Habari

Mungiki waleta Wasomali kuhujumu CUF Zanzibar

Na Mwandishi Wetu

Taarifa kutoka ndani ya kundi la wafuasi wa Prof. Ibrahim Lipumba, maarufu kama Mungiki, zinasema kwamba kwa kushirikiana na kiongozi mmoja wa juu kabisa kwenye Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na pia mtoto wa kiume wa aliyekuwa rais wa Zanzibar wakati nchi inaingia kwenye vyama vingi, kundi hilo limeingiza kundi la raia wa Kisomali kwa ajili ya kufanya hujuma katika ofisi za CUF – Chama cha Wananchi kisiwani Unguja.

Mpasha taarifa wetu, ambaye mwenyewe ni sehemu ya Mungiki hao lakini asiyependezewa na hatua ilipofika sasa, ametuthibitishia kwamba Wasomali hao waliwekwa kwenye nyumba moja eneo la Mbweni , kando kidogo ya mji wa Zanzibar na kisha kuhamishiwa kwenye nyumba nyengine iliyopo Dunga, katikati ya kisiwa cha Unguja, tayari kwa kufanya operesheni yenyewe, ambayo lengo lake ni kukiona chama cha CUF kikifutwa kwa tuhuma za ugaidi.

“Kilichopangwa kufanywa hasa ni kuingiza miripuko kutoka Gongo la Mboto katika ofisi za CUF. Aidha ya Mtendeni, au ya Vuga au ya Kilimahewa. Tena mipango ni kwamba isubiriwe siku ambayo Maalim Seif (Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad) au Mazrui (Naibu Katibu Mkuu Nassor Ahmed Mazrui) wamo ndani kwenye ofisi hizo, kisha utafanyika uvamizi wa vikosi vya usalama. Watasema wamekamata miripuko hiyo, viongozi hao watawekwa ndani na kisha hao Wasomali wataoneshwa kwenye televisheni wakidai kuwa waliileta wao kwa kutumwa na viongozi wa CUF,“ kilitufafanulia chanzo hicho.

Alipoulizwa ni nani hasa wanahusika na mpango huo ndani ya kundi la Mungiki, aliwataja watu wawili mahsusi kabisa, ambao ni aliyekuwa mkuu wa ulinzi wa CUF, Thiney Juma Mohamed, na aliyekuwa msaidizi mshika fedha, Said Omar maarufu Vibega, ambao wote wawili walifukuzwa kwenye nafasi zao kabla ya kujiunga na akina Profesa Lipumba.

Kwa upande wa wanaohusika na mpango huo upande wa serikalini, mpasha taarifa wetu amesema kuwa ni kiongozi mmoja mkubwa bila kumtaja jina, lakini akisema kuwa ndiye pia aliyehusika moja kwa moja na kukamatwa kwa viongozi wa Jumuiya ya Kiislamu ya Uamsho, ambao hadi leo wameshikiliwa kwenye magereza ya Tanzania Bara zaidi ya mwaka wa nne sasa.
“Mimi ninatafautiana na Maalim Seif na wenzake. Lakini baada ya yote mimi ni Mzanzibari na ni Muislamu. Haya ni mambo ya kisiasa tu. Siwezi kukubali kuona kuwa nchi yangu sasa inatumbukizwa kwenye upuuzi huu wa kigaidi. Tunawaalika Wasomali ambao nchi yao wameshaiangamiza kwenye suala letu hili. Wataimaliza na hii yetu,” alisema mpasha taarifa huyo alipoulizwa kwa nini anaiweka hadharani mipango ya wenzake.

Hujuma za aina hii ni maarufu visiwani Zanzibar, zikiwa zinahusishwa moja kwa moja na vyombo vya dola na chama tawala cha CCM. Miripuko imewahi kuripotiwa na hata kufanyiwa uchunguzi na vyombo vya usalama kutoka Bara na nje ya nchi, lakini matokeo ya uchunguzi huo hayajawahi kuwekwa hadharani, kwa vile inasemekana ushahidi wote umekuwa ukielekeza vidole kwenye maskani za CCM na nyumba za viongozi wa vikosi vya SMZ.

Hata hivyo, viongozi kadhaa wa CUF na wafuasi wao wamewahi kukamatwa na kuwekwa ndani kwa kutuhumiwa kuwa eti wao ndio wamehusika na miripuko hiyo, akiwemo Mansoor Yusuf Himidi aliyekamatwa kwa kumiliki silaha.

Tangu Profesa Lipumba kuamua kurudi kwenye nafasi ya uwenyekiti wa CUF aliyoikimbia wakati wa uchaguzi mkuu wa 2015, amekuwa akipigania sana kudhibiti madaraka ya chama hicho akisaidiwa kwa karibu na vyombo na taasisi mbalimbali za dola, ingawa mafanikio yake yamekuwa madogo sana kuliko alivyotazamia.

Kesi kadhaa zimefunguliwa mahakamani na upande wake na upande wa CUF, huku kukiwa hakuna njia ya mkato aliyotarajia kuwa angeipita kufikia lengo lake la kukichukuwa chama chote. Wengine wanasema ndio maana sasa yeye na kundi lake wamebakiwa na njia moja tu, ambayo ni kukivunja chama kwa hujuma za kihalifu na kigaidi kama unavyoonekana mpango huu wa Wasomali.

“Ninasema haya kwa kuwa nataka viongozi wa CUF na wanachama wao wote kote Zanzibar, Unguja na Pemba, walinde matawi yao na ofisi zao zote kuanzia leo hii. Huu mpango ni mkubwa na ni wa upo kwenye hatua za mwisho mwisho kabisa. Wakichelewa, chama kimefutwa na Zanzibar nzima inatumbukizwa kwenye janga kubwa kuliko hata hilo la kufutwa kwa uchaguzi wanalopigania sasa,” alionya mpasha taarifa wetu.

Share: