Habari

Msemo: ‘Lisilobudi hutendwa’

Picha: Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa na mbunge wa chama hicho, Yussuf Salim (Chambani Pemba) ambaye wiki iliyopita alisema bila kutafuna maneno kuwa anaazimia kumfata Maalim Seif Sharif Hamad, ACT Wazalendo aliyehamia chama hicho wiki tatu zilizopita.

Habari kutoka vyanzo mbalimbali Tz.

Jumapili, Aprili 7, 2019

Hatima ya wabunge 23 wa Chama cha Wananchi (CUF) kutoka Unguja na Pemba itajulikana ndani ya kipindi hichi cha bunge la bajeti kilichoanza wiki iliyopita.

Hiyo inatokana na taarifa kwamba baadhi ya wabunge hao watajiuzulu ndani ya bunge hili na kumuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambaye amejiunga na ACT Wazalendo.

Wabunge hao ambao awali walikuwa wakimuunga mkono Maalim Seif katika mgogoro na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba sasa wanatakiwa kufanya uamuzi kama watabaki CUF ama nao wataondoka.

Hata hivyo, mara kadhaa Maalim Seif amezungumza na umma akisema amewaachia wabunge hao kuamua wenyewe kama watajiunga naye sasa hivi au la.

Kwa upande wake, Profesa Lipumba amekuwa akisema ni wakati sasa wa wabunge hao kujitokeza kwa umma na kuomba radhi kwa waliyofanya nyuma ili waendelee kukijenga chama chao.

Tayari baadhi ya wabunge wa CUF kutoka bara, akiwamo Mussa Mbaruku (Tanga mjini), Hamidu Bobali (Mchinga) na Selemani Bungara Bwege (Kilwa Kusini) wametangaza kumuunga mkono Profesa Lipumba.

Kwa Wabunge wa Zanzibar, wanakabiliwa zaidi na shinikizo la kuondoka kutoka kwa wapigakura wao ambao wengi wamejiunga na ACT.

Lakini, ‘lisilobudi hutendwa’ wabunge wa Zanzibar, itabidi kuwa na msimamo, waamue moja hivi sasa bila kusubiri kitanzi cha Profesa Lipumba kuwanyonga. Msimamo wa wabunge hao ni muhimu kwa sasa.

Wanachama wa CUF, waliowengi hasa kutoka Zanzibar (Unguja na Pemba), safu za uongozi wao wa majimbo kuanzia ngazi za matawi wamejiunga na ACT, jambo litakalokuwa vigumu kwao kufanya kazi.

Lakini, Mbunge wa Jimbo la Chambani, Pemba, Yussuf Salim ameweka wazi amesema, hana hofu kufukuzwa na kwamba, hayupo tayari kubaki Chama cha Wananchi (CUF), kinachoelekea kufa. “Maalim Seif ametoka na watu wote.”

Mbunge huyo mwenye ufasaha mkubwa wa kuzungumza na muwazi amesema kuwa, anakusudia kujiunga na ACT-Wazalendo kwa kuwa, hana sababu ya kubaki CUF.

Yussuf alitoa kauli hiyo licha ya kuwepo kwa wito uliotolewa na Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman Khalifa, kwamba wabunge wa chama hicho ‘waliowatusi’ viongozi wao waende kuungama ili wasifukuzwe.

Mbunge huyo alisema kuwa: “Nakwenda kujiunga na Chama cha ACT-Wazalendo kwa kuwa, sina sababu ya kuendelea kubaki CUF,” alisema na kuongeza:

“Na kwamba, Chama cha CUF kimepoteza uhai kwani kinachofanya kipumue kwa miezi 15 iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao ni ‘viruzuku’ tu.”

“CUF imekufa, haipo…wewe unaiona CUF ipo? Itadumu labda kwa sababu ya hivi ‘vi-ruzuku’ kwa huu mwaka mmoja na nusu uliobakia wa uhai wa Bunge…baada ya hapo, CUF haipo,” alisema Yussuf Salim.

Alisema kwamba, kwa kuwa CUF hakina pumzi tena, anasubiri muda wa kwenda kujiunga na ACT Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe, ambayo ndiyo mbadala wa CUF.

”Msimamo wangu unaeleweka na upo wazi kabisa kuwa mimi ni mbunge wa CUF kwa sasa lakini sibaki CUF, nakwenda zangu ACT Wazalendo. Kama nitamaliza kipindi hiki sawa, na kama sintomaliza sawa lakini nakwenda ACT Wazalendo.”

Aliongeza: “Wala sitafuni maneno katika hilo, nasisitiza nakwenda ACT Wazalendo, huko ndiko kuliko ‘shusha tanga pandisha tanga safari iendelee.”

Yussuf Salim alisema, kwa sasa anaendelea kubaki CUF kwa kuwa, wananchi wamemchagua kupitia chama hicho ili kuwakilisha kero zao bungeni na si vinginevyo.

“Mimi ni mbunge kwa sasa kwa kuwa wananchi wamenichagua, lakini nikiambiwa leo ondoka, basi naondoka, wala sina tatizo, kabisa!” alisema,” alisema Mbunge wa Chambani.

Yussuf Salim alisema kwamba, mara kadhaa CUF ilikuwa ikipiga kelele kwamba, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake wamekuwa wakipanga kuua chama chao, ndiyo kilichofanyika.

“Hili tulisema sana, sasa kama chama ni jina sawa, lakini CUF ni wanachama, ndiyo maana wanachama wanaondoka. “Chama ni watu sio jina,” alisema na kuhoji:

“Maalim katoka na watu wote wametoka. Sasa wao wanahangaika tu, si walitaka chama, wameachiwa chama, sasa kwanini wanababaika?.”

Mbunge huyo wa Chambani alisema, kwenye Uchaguzi Mkuu ujao kama uchaguzi utakuwa huru na haki, ACT Wazalendo inaweza kupata wabunge zaidi ya 30 kwa Zanzibar tu.

“Si kwa ACT Wazalendo, chama chochote tutakachoamua kwenda sisi, si wamesema wanataka kukifuta chama cha ACT, wakifute,” alisisitiza Yussuf Salim.

Akizungumzia hatima ya wabunge wanaomuunga mkono Maalim Seif, Profesa Lipumba alisema bado wana fursa ya kueleza msimamo wao hadharani na kuwaomba radhi wanachama ili kuendelea na uanachama wao.

Lipumba alisema wabunge hao wanatakiwa kueleza msimamo wao wakati uongozi wa chama hicho ukiendelea kujipanga kuijenga upya CUF, baada ya kuondoka kwa Maalim Seif.

“Kwa sasa tunawasikiliza msimamo wao mmoja baada ya mwingine. Bado wanapewa fursa hiyo ya kueleza msimamo wao iwapo wanaendelea kuwa kwenye chama au wanaondoka. Kwa walio tayari kubaki, watatakiwa kufuata taratibu za chama.”

“Wanatakiwa kuwa wazi. Waeleze utayari wao wa kushiriki kukijenga chama na wataomba radhi kwa wanachama ili kurejesha imani yao kwa chama. Kila mmoja atatakiwa kutekeleza hili, kwa taratibu zetu hili lazima lifanyike kwa uwazi,” alisema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba alisema hatua hizo ni muhimu katika kusimamia kujenga chama chao kilichokumbwa na misukosuko ikiwamo hatua ya Maalim Seif na wafuasi wake waliohitimisha kesi zaidi ya 35 dhidi yake kwa kutangaza kuhamia ACT-Wazalendo Machi 18, mwaka huu.

Alisema kwa sasa wanaona hakuna tena ukomo wa muda ila wanahitaji hatua hiyo ichukuliwe mapema na uongozi wa chama unaendelea kuwasiliana na wabunge hao ili kujua misimamo yao iwapo wataendelea kuunga mkono chama hicho au watahama kama walivyofanya wanachama na viongozi wengine waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif.

Profesa Lipumba alisema msimamo huo unawahusu wabunge hao 27 wa CUF ambao walikuwa wakimuunga mkono Maalim Seif katika kipindi cha miaka mitatu ya mgogoro wa kiuongozi.

Awali, wabunge 28 wa majimbo kati yao 22 kutoka Zanzibar, wanne wa Bara na mmoja wa viti maalumu walionekana kuwa na Maalim Seif, huku watatu wa majimbo ya Bara na tisa viti maalumu wakionekana kuwa upande wa Lipumba.

Tayari Profesa Lipumba na wenzake wameshabadili katiba inayompa mamlaka ya kuteua katibu mkuu, na alimteua Khalifa Suleiman Khalifa kuchukua nafasi ya Maalim Seif.

Hadi sasa, kati ya wabunge hao 28 waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif, ni mmoja tu, Bobali (Mchinga) ambaye ametekeleza masharti hayo, kwa kuomba radhi wanachama katika mkutano wa wazi wa Machi 17, 2019 huku akieleza msimamo wake kuwa yuko tayari kushiriki kuijenga CUF.

Mvutano huo ulianza baada ya Maalim Seif kutangaza uamuzi wa kuhama CUF na kuhamia ACT-Wazalendo, baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi namba 23 ya mwaka 2016 kuhalalisha uenyekiti wa Profesa Lipumba.

Katika mgogoro huo, wabunge wengi zaidi walijitokeza hadharani kuunga mkono upande wa Maalim Seif, hata kuamua kugharamia zaidi ya kesi 33 zilizofunguliwa Mahakama Kuu na kukodi ofisi mpya za CUF Magomeni, hivyo kumwachia Profesa Lipumba ofisi za CUF, Buguruni.

Katika hatua nyingine, CUF hususan Zanzibar chini ya uongozi mpya wa Katibu Mkuu wake, Khalifa Suleiman na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Abass Muhunzi kimeanza kudoda kwa kukosa kuungwa mkono na wanachama wake waliyowengi.

Watu wenye uzoefu katika CUF, wanadai kwamba wananchi wanaojitambulisha kuwa ni wanachama wa chama hicho si kweli, wengi ni wanachama wa kukodi kutoka CCM.

Hata hivyo, baadhi Watanzania wakiwemo wasomi wa fani mbalimbali wanashangaa kuwa CUF ya sasa ina fursa nyingi, ikiwa ni pamoja na kufanya shughuli za kisiasa kwa uhuru na uwazi bila vikwazo vya polisi kama ilivyo kwa vyama vingine vya upinzani.

Watu wengi wanahoji kuwa Chadema na ACT Wazalendo haviruhusiwi kufanya shughuli zozote za siasa huku, CCM ya Rais Magufuli na CUF ya sasa ya Profesa Lipumba vikifanya shughuli zake za kisiasa pamoja na mikutano ya ndani na ya hadhara bila kubugudhiwa na Polisi.

Kwa hoja hiyo, ndipo baadhi ya wananchi wanaona hawana sababu ya kuunga mkono CUF mpya ya Profesa Lipumba inayoendeshwa kwa nguvu za dola. Wanasema: “sheria za nchi hazibagui.”

Share: