Habari

Mussa Haji: Aratibu upatanishi baina ya Maalim Seif na Lipumba

Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya CUF upande wa Profesa Lipumba, Mussa Haji Kombo anajipanga kuzikutanisha pande mbili za uongozi za Chama cha Wananchi (CUF) ili kukiokoa chama hicho kilichokumbwa na mgogoro kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

By Muhammed Khamis na Haji Mtumwa – Mwananchi
Friday, April 13, 2018

Mgogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) umeanza kuwafikirisha wanachama kuchukua hatua, ambapo vigogo wawili wanaovutana wanatarajiwa kujadiliwa ili kusaka suluhu ya kudumu.

Mgogoro huo ulioifikisha CUF kugawanyika pande mbili, ulikolea zaidi baada ya mwenyekiti anayeungwa mkono na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kurejea uongozini, huku upande wa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ukipinga kurejea kwake.

Kutokana na mgogoro huo, baadhi ya viongozi na wanachama waliamua kukihama chama hicho na kutimkia vyama vingine vya siasa.

Kufuatia mgogoro kufikia hatua mbaya kwa pande husika kuanza kuhasimiana, mjumbe wa Bodi ya Wadhamini upande wa Profesa Lipumba, Mussa Haji Kombo aliwaambia wanahabari mjini hapa jana kuwa, wanatarajia kuzikutanisha pande hizo kupitia kwa wanachama ambao watajadili kwa kina namna ya kumaliza suala hilo.

Alisema mbali na kujadili mgogoro huo, pia wanakusudia kumfikia Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kujadiliana naye kuhusu tofauti baina ya chama chao na CCM zilizojitokeza kabla na baada ya uchaguzi wa Zanzibar.

Kombo alidai kwamba, tofauti ya kisiasa iliyopo Zanzibar baina ya CUF na CCM inaweza kumalizwa kwa viongozi wa juu wa vyama vya siasa kukutana na kufanya mazungumzo kwa masilahi ya vyama na wanachama wao.

Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na kuandaa utaratibu huo wa kukutana na Rais Shein, pia wanaendelea na mpango wa kufanya semina maalumu itakayowakutanisha wanachama na viongozi wao ili kujadili undani wa mgogoro wa chama hicho.

Alisema lengo la semina hiyo ni kuangalia kwa upana mgogoro huo wa muda mrefu wakianzia na historia hadi ulipofikia hivi sasa.

“Kwa kuwa tumeona muda ulishakuwa mwingi na mgogoro bado unaendelea ni bora tuwashirikishe wanachama wetu ili nao waweze kutoa michango yao nini kifanyike ili kupatikana kwa ufumbuzi,” alisema Kombo.

Alisema semina kama hiyo ilifanyika mwishoni mwa 2017 jijini Dar es Salaam pamoja na mwanzoni wa mwaka huu Kisiwani Pemba ambapo wajumbe waliagiza kila jimbo litenge nafasi mbili za vijana ili waweze kutoa michango ya kukijenga chama hicho.

“Tumedhamiria kulifanya hili baada ya kuona kuna watu wengi wakiwamo viongozi wa dini wanataka kupatikana kwa suluhisho la viongozi hao, lakini imeshindikana,” alisema.

Akizungumzia dhamira hiyo ya upande wa Profesa Lipumba kusaka suluhu ya mgogoro uliopo, mkurugenzi wa Habari wa CUF upande wa Maalim Seif, Salim Bimani alisema hawawezi kujibu chochote kwa kile alichokiita kikundi cha Lipumba na siyo wanachama wa CUF.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza kuwepo kwa umuhimu wa pande husika kumaliza tofauti zao ili maisha mapya yaendelee.

“Hivi kwani huu mgogoro hawa mabwana wakubwa wanataka uende mpaka mwaka gani, maana sasa tulishachoka kuwasikia wao tu wanavurugana,” alisema Salim Mansour Jabu.

Mwanaheri Salimin Jecha aliwataka Profesa Lipumba na Maalim Seif kusahau yaliyopita kwa kukaa meza moja kujadiliana mambo yenye manufaa kwa chama na siyo wao. “Inawezekanaje mgogoro ukawa mkubwa na usiishe?” alihoji.

 

Share: