Habari

Msemo: ‘Mungu si Athumani’

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akiwa na mwanachama mpya wa chama hicho – kadi No. 1, Maalim Seif Sharif Hamad. Walipokuwa wakitafakari namna ya kupokea mamilioni ya watanzania kutoka katika mikoa mbali mbali ya Tanzania Bara, wanaosubiri kujiunga na ACT-Wazalendo.

Al Nofli
Jumamosi, March 30, 2019

Msemo wa ‘Mungu si Athumani’ ni maarufu katika shida au baada ya shida yaani wakati wa faraja na raha. Jamii inapokumbwa na majanga au shida, watu husema ‘Mungu si Athumani’ kwa maana iko siku wataondokana na shida wanayokabiliana nayo.

Shida inapokwisha jamii ikapata faraja na raha na kutulia katika maisha yao ya kila siku watu humshukuru Mwenyezi Mungu, hapo ndipo wanaposema kuwa ‘Mungu si Athumani.’

Vilevile, jambo la ubaya analofanyiwa mtu au jamii kwa sababu za kuwakomoa au kuwadhibu watu katika dhamira yao; mtu au jamii husema kuwa ‘Mungu si Athumani.’

Pia, kuna msemo mwingine, tunasema: ‘hakuna shari isiyokuwa na kheri’ watu wengine husema ‘kheri imo ndani ya tumbo la shari.’ Tafsiri yake ni kwamba kila penye shari, hapakosi kuwa na kheri.

Misemo ya aina hii yote ni ya watu wa enzi za zamani ambao Mwenyezi Mungu, aliwajaalia kuona mbali na kujuwa mambo mengi na matukio ya baadaye.

Mifano yake ndiyo hii inayojitokeza sasa. Na hata hili suala la Maalim Seif ambaye ni muasisi wa Chama cha Wananchi (CUF) kupokonywa chama na watu waliyokaribishwa, tunaliona kama ni jambo la shari lakini, mbele tunakoelekea kuna kheri kubwa.

Katika mazungumzo yake ya siku ya Alhamisi (March 28) mjini Dar es Salaa, Maalim Seif alisema: “yote yaliyofanywa na niliyofanyiwa ni kutaka kuzuia haki niliyokuwa ninaipigania nikiwa CUF na sasa ACT-Wazalendo.”

Aliongeza kusema kuwa alikuwa anaendelea kufuatilia ahadi yake ya kutafuta haki ya Wazanzibari hadi washindani wake wakafika mahali wakaona hakuna namna isipokuwa wamtoe Seif CUF kwa kupandikiza mgogoro.

“Ningebaki CUF, nina uhakika isingefika mwaka 2020 Wazanzibari wangepata haki yao,” alisema Maalim Seif.

“Pamoja na chama kupewa Profesa Lipumba (Ibrahim), lakini maadam jina lipo la CUF haki ingekuja. Wakaona njia nyepesi ni kumwondoa Seif ili hata wakija wale wanaoweka shinikizo kwao, wakiuliza wanajibiwa kuwa huyu si mwanachama wa CUF tena,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alisema kufukuzwa kwake CUF ni kitendo cha makusudi ili kuhakikisha ndoto yake ya kuwapatia haki Wazanzibari isifanikiwe.

Pamoja na hatua hiyo, Maalim Seif alisisitiza: “madhumuni yote hayo ni kutuzuia tusipate haki yetu, lakini nawaambia haki haizami. Unaweza kuichelewesha tu,” alisema Maalim Seif.

Maalim Seif alihusisha ucheleweshaji wa haki hiyo na matukio wanayokumbana nayo katika siku za karibuni, kama polisi kuzuia mkutano wa ACT-Wazalendo uliopangwa kufanyika katika ukumbi wa PR, Temeke kwa madai kuwa wanachama wa CUF wanataka kufanya vurugu.

“Polisi wanakuja wanatuzuia na kutueleza kuna taarifa za intelijensia kuwa CUF wanataka kufanya vurugu. Hizi ni sababu zisizo na mashiko.”

“Wao ni polisi, moja ya kazi zao ni kulinda usalama wa raia na kulinda mikutano ya kisiasa. Hivi kama mnawajua hao wanataka kufanya vurugu, kwa nini msiwazuie. Kazi yenu ni kutuzuia sisi au wale wanaotaka kufanya vurugu?” alihoji Maalim Seif.

Anafafanua kuwa kulikuwa na amri ya mahakama kuu ya kuzuia mkutano mkuu wa CUF usifanyike, lakini polisi haohao ndio walikwenda kuulinda mkutano huo.

“Kwa hali hii ni ngumu kuamini kama jeshi la polisi linatendeka haki. Hawa waliozuiwa na mahakama wasifanye mkutano mnakwenda kuwalinda. Sisi tuliojifungia ndani pahala mnatuzuia, tena tunafuatwa hadi makao makuu ya ACT-Wazalendo,” alisema Maalim Seif.

Aliongeza: “Mbona Bashiru Ally (Katibu Mkuu wa CCM) anafanya mikutano. Alipotoka Lowassa (Edward – waziri mkuu mstaafu) Chadema kwenda CCM, Monduli kule kulikuwa na maandamano na mikutano ya hadhara polisi walichukua hatua gani?” aliuliza Maalim Seif.

Alisema jambo hilo (undumila kuwili) lipo wazi kwamba kuna watu wana haki lakini kuna wengine wana haki zaidi ya wenzao.

Maoni yangu: Mihimili yoto ya Tanzania ni kichefuchefu si utawala, si mahakama, si bunge ambalo limefurutu ada kwa ukandamizaji.

Dunia yote inajuwa kuwa CUF, imechukuliwa na CCM kwa nguvu za dola kwa sababu Tanzania wapo mabalozi wa kigeni na wawakilishi wa kimataifa wanaripoti katika nchi na taasisi zao kila tukio zuri na baya.

Halafu, hakuna kujuta kwa sababu ya CUF, hata ikitokea ACT-Wazalendo kufutwa pia tusisikitike hapo ndipo utakapozaliwa upinzani wa kweli wenye nguvu na imara kuweza kuimaliza CCM hasa upande wa Tanzania Bara ambako kidogo CCM inaonekana kuwa na afya.

CCM na dola yake kupitia mahakama, hawakukufikiria kuwa CUF wakishamkabidhi Lipumba itakuwa ndiyo mwisho wa viongozi na wanachama wake. Mungu si Athamani, ACT-Wazalendo kimeibuka kuchukuwa nafasi. Wanachokifanya sasa ni ‘jealous’. Ishara kwamba wananchi wamewachoka.

Baada ya misemo hiyo sasa nataka nifafanue.

Akiulizwa, Maalim Seif kwamba muda wote aliyokaa katika uongozi wa CUF, alitarajia kuwa itatokea siku moja Profesa Lipumba, anaweza kumgeuka kama ilivyotokea sasa?. Naamini, Maalim Seif atasema hakutarajia kutokea jambo hilo kufanywa na Lipumba. Ndiyo maana Maalim Seif anasema mgogoro wa CUF, umemfunza.

Profesa Lipumba, kabla ya kujitumbukiza katika dimbwi la usaliti dhidi ya chama cha CUF, hakuna kiongozi wala mwanachama wa kawaida aliyetarajia kuwa anaweza kuwa msaliti. Mfano wa Profesa Lipumba ni sawa na mchawi au mwanga na wanawe wanaompenda na kumuenzi. CUF chini ya uongozi wa Lipumba, imebaki herufi.

Profesa Lipumba mbali ya kuwa ana elimu kubwa ya dunia lakini pia, ni Al-Hajj. Muislam aliyefika Makka kwa dhamira ya kujitakasa na changamoto za dunia, ghafla kajisahau na kukumbatia tabia za unafiki na kugombanisha watu. Mtu wa aina hiyo amekumbwa na LAANA ya Mwenyezi Mungu.

Ni kweli nimeamini kuwa mnafiki atajulikana kwa ishara tatu ambazo zote tayari tumeziona kwa Profesa Lipumba.

Pia, nimeamini sababu ya Wazanzibari kuwa na mapenzi makubwa na Maalim Seif ni kutokana na kusimamia ahadi yake ya kuwa pamoja na Wazanzibari, aliyoitoa tangu akiwa waziri kiongozi takriban miaka 31 sasa.

Viongozi na wanachama wa CUF, wamemuachia Profesa Lipumba chama na wao wametafuta chama kingine kuweza kuendelea kufanya siasa na kutimiza malengo yao.

Lakini inashangaza kuwa, Profesa Lipumba hajaridhika na hatua ya Maalim Seif na wafuasi wake kujiunga na ACT-Wazalendo, kila kukicha anaamsha chokochoko hii na ile.

Inashangaza sana msomi ya daraja ya juu mtaalamu wa uchumi, aliyekwisha kuzifanyia kazi serikali na taasisi za kimataifa, akajigeuza ngumbaro na kujidhalilisha kwa wasomi wenzake na watu wengine. Aibu kubwa isiyowahi kutokea popote duniani.

‘Mungu si Athamani na shari huzaa kheri’

Nimesema kwamba ‘Mungu si Athamani na kheri imo ndani ya tumbo la shari.’ Iwapo Msajili wa Vyama vya Siasa, Francis Mutungi kama atakifuta ACT-Wazalendo, ajue kuwa bado vyama venye sura ya upinzani wa kweli vipo. CHADEMA ipo, NCCR-Mageuzi ipo NLD ipo na kadhalika, atafuta vingapi?.

Ili tuamini kama alivyotangaza Magufuli kuwa hadi ikifika 2020 atahakikisha hakuna upinzani. Hapo tutaamini kuwa anayofanya Francis Mutungi, kufuta vyama anatekeza agizo hilo.

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) inakutana leo Jumamosi, ili kupokea taarifa na kujadili mwenendo wa hali ya siasa nchini.

Kikao kinafanyika Dar es Salaam, chini ya mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na naamini moja katika ajenda za kikao hicho suala la tishio la Msajili wa Vyama, Francis Mutungi litajadiliwa japo kwa muhtasari na hatua za kujipanga kuipokea ACT-Wazalendo, litakuwa ni sehemu ya moja ya ajenda.

Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa (March 29) na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema kikao hicho kitakuwa cha siku moja.

“Kamati Kuu ya Chadema itakutana katika kikao chake maalum Jumamosi, mjini Dar es Salaam kupokea taarifa na kujadili pamoja na masuala mengine, mwenendo na hali ya siasa nchini,” alisema Makene.

Binafsi, naamini kuwa upinzani hususan ACT-Wazalendo na Chadema vinakabili na hali ngumu chini ya utawala wa Magufuli, lakini sina shaka vitaweza ku-survive.

Kila mtu anajuwa na hasa kwa wale wanaofuatilia siasa za Tanzania na uongozi wa Rais Magufuli anavyozitumia taasisi za uma kuvunja katiba na sheria kuivuruga nchi kuna kila dalili kwamba ACT-Wazalendo, kinafutwa.

Kwa hili naweza kusema ‘ya Mungu mengi’ endepo kitasalimika kufutwa basi itakuwa ni kwa manusra yake Mwenyezi Mungu. Kauli za Magufuli na vitendo vyake ni tofauti.

Hapa namnukuu tena Maalim Seif

Mwanachama mpya (kadi No. 1) wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatua zinazochukuliwa dhidi ya chama hicho zinamlenga yeye binafsi: “madam niko hai sitakubali kunyamazishwa.”

Maalim Seif alikuwa anakumbusha hatua ya hivi karibuni ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukiandikia barua chama cha ACT-Wazalendo, akieleza nia ya kukifuta.

Alimtaja waziri wa mambo ya ndani, Kangi Lugola kupiga marufuku ziara ya chama hicho Zanzibar, ingawa ilikuwa imemalizika.

Maalim Seif ambaye ni muanzilishi wa chama chake cha zamani cha CUF, alisema kuna watu wana woga naye na wengine wana “personal vendetta” (chuki binafsi).

Narudia: Akizungumza Dar es Salaam, Alhamisi March 28, Maalim Seif alisema kuna watu wana chuki naye na wala si ACT-Wazalendo ambayo ilikuwapo, lakini haijawahi kufanyiwa yanayotokea sasa.

Alisema hata barua ya msajili kutishia kuifuta ACT-Wazalendo imeibua suala la miaka mitano nyuma na kupenyeza jingine tete la kidini ambalo kwa busara halikupaswa kuibuliwa.

Katika barua hiyo ya March 25, msajili alidai “wafuasi wanaodhaniwa kuwa ni wa Maalim Seif walitumia neno Taqbir wakati wanapandisha bendera ya ACT-wazalendo.”

Alipoulizwa kama anadhani kuna mpango wa kufuta chama hicho, Maalim Seif alisema uwezekano huo upo kwa kuwa yameshafanyika mambo mengi.

“Hatuwezi kusema (msajili) hawezi kuifuta ACT. Akiifuta tutajua la kufanya. Wasidhani watamnyamazisha Seif, madam niko hai sitokubali kunyamazishwa,” alisema Maalim Seif.

Kuhusu madai kuwa wafuasi wake wamechoma bendera na kubadili ofisi za CUF, Maalim Seif alisema hawakufanya fujo zozote, bali baada ya mkutano mkuu kumfukuza yeye na viongozi wengine, baadhi ya wafuasi waliungana nao kutafuta jukwaa jingine la kisiasa.

Alisema majengo mengi yaliyokuwa yanatumiwa na CUF Zanzibar, isipokuwa ofisi mbili za Mtendeni na Kilimahewa ni mali ya watu binafsi na kama wameamua kuhama chama, hawakuwa na sababu ya kuacha alama wala nembo za CUF.

Kuhusu samani za ofisi hizo, alisema hakukuwa na samani ambazo ni mali za CUF. “Mfano ni katika ofisi yangu, kila kilichokuwamo ni mali yangu binafsi,” alisema huku akisisitiza kuwa hata ruzuku ilikuwa inatolewa kwa upande wa Profesa Lipumba kwa miaka zaidi ya miwili.

“Nilimwandikia CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kwamba hakuna fedha za ruzuku ninazopata kwa hiyo sihusiki nazo kwa lolote” alisema Maalim Seif.

Pamoja na hukumu mbili za mahakama kuu zilizotolewa na Jaji Benhajj Masoud Aliwashauri Watanzania waendelee kuwa na imani na mahakama kwa kuwa huko ndiko matumaini yaliko.

Naamini kuwa Mungu si Athumani na kheri imo ndani ya tumbo la shari, yanayofanywa sasa na Rais John Magufuli dhidi ya viongozi wa upinzani, wafuasi wao na wananchi ni dalili za kheri..

Share: