Habari

Mtatiro azungumzia saa 17 za mahojiano yake na Polisi Dar

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro

By Fidelis Butahe, Mwananchi
Sunday, July 8, 2018

Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro amesema mbali na kuhojiwa kwa saa 17 na polisi akituhumiwa kumkejeli Rais John Magufuli, askari waliofanya upekuzi nyumbani kwake walichukua simu, kifaa cha kurekodi sauti na ‘flashi diski’ tatu.

Mtatiro alisema pia walichukua Ipad yake aliyoitumia kuandika ujumbe unaodaiwa kumkejeli kiongozi huyo mkuu wa nchi na kubainisha kuwa walitaka awape kadi zake za simu lakini aliwagomea kwa maelezo kuwa hazihusiani na tuhuma zinazomkabili.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uongozi ya CUF, aliripoti kituo kikuu cha polisi cha Dar es Salaam, siku ya Alhamisi, Julai 5 asubuhi na kuhojiwa hadi Ijumaa jioni, Julai 6, alipoachiwa kwa dhamana akituhumiwa kuandika ujumbe katika mtandao wa Facebook unaosema ‘rais kitu gani bwana’.

Hata hivyo, siku ya Alhamisi, Julai 5, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Liberatus Sabbas alisema hana taarifa za kukamatwa kwa mwenyekiti huyo wa kamati ya uongozi ya chama hicho.

“Sijui lolote kuhusu hilo suala,”alisema Sabbas kwa kifupi alipoulizwa na Mwandishi wa Gazeti la Mwananchi kuhusu suala la kukamatwa kwa Mtatiro.

Akizungumza na Gazeti la Mwananchi Ijumaa, Julai 6, Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma wa CUF, Mbarala Maharagande alisema Mtatiro mbali na kukamatwa na kuhojiwa, alipelekwa nyumbani kwake kupekuliwa na kurejeshwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Alisema Mtatiro amekamatwa kutokana na ujumbe alioutuma katika ukurasa wake wa Facebook unaodaiwa kumkejeli Rais John Magufuli. Alisema mwenyekiti huyo katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook ameandika, ‘Rais kitu gani bwana’.

Maharagande alisema: “Juzi (Jumatano, Julai 4) Mtatiro alipokea simu ya wito wa kuhitajika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam. Jana (Alhamisi, Julai 5) alikuwa amealikwa kama mmoja wa wageni wawezeshaji wa mjadala wa taasisi ya Twaweza katika kongamano la kujadili maoni ya wananchi kuhusu kushiriki maandamano na siasa.”

“Ilipofika saa tatu asubuhi akiwa anaelekea huko alipigiwa simu kujulishwa afike kituoni hapo saa nne asubuhi,” Maharagande alisema.

“Niliambatana naye mpaka kituoni hapo na tulipokelewa na Kamanda wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) na kujulishwa kuwa anahitajika achukuliwe maelezo yake kuhusu ujumbe alioutuma katika mtandao huo.”

Maharagande alisema, “Tukakabidhiwa maofisa wa polisi wa kufanya kazi hiyo. Wakati wa kuanza kuchukuliwa maelezo yake alielezwa kuwa anatuhumiwa kwa kutuma ujumbe wa kejeli na kashfa dhidi ya Rais Magufuli kupitia mtandao wa kijamii.”

Alisema kuwa Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uongozi ya CUF upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad alichukuliwa maelezo hadi saa 10 jioni kabla ya kupelekwa nyumbani kwake kwa upekuzi.

Alisema walirejea tena kituoni hapo saa 4 usiku na maofisa wa polisi walimueleza kuwa wataendelea kuwa naye mpaka leo asubuhi (Ijumaa Julai 6): “Walisema watatujulisha kama watampatia dhamana au vinginevyo.”

Akizungumza na Gazeti la Mwamananchi jana (Jumamosi, Julai 7) Mtatiro alisema: “Alhamisi nikiwa naelekea katika mjadala wa taasisi ya Twaweza nilipigiwa simu na ZCO (Kamanda wa Upelelezi wa Kanda) kuwa nahitajika kituo kikuu cha polisi. Niliitikia wito na nilipofika nikaelezwa nimeandika ujumbe huo wa kumkejeli rais.”

“Ujumbe ule uliandikwa na kijana mmoja Misungwi ambaye ameshtakiwa mahakamani kwa kumtukana rais kwa kusema ‘rais kitu gani bwana’, mimi nilishangazwa na jambo hilo na niliandika kitu na kisha nikarejea alichokisema kijana huyo.”

Alisema alichokiandika si kosa ni swali alilohoji kupitia mtandao huo na kuwa alipofika kituoni hapo alihojiwa kwa saa saba na kisha kuwaongoza askari hadi nyumbani kwake ambako walimpekua.

“Walichukua simu yangu moja, flashi diski zangu tatu pamoja na kifaa cha kurekodia sauti. Ila nilivyokwenda kituoni nilikuwa na Ipad yangu niliyotumia kuandikia ujumbe huo mtandaoni, nayo waliichukua,” alisema Mtatiro.

Alisema: “Siku iliyofuata (Ijumaa) nilihojiwa kuanzia asubuhi hadi saa 10 jioni na kuachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti tena kituoni hapo Jumatatu (Julai 9) saa 2 asubuhi.”

Alisema akiwa mahabusu kituoni hapo, alitoa ushauri kwa vijana 16 wanaoshikiliwa kwa tuhuma mbalimbali na kubainisha kuwa wengi mashtaka yao yana dhamana na wengine kwa tuhuma zao hawapaswi kuwekwa ndani.

Alisema: “Vijana wawili kati ya niliowapa ushauri wa kisheria, wamenipigia simu kuwa wameachiwa huru. Kwa kweli nilichokibaini watu wengi wanaonewa, kwa kweli.”

Alisema katika mahojiano hayo, walimtaka awapatie kadi zake za simu, lakini aliwagomea kwa maelezo kuwa kadi hizo hazihusiani na tuhuma zinazomkabili.

“Hili la kuwapa kadi zangu za simu kwa kweli sikulikubali kwa kuwa halihusiani na wanachonituhumu,” alisema Mtatiro.

Alisema jambo lililompata ni mwendelezo wa watu wa kada mbalimbali kuminywa kutoa maoni yao katika mambo mbalimbali.

“Uhuru wa kutoa maoni watu wamezaliwa nao. Nadhani kadri inavyotumika nguvu kuzuia watu kutoa maoni yao ndivyo wanavyozidi kuwakomaza,” alisema Mtatiro.

Julius Mtatiro anakuwa mwanasiasa wa tatu kuhojiwa na kitengo cha mtandao cha polisi. Wanasiasa wengine waliowahi kukumbwa na kadhia hiyo ni Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini.

Share: