Habari

Mtikila Adhamiria Kuiburuza Serikali Mahakamani

Na Moshi Lusonzo

17th August 2014

MWENYEKITI WA CHAMA cha DP, Mchungaji Christopher Mtikila ameanza zoezi la ukusanyaji saini za Watanzania kwa ajili ya kuifikisha serikali mahakamani kwa kukataa kusitisha Bunge Maalum la Katiba.

Hata hivyo, Mchungaji Mtikila ametangaza rasmi kuachana na kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) akisema wametofautiana kimtazamo.

Akizungumza na NIPASHE mjini Dar es Salaam, Mtikila alisema tayari ukusanyaji wa sahini hizo umeanza kwa baadhi ya mikoa na itakapokamilika atafungua shauri Mahakama Kuu, akitaka Bunge hilo linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma, lisimamishwe haraka.

Alisema kwa upande wake hana ndoto za kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na kuzidiwa na kazi hiyo pamoja na kuona katiba itakayopatikana haitakuwa halali kwa Watanzania.

Alisema: “Nimekuwa na kazi ngumu ya kutetea Tanganyika, nitapita kila sehemu ya nchi kwa ajili ya kukusanya saini zao ili kile tunachopigania tupatiwe bila shuruti,”.

Akielezea tofauti za kimtazamo kati yake na wajumbe wengine wa UKAWA, Mchungaji Mtikila alisema yeye alikuwa mmoja wa waanzilishi wa kundi hilo, lakini ameshindwa kuelewana kutokana na ukinzani wa kimtazamo wa muundo wa serikali.

Alisema wakati yeye anataka kuwa na serikali ‘Huru ya Tanganyika’, wenzake wanaamini uwepo wa serikali tatu ndani ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, alisisitiza kutorejea bungeni licha ya kuamua kukaa pembeni na kundi hiilo.

Hivi karibuni umoja huo umejikuta ukiwa katika mgawanyiko wa kimawazo baada ya baadhi ya wabunge wa CHADEMA kuamua kurejea bungeni na kukiuka uamuzi uliopitishwa na viongozi wa Vyama vya upinzani vinavyounda UKAWA.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Share: