Habari

Mtatiro amaliziana biashara na CUF, ajiunga CCM

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro…kama kawaida ni muendelezo wa Watanganyika wenye misimamo dhaifu katika siasa za Tanganyika upande wa upinzani..

Dar es Salaam, Tanzania
Jumamosi, Agosti 11, 2018

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ametangaza kujiondoa kwenye chama hicho na sasa kuanzisha biashara mpya na CCM.

Akizungumza Dar es Salaam leo Jumamosi, Agosti 11, 2018 na waandishi wa habari, Mtatiro alisema ametafakari kwa miaka zaidi ya kumi aliyofanya siasa na kugundua kwamba umefika wakati wa kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

“Masuala ya misimamo yangu ya sera na ilani ya CUF na misimamo ya CUF hayo yanabaki CUF, hivi sasa mimi ni Mtatiro ambaye ninajiandaa kuhamia CCM, kama mwananchi ninayo haki kikatiba,” alisema Mtatiro.

Alisema amejiridhisha kwa matakwa ya nafsi yake kwamba ajiunge na CCM na alisema anawajulisha watanzania kuwa ameanza mipango ya kutekeleza hilo haraka.

Alisema hajanunuliwa wala kurubuniwa na CCM bali ameitumia siku ya leo kuonyesha nia yake ya kuhamia CCM na kuomba wampokee.

Lakini alisema kuwa huu ni wakati wake wa kwenda kutumia vipaji vyake kikamilifu pia kuwa balozi mkubwa wa Rais Magufuli ndani na nje ya Nchi.

Mtatiro alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kwa kuwa jukwaa alilokuwa analisimamia katika siasa kwa miaka kumi limeshindwa kumpa nafasi yakuifanyia nchi yake maendeleo.

Katika hatua nyingine baada ya kutangaza nia hiyo Mtatiro ametoa ahadi yakuwatumikia watanzania pamoja na kupambana na umasikini. Alisema uamuzi alioufanya sio kwa ajili yakutafuta cheo.

Muda mfupi baada ya kutangaza uamuzi huo, wanasiasa mbalimbali wakiwamo Zitto, Bashe, Nape na Polepole waliibuka na kuandika kwenye mitandao ya kijamii wengine wakimpongeza na wengine wakimkosoa.

Mbunge wa Kigoma Mjini, (ACT-Wazalendo) Zitto Kabwe ameandika kwenye ukurasa wake wa Twita ameandika akisema:

“Huko wanakokutegea kukufukuza kila usemapo ukweli? Ninaamini kwenye maendeleo ndani ya demokrasia na siyo maendeleo ndani ya udikteta.”

“Ninaamini katika uhuru wa fikra na siyo mawazo ya kiimla. Ninaamini nchi yetu inahitaaji chama kingine kuirudisha kwenye reli. Nafasi ya CCM ni Museum (makumbusho),” ameandika Zitto.

Mbunge wa Nzega, (CCM) Hussein Bashe ameujibu ujumbe wa Zitto akisema:

“Ni rahisi kuleta mabadiliko ya haki, demokrasia na maendeleo ndani ya CCM) kuliko kutafuta mabadiliko nje kwa sababu kuna mgogoro wa kimawazo, kimuundo na kimadili huko nje. Kuna wanajeshi wachache wa ukweli.”

Kwa upande wake, Nape Nnauye Mbunge wa Mtama (CCM) ameandika akisema:

“Tunachagua rangi ya Paka wakati shida yetu ni kukamata Panya. Nguvu tunayopoteza kuhoji rangi ya paka ingetumika kushughulika na panya tungekuwa mbali sana.”

Nape katika nukuu yake nyingine ameandika akisema:

“Kama msomi wa Sayansi ya Siasa, naona hii ni fursa muhimu ya kujengwa kwa aina mpya ya vyama na siasa za upinzani nchini.”

“Kwa demokrasia, hamahama hii muhimu itumike kama fursa ya kujenga upya uimara wa CCM unaotegemea ubora wa upinzani (Simba/Yanga),” huyo ni Nape Nnauye.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole yeye ameandika:

“Huu unaitwa uhuru wa kisiasa kwa mujibu wa katiba yetu, halafu wale wa ‘siasa za bei nafuu mseme kanunuliwa.” Hongera kaka, ndugu, kamaradi.”

“Historia na Mungu pekee atakupa tuzo ya dhamira yako njema. Na mimi nimeikuta mtandaoni,” Polepole.

Wakati huo huo katika ‘facebook’ baadhi ya watu wametoa maoni kuhusu aliyekuwa Mwenyekiti wa ‘Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro kujiondoa kwenye chama hicho, leo Jumamosi, tarehe 11/8/2018.

Sa Elieshi Shuma, anasema: “Pamoja na lipumba kuwa msaliti hajahama chama mtatiro kamzidi lipumba.” anajibiwa na

Salah Al Asad, anasema: “Ni bora adui wa nje kuliko wa ndani..lipumba ni mbaya zaidi ya mtatiro…lipumba bado anatumika kuiua cuf..sasa mtatiro hatokuwa tena mwanacuf wala kuvuruga cuf.”

Salim Mussa Omar, “Hilmi karibu ccm jahazi inaondoka kaka hii acha ushabiki kaka yangu njoo hukuuuu.”

Naye Hilmi alijibu:

Hilmi Hilal Kaka Salim Mussa Omar mimi sipiganii tumbo. napigania uhuru, haki na usawa, naipigania Zanzibar sipiganii chama. Hivyo utasahau wala haitokuja kutokea kuuza utu wangu kwa kuendekeza tumbo.

Hamza Ali Moyo: watamaa hauna kumbukumbu aliwazalo mjinga ndio humtokea. Frank John kaandika: Nae kala matapishi yake!! kuwaamini wanasiasa ni kazi ngumu sana..imani yangu kwa Mbowe, Lisu, Maalim Seif, Lema, etc..

Mwingine kutoka Zanzibar, ameandika hivi:

“Siyo kazi sana kuweza kuwafahamu ndugu zetu wa Tanganyika katika masuala ya siasa na wanachokitafuta. Hoja za Watanganyika ni tofauti na hoja au madai ya Wazanzibari ndani ya siasa za Tanzania.”

Mzanzibari mmoja ambaye hakutaka kutaja jina, kaandika baada ya Mtatiro kujiondoa CUF na kuonesha imani yake kwa asilimia mia moja ya kujiunga na CCM.

Anasema: “Hawa ndio watanganyika tunaowaamini na kuwapa mapenzi yetu kwa kushirikiana nao na tukawaona kuwa ndio wenzetu.”

Anasema: “CUF wana mdorongo wa kesi mahakamani na mtu huyu ndiye aliyekuwa na nafasi kubwa na muhimu kwa uongozi wa CUF.”

Anasema: “ndiye huyu aliyejinadi na pia akawa ni silaha ya kukisaidia chama kwa madhila na maovu ya ndugu Lipumba na pia na kuzawadiwa nishani.”

“Leo hii huyu juu ya jamvi mchana kweupe Mtatiro anakula matapishi yake. Hawa ndio watu tunaowaamini na ndio wenye siri za chama.”

Anasema: “Mimi huwa namsemo ambao hupenda kuukariri, kuwa kisiasa wabara kwao ni maslahi, kwa sababu wana nchi na uhuru wao kamili, lililobaki ni kujiimarisha kimaendeleo.”

Anaongeza: “Lakini kwetu sisi Zanzibar, tunakazi kubwa ya kupigania uhuru wa nchi yetu ndani ya serikali ya Tanganyika inayojiita Tanzania.”

“Hizo ndio siasa za maslahi, la msingi ni kuendelea kujipanga na kujikwamua pale tulipojikwaa, lakini chama cha CUF, umefika wakati wa kujitafakari upya kwa mikakati yake,” anamaliza.

Mohammed Ghassani: “Ushauri wa bure kwa wajao. Siku hizi kabla ya kutangaza kuunga mkono juhudi, kwanza pitia akaunti zako zote za mitandao ya kijamii na fyagio la chuma.”

“Maana hata kama unajifanya hujali, bado wewe u mtu. Una roho. Una hisia. Una ubongo. Miye naanza kufuta vyangu nikiwa njiani kuelekea Peacock kukutana na wanahabari.” huyo ni Mohammed Ghassani kwenye ‘facebook’ leo.

Mohammed Amour , kwenye ukursa wa ‘facebook’ kaandika: “Njaa haijawahi kumuacha mtu Salama na ndio maana Waislamu tukaamrishwa tufunge ili tupate IBRA. ona yanayowakuta Watanganyika!”.

Share: