Habari

Mtatiro ajiondoa CUF, ajipeleka CCM

Julius Mtatiro akitangaza kujiondoa CUF na kujiunga na CCM Dar es Salaam Jumamosi, Agosti 11, 2018. Picha na Said Khamis

By Elias Msuya na Bakari Kiango – Mwananchi
Sunday, August 12, 2018

Upinzani umepata pigo jingine baada ya Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa CUF upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kujiengua na kujipeleka CCM.

Mtatiro aliyekuwa akiwashangaa na kuwabeza viongozi wa upinzani na wanachama wanaohama na kwenda CCM, jana Jumamosi, Agosti 11, 2018 aliomba kujiunga na chama tawala CCM.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, mara kwa mara amekuwa akiandika makala mbalimbali za kuikosoa serikali kupitia vyombo vya habari, alitangaza uamuzi huo katika mkutano wake na wanahabari mjini Dar es Salaam.

Mtatiro alisema ameamua kujivua uanachama na uongozi wa CUF baada ya kuangalia na kutafakari kwa mwezi mmoja.
Alisema kilichomfanya aondoke CUF ni pamoja na mgogoro ndani ya chama hicho.

Mtatiro alisema alijipa muda wa kutosha kufanya uchambuzi wake pamoja na kuwahusisha marafiki, washauri wake na familia yake.

“Baada ya kujitafakari kwa mwezi mmoja, Agosti 8 mwaka huu nilimuandikia barua rasmi Maalim Seif kuhusu lengo la kujivua uanachama na nyadhifa zangu zote ndani ya CUF. Kutojibiwa kwa barua yangu hakuniondolei wala kubadilisha msimamo wangu wa kuondoka,” alisema Mtatiro.

Mtatiro alimtakia kila heri Maalim Seif katika mapambano na kurejesha hadhi ya CUF, huku akiiomba CCM kumpokea ili amsaidie Rais John Magufuli kutatua kero za Watanzania.

Alisema anakwenda CCM kama mwanachama wa kawaida, hafuati vyeo, hajanunuliwa kwa sababu hana bei na hakuwahi kuwasaliana na viongozi wa chama hicho tawala kuhusu uamuzi wake huo wa kujiunga na chama hicho.

“Hii ni kama surprise (mshtuko) tu leo (jana Jumamosi, 11/8/18), ndiyo maana nawaomba CCM wanipokee. CCM ndiyo sehemu sahihi kwangu na hitaji la moyo wangu limejiridhisha,” alisema Mtatiro.

Alisema ametumia kidogo uwezo wake wa uongozi katika kuchochea maendeleo ya nchi pindi akiwa CUF na kuanzia sasa anaanza kulisaidia Taifa, Serikali na Watanzania kwa kutumia kipaji na uwezo huo.

“Nimejiridhisha Watanzania wana matatizo mengi na yanahitaji watatuzi. Baadhi ya watatuzi hao ni wenye uwezo na vipawa binafsi nikiwemo mimi, ambapo hatuna majukwaa muafaka ya kufanya hii kazi, nimejiridhisha,” alisema Mtatiro na kuongeza:

“Nawajulisha Watanzania kuanzia leo (jana Jumamosi, 11/8/18), nitaanza kufanya siasa za vitendo, maendeleo, kujitolea kwa hali na mali na kuishauri serikali pamoja na rais na watendaji wake kwa njia muafaka na kwa ukaribu zaidi.”

Mtatiro ambaye aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), alisema misimamo na sera aliyokuwa nayo ndani ya CUF ameiacha ndani ya chama hicho, badala yake atafuata miongozo na misimamo ya CCM endapo atakubaliwa kujiunga nayo.

“Nina uwezo wa kusimamia misimamo ya CCM na nitaifuata, lakini ninavyozungumza hivi sasa mimi ni Mtatiro, sera na misimamo yangu nimeacha CUF,” alisema Mtatiro.

Alisisitiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, inasimamia kwa juhudi kubwa ajenda ya maendeleo ambayo mara kwa mara ilikuwa ikipigiwa kelele na wapinzani akiwamo yeye wakati yupo CUF.

“Tafiti zinaonyesha hali ya rushwa kubwa kubwa hapa Tanzania zimepungua sana. Sasa hivi watu wanaohisiwa na masuala ya rushwa au kuiba fedha wanachukuliwa hatua za kisheria, lakini huko nyuma walikuwa hawakamatiki.”

Alisema baada ya tafakuri hiyo ya mwezi mmoja ameamua kuanza kazi kubwa ya kumsadia Rais Magufuli kuendelea kutatua matatizo ya Watanzania na hatamtendea haki endapo hatashiriki kikamilifu.

“Nimeamua kwa dhati kuanzia sasa kuwa mmoja wa mabalozi wakubwa wa taifa langu na wa Rais Magufuli,” alisema Mtatiro na kusisitiza:

“Kazi hii nitaifanya kwa vitendo na maneno na imani ndani ya nchi na nje na sitasita, nimeona nina potential ya kusaidia nchi na maendeleo ya taifa.”

Wapinzani watoa ya moyoni
Wakizungumza kwa njia ya simu na Gazeti la Mwananchi, baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani walisema kuondoka kwa Mtatiro ni wimbi la makada wa vyama hivyo kwenda CCM linalotokana na mkakati wa chama tawala kuua upinzani.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Zanzibar), Nassor Mazrui alihusisha kuondoka huko na vitendo vya rushwa ya kisiasa.

“Rushwa ya siasa ni mbaya kuliko rushwa ya uchumi. Nchi yetu inapitia katika kipindi kigumu cha kiuchumi, lakini sasa tunaona tena rushwa ya siasa.”

“Hii ni baba na mama wa rushwa zote. Wanachofanya ni kujipalilia makaa ya moto kama anavyofanya pweza,” alisema Mazrui.

Alisema aliwasiliana na Mtatiro siku tano zilizopita ambapo alimjulisha kuwa anakwenda kushughulikia madiwani wa chama hicho wanaotaka kuhamia CCM, lakini hakumjulisha kuhusu kuhama chama.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema ameshtushwa kusikia taarifa hiyo.

Alisema hatua hiyo ni wimbi la viongozi wa upinzani kuhamia CCM linalofanywa kuua nguvu ya kambi ya upinzani, jambo ambalo hawakubaliani nalo.

“Mimi siangalii CUF, wala CHADEMA wala chama gani. Ninachoangalia ni ukuaji wa demokrasia, naangalia tangu wakati wa Mwalimu Nyerere aliyeasisi mfumo wa vyama vingi.”

“Lengo la vyama vya upinzani ni kuleta demokrasia na kuwa na dira katika nchi,” alisema Sakaya.

Aliongeza, “Suala siyo Mtatiro tu, bali haya ni maangamizi ya upinzani. Nimekuwa nikiwaambia CHADEMA wasiinyooshee tu kidole CUF kumbe vile vinne vinawanyooshea wenyewe.”

“Kwa sasa wabunge, madiwani na viongozi wa upinzani wanahamia CCM, hali ni mbaya. Mimi nataka tuwe na upinzani wenye nguvu.”

Sakaya ambaye wakati wa mgawanyiko wa CUF alibaki kundi la mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kama ni kuhamia CCM angeshahamia siku nyingi, bali hataki kwa sababu anataka kujenga upinzani imara.

“Tangu mwaka 2006 nilipoingia bungeni kwa mara ya kwanza CCM walinishawishi sana nihamie kwao baada ya kuona uwezo wangu. Nilikataa kwa sababu nataka tuwe na upinzani imara, niliwauliza hivi wote tukihama nani ataikumbusha serikali wajibu wake?”

Alisema licha ya mgawanyiko wa chama chao, bado anaamini kundi linaloongozwa na Maalim Seif litarejea na kujiunga na mwenyekiti wao.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), John Mnyika alisema wimbi la viongozi wa upinzani kuhamia CCM lilishatangazwa.

“Nimekutana na Mtatiro mara kadhaa na nilibaini kwamba alishaanza kukata tamaa na kupata tamaa. Hivyo hatua yake ya leo haijanishangaza.”

“Mwito wangu ni wote tunaotaka kuiondoa CCM madarakani na kuleta mabadiliko nchini tusirudi nyuma pamoja na magumu tunayopitia,” alisema Mnyika.

“Kwa upande wa CUF kama taasisi, kinara wa chama hicho katika uongozi wake ni Katibu Mkuu Maalim Seif, hivyo kuhama kwa Mtatiro hakuwezi kuteteresha Ukawa.”

Akifafanua zaidi, Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Kibamba alisema kwa sasa mahitaji ya kupata katiba mpya yameongezeka, hivyo kuhama kwa viongozi hao hakutawayumbisha.

Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe alisema wimbi la wapinzani kuhamia CCM halitaua upinzani nchini kwani uko mioyoni mwa wananchi.

“Kwanza ni vigumu mpaka ikifika mwaka 2020 wapinzani wote kuwa wamepukutika. Upinzani siyo mtu mmoja ni watu wengi. Hata kama mtu mmoja kaamua kutundika daluga kwa sababu ya njaa zake, basi wataibuka wengine wengi, hata kama sisi hatutakuwepo,” alisema Zitto.

“Hili wimbi litapita tu, ni kama tuko kwenye treni tunasafiri, huyu atashuka Morogoro, huyu atashukia Zuzu, huyu atashukia Sekenke, mwingine atashukia Kazuramimba, lakini lazima treni ifike.”

Wakati huohuo, mwenyekiti wa madiwani wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Isaac Joseph amejiuzulu na kuhamia CCM.

Pia, CHADEMA wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa jana ilimvua uanachama diwani wa Majengo, Dickson Mwanandenenje kwa madai ya usaliti.

Gazeti hilo hilo la Mwananchi la leo Jumapili, Agosti 12 kupitia mwandishi wake, Peter Elias limeandika habari yenye kichwa kisemacho CUF wamshukia Mtatiro, wadai ndiye chanzo cha migogoro.

Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Taifa, Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro kutangaza kuhamia CCM, Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa chama hicho, Abdul Kambaya amesema zaidi ya asilimia 70 ya migogoro ndani ya chama hicho imechangiwa na Mtatiro.

Mtatiro aliyekuwa upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, jana Jumamosi Agosti 11, 2018 alitangaza kuachana na chama hicho na kujiunga na CCM.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Agosti 12, 2018 Kambaya ambaye yupo upande unaomuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba amesema Mtatiro akiwa mwenyekiti wa mkutano mkuu alisababisha chama hicho kugawanyika kwa kutosikiliza maoni ya wajumbe wa mkutano huo na kuamua kuuendesha kibabe.

Amesema Mtatiro akiwa naibu katibu mkuu alikiingiza chama hicho katika mgogoro uliosababisha Hamad Rashid kufukuzwa uanachama baada ya kuhoji ubadhirifu wa fedha kiasi cha Sh300milioni katika uchaguzi mdogo wa ubunge Igunga.

“Hakuna kitu ambacho Mtatiro amekifanya kwenye chama hiki, kubwa zaidi amesababisha migogoro. Wanasiasa wapambanaji hawakimbii migogoro ndani ya vyama vyao bali wanakaa humo humo mpaka migogoro itakapokwisha,” amedai Kambaya.

“Tazama Sophia Simba hakukimbia CCM sambamba na Nape Nnauye (mbunge wa Mtama-CCM). Hata Mnyika (John Mbunge wa Kibamba-CHADEMA) hakukimbia chama hicho,” amesema Kambaya.

Share: