kwamba tunaitisha kikao rasmi ili kufanya uteuzi upya,” alisema Wakili Ngole.

Wajumbe waliokuwa wamependekezwa na kambi ya Maalim Seif, ambao hawakusajiliwa na Rita na ambao Ally Saleh alikuwa anataka mahakama itamke kuwa ni wajumbe halali ni Abdallah Khatau, Joran Bashange, Ali Suleiman, Juma Muchi, Mohamed Mohamed na Yohana Mbelwa.

Hata hivyo, Jaji Benhajj katika uamuzi wake alisema majina ya pande hizo zote hayakuwa na sifa kuteuliwa kuwa wajumbe wa bodi hiyo kwa kuwa walipendekezwa kinyume cha Sheria ya Muungano wa Wadhamini, kwani hapakuwa na kikao halali kilichowapendekeza.

“Kwa sababu hizo, kwa maoni yangu ni kwamba kwa kuzingatia kifungu cha 17 cha Sheria ya Muungano wa Wadhamini, hakuna hata mmoja aliyestahili kusajiliwa kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini,” alisema Jaji Benhajj.

Alisisitiza: “Kama mdaiwa wa kwanza (Rita) angezingatia matakwa ya sheria, hawa wote (majina ya pande zote mbili yaliyokuwa yamependekezwa) hawastahili.”

Alisema kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria, mambo yanayotakiwa kuzingatiwa na Rita katika kusajili wajumbe wa bodi za taasisi au bodi ni kuwepo kwa mkutano halali wa taasisi au bodi husika ulioteua au kupendekeza majina.

Jambo lingine ni mkutano huo uwe umesimamiwa na mamlaka halali ya kiserikali.

Kwa mfano mdogo, kwani upande wa Maalim Seif ugewaalika Rita na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa katika mkutano wake wengekwenda huku wakijuwa wanachokifanya ni kutekeleza maagizo ya seriakili za CCM.

Hata hivyo, wajumbe wa kambi ya Maalim Seif hawakuwa wanatambuliwa na Rita ndiyo sababu Ally Saleh alipeleka shauri mahakamani.

Kwa hivyo, Rita na Msajili wa Vyama vya Siasa chochote kutoka upande wa Maalim Seif walikuwa hawakitambui. Hilo ni agizo kwa malengo makusudi.

Kwa ufupi niseme ya Mungu mengi: Lakini, CUF upande wa Maalim Seif una hali ngumu sana, imekumbwa na janga kubwa. Janga la kutengenezwa tangu siku ya kwanza Lipumba alipong’atuka uenyekiti na kwenda likizo Rwanda.

Balozi Seif Ali Iddi katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiembe Samaki, aliwahi kuzungumzia mwisho wa CUF. Lakini CUF wahawakutanabahi ama hawakufahamu mbinu ovu zilizopangwa na CCM na serikali zake.

Lipumba kama Lipumba hana uwezo wa kuiua CUF Taasisi, si Msajili wa Vyama wala si Rita wenye uwezo wa kuiua CUF kwani siku zote hawa walikuwepo na hawakuthubutu kufanya wanayofanya sasa.

Narudia tena: Jaji Benhajj, Akizungumzia madai na ushahidi wa mdai (Ally Saleh) alisema kulikuwa na mkanganyiko hasa kuhusiana na muda wa kuisha kwa bodi ya awali na lengo la usajili wa wajumbe wapya.

Alibainisha kuwa Ally Saleh katika hati yake ya madai alidai kuwa muda wa wajumbe wa bodi wa awali unaisha mwaka 2017, lakini wakati akitoa ushahidi wake mahakamani alieleza kuwa muda wa wajumbe wa bodi wa awali unakwisha mwaka 2019.

Pia Jaji Benhajj alisema kuwa Ally Saleh katika ushahidi wake alieleza kwamba majina yaliyopendekezwa yalikuwa ni kwa ajili ya kujaza nafasi zilizokuwa zimeachwa wazi tu.

Jaji huyo alisema kwamba mkanganyiko huo hauwezi kufumbiwa macho.

Uamuzi wa kesi kuu ya uhalali wa uenyekiti wa Lipumba, Jumatatu tarehe 18 mwezi huu, ndiyo kitanzi cha mwisho kwa pande zote mbili za chama hicho.

Jana (Ijumaa Machi 8) Magdalena Sakaya alisema usajili wao umefanikiwa baada ya kurekebisha dosari zilizoelezwa na mahakama na kufuata maelekezo waliyopewa ili kuirasimisha bodi yao.

Alisema hatua inayofuata ni bodi hiyo kukaa na kuchagua mwenyekiti ili kuanza kazi ya kuendesha chama na kushughulikia kesi zilizopo mahakamani.

“Niwasihi wanachama wa CUF na Watanzania kwa ujumla waache kusikiliza habari zisizoeleweka zinazozungumzwa huko mitaani na kwenye mitandao ya kijamii,” alisema Sakaya.

“Chama kipo imara chini ya Profesa Lipumba na tunasubiri bodi ianze kazi mara moja kukipeleka mbele zaidi.”

Wakati Sakaya akieleza hayo, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor Mazrui alisema kwamba Rita inawarudisha nyuma walikotoka kwa kusajili bodi ya upande wa Profesa Lipumba.

“Awali tulipowauliza Rita mnasajili lini Bodi walitujibu wanasubiri hukumu ya Machi 18 kuhusu uhalali wa Lipumba.”

“Lakini leo (Ijumaa Machi 8, 2019) tunasikia Rita imekubali kuisajili bodi ya Lipumba…hii siyo dalili nzuri ina lengo la kukivuruga na kuisambaratisha CUF,” alisema Mazrui na kuongeza:

“Sisi tulikuwa wa kwanza kupeleka majina ya wajumbe lakini waliojibiwa ni wale waliopeleka mwisho.”

Alisema kwa sasa hawawezi kuzungumza au kufanya lolote badala yake wanasubiri uamuzi wa kesi yao Machi 18 utakaowapa mwelekeo wa hatua za kuchukua kuhusu mwenendo wa chama hicho.

Uamuzi huo unatarajiwa kuamua kama Profesa Lipumba ni mwenyekiti halali wa CUF au la, baada ya mwaka 2015 kutangaza kujiuzulu nafasi hiyo kisha baadaye kurejea na kusema ametengua uamuzi wake.

Kwa ufupi, kwa mtazamo wangu nasema ‘Inna lillah wa Inna Ilayhi Raajiun’ Dalili zote zinaonesha kuwa CUF haipo tena kwenye ramani ya Zanzibar, haipo tena kwenye ramani ya Tanganyika na Dunia kutokana na hujuma za viongozi wa CCM na serikali zao.

Ila najivunia sana kuwa upinzani wa Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) dhidi ya CCM na seriakali zake umo ndani ya damu ndani ya mioyo yao si wa majengo wala bendera wala sare zao.

Kwa hiyo chochote kitakachotokea Jumatatu, Machi 18, 2019 Makahama itakapotoa hukumu kuhusu Lipumba, naamini upinzani hautatetereka na utazidi kuimarika kwa sababu ni njama na njama hazijawahi kufanikiwa, njama ni dhulma.

Share: