Habari

Muungano mpya wa Zitto Kabwe utaua au utaimarisha UKAWA?..

By Khalifa Said – Mwananchi (Phone: 0716 874 501)
Sunday, Augost 5, 2018

Makubaliano ya hivi karibuni kati ya chama kikuu cha upinzani, CHADEMA na ACT-Wazalendo kwamba vitashirikiana katika uchaguzi mdogo wa Agosti 12 yametajwa kuwa ni kiashiria cha ushirikiano unaotafutwa wa United Democratic Front (DeFront).

Makubaliano hayo yanakuja kufuatia maridhiano ya awali kati ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe yaliofikiwa wilayani Kakonko wakati wa mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (CHADEMA).

Jimbo la Buyungu liko wazi kufuatia kifo cha Mbunge wake kufariki na kampeni zake zinaendelea sambamba na za madiwani wa kata 77 zilizokuwa wazi kutokana na ama kuhama vyama au kufariki dunia.

Katika makubaliano hayo, ACT-Wazalendo itaiunga mkono CHADEMA katika Jimbo la Buyungu na kata zote ambazo za chama hicho cha mrengo wa ujamaa wa kidemokrasia hakina wagombea.

Na CHADEMA yenye mrengo wa kati (siasa za wastani) itafanya hivyohivyo kwenye kata ambazo haikusimamisha wagombea.

Pia, CHADEMA itamuunga mkono mgombea wa udiwani katika Kata ya Gehandu, wilayani Hanang, mkoani Manyara kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.

Wagombea wengine kutoka vyama hivyo viwili kutoka katika kata ambazo hazikubainishwa kwenye makubaliano wataruhusiwa kuendelea na kampeni zao za kujinadi.

Makubaliano hayo ni sehemu ya mkakati wa Zitto kuelekea kile anachokiita ‘The United Democratic Front (DeFront).

Kimsingi ni ushirikiano kati ya vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyama vya ushirika, vyama vya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla ambao Zitto anasema yuko tayari kujitoa muhanga kufanikisha upatikanaji wake.

Zitto (42) anajulikana kwa msimamo wake kwamba nchi inahitaji mabadiliko ya msingi ya kisiasa ambayo kwa maoni yake ni DeFront pekee ndiyo inaweza kuyafanikisha.

Kwa mujibu wa mbunge huyo wa Kigoma Mjini, uundwaji wa DeFront ni muhimu kwa kuwa itakuwa ni kuweka maslahi ya taifa mbele kuliko yale ya mtu binafsi.

DeFront vs UKAWA
Swali moja ambalo majibu yake hayakuwa yamepatikana ni kwamba ni kwa namna gani hiyo DeFront inaenda kuwa tofauti na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)?.

Je, DeFront ni mbadala wa UKAWA katika mchakato mzima wa kujenga maridhiano baina ya vyama?. Kama hivyo ndivyo, kuna kipi cha kujifunza kutoka UKAWA?.

Pamoja na mazuri yake, UKAWA imekutana na misukosuko ya aina mbalimbali.

Ukiacha hatua ya Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa kujiondoa CHADEMA, pia Profesa Ibrahim Lipumba aliyeamua kujiuzulu uenyekiti wa CUF na baada ya uchaguzi kurejea madarakani akidai barua yake ya kujiuzulu haikujibiwa.

Kutokana na uamuzi huo, umoja huo umeendelea kukutwa na jinamizi na mgogoro unaoendelea ndani ya CUF kufuatia hatua ya Lipumba kurudi na kukalia kiti alichoachia mwenyewe.

Mgogoro huo umesababisha CUF kumeguka vipande viwili, kimoja kikiongozwa na Profesa Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kingine cha Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Ukiachilia mbali mgogoro huo, UKAWA pia haijabaki salama kutokana na hali ya sasa ya siasa, inayoelezwa na wachambuzi wa masuala hayo kuwa ni kurudi nyuma kwa maendeleo madogo ya kisiasa na kidemokrasia yaliokwishafikiwa na Tanzania.

Ni dhahiri kuwa upinzani kwa sasa unakabiliwa na kazi kubwa ya kukabiliana na CCM, chama ambacho kimeendelea kujikusanyia nguvu kikinufaika na fursa ambazo wengine hawapati.

Huku maji yakiendelea kuzidi unga kwa viongozi kadhaa wa upinzani kutokana na kuminywa wasifanye siasa, kukabiliwa na kesi mbalimbali na wengine wakihamia CCM, mawazo yote sasa yameelekezwa kwenye swali moja tu:

Nini kitafuata?
Ukimuuliza Zitto nini kinafuata, atakwambia hakukuwahi kuwa na muda muafaka wa kuwa na DeFront kama ilivyo sasa.

Katika mahojiano yake na Gazeti la The Citizen, Zitto anakiri kuwa makubaliano ya chama chake na CHADEMA yaliofikiwa hivi karibuni ni hatua moja ya kufanikisha uundwaji wa hiyo DeFront, itakayokuwa daraja la kuvuka kizingiti cha hali ya siasa.

Hata hivyo, wengi wanayatazama mahusiano kati ya vyama hivyo viwili – CHADEMA na ACT-Wazalendo yamekuwa kama yale kati ya kuku na mwewe kwa kile ambacho Zitto anakielezea kama “chuki za kihistoria.”

Ingawa hajasema ni chuki ipi ya kihistoria, lakini inajulikana kwamba Zitto aliwahi kuwa kiongozi mwandamizi wa CHADEMA na hatimaye kufukuzwa uanachama na kupoteza ubunge kwa tuhuma za kutaka kukihujumu chama, shutuma ambazo ameendelea kuzikana vikali lakini alipokwenda mahakamani kutetea uanachama wake alishindwa.

“Makubaliano haya ilikuwa ni fursa ya kusahihisha makosa yetu,” anasema Zitto.

Zitto, haijalishi nia yake ni nzuri kiasi gani, anajua kwamba kama DeFront haitakuwa na uungwaji mkono katika ngazi za mashina basi itakuwa ni vigumu kufanikisha lengo lake.

Ukosefu wa uungwaji mkono kutoka ngazi ya chini kumehusishwa na hali inayoukabili UKAWA kwa sasa.

Ndio maana Dk Richard Mbunda, mhadhiri wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema hakuna muungano wowote unaoweza kuiondosha CCM madarakani bila ya kuwa na uungwaji mkono kutoka ngazi ya chini:

“Bila ya kujenga ngome mashinani hakuna cha maana kinachoweza kutokea,” anatabiri msomi huyo na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii nchini.

Lakini unajengaje uungwaji mkono mashinani katika mazingira ambayo siasa zimepigwa marufuku?: “Nadhani hatua ya kwanza kwa muungano wowote utakaoundwa ni kupinga hii marufuku ili iondoshwe,” anashauri Dk Mbunda.

Akizungumzia kuhusu DeFront, Dk Mbunda anasema kinachohitajika ni kiwango cha juu cha kujitoa na utayari ili kuurasimisha muungano huo na kuufaanya madhubuti.

Anadhani kwamba moja kati ya udhaifu ya UKAWA ni kutokuwa rasmi na ulegelege wake, hali ambayo inaufanya uwezo wake wa kuleta mabadiliko kuwa mdogo.

“Katika mazingira ya kisiasa yaliyopo sasa…vyama vya upinzani havitaweza kuishi kwa kujitengatenga,” anasema Msomi huyo.

Kuifanya DeFront kuwa rasmi, Dk Mbunda anashauri vyama vyote vya upinzani vijifute na kuunda chama kimoja cha siasa.

Hata hivyo, ushauri huo, unapingwa na Zitto anayesema kwamba vyama lazima viwemo.

Hata kama Zitto asingepinga, mazingira ya kisheria ya vyama kushirikiana yasiowezeshi. Chama kilichosajiliwa ndicho kinatambuliwa, kinasimamisha wagombea na kikikidhi vigezo kinapata ruzuku.

Mwanasiasa mkongwe nchini na spika mstaafu Pius Msekwa ana maoni tofauti na wengine. Yeye haoni kama DeFront inaweza kubadilisha kitu chochote kwa CCM na anadhani ya kwamba CCM haina sababu ya kuwa na wasiwasi.

“Angalia hatua zinazochukuliwa na (Raisi John) Magufuli katika kutekeleza ilani ya CCM, huridhishwi na utendaji wake?” anauliza Msekwa akionyesha ni jinsi anakunwa na utendaji wa mwenyekiti wa chama chake.

Kwake yeye, kwa kuwa viongozi waandamizi kutoka upinzani wanaendelea kuhamia CCM, kuundwa kwa muungano wowote ni kujisumbua tu.

“Maana pekee ya hicho kinachoitwa DeFront ni kwamba hao wanaotaka kuuunda wanatumia haki yao ya kikatiba ya uhuru wa kujikusanya.”

Hata hivyo, Msekwa anaona ni kichekesho kwa kuwa DeFront inasema inakuja kupigania demokrasia, hivyo kama ingekuwa haipo hata huo muungano usingeweza kuundwa.

Maoni ya Msekwa hata hivyo yamemsikitisha msomi mashuhuri wa sayansi ya siasa na mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu.

Yeye anadhani Msekwa alipaswa ajue zaidi kwamba demokrasia ni mchakato na mapambano ya kuhakikisha ustawi wake hufanywa wakati wowote.

“Nashangaa kumsikia (Msekwa) akisema kwamba demokrasia ipo huku akisahau kuwa demokrasia pia inajumuisha utawala wa sheria na kuheshimu haki za binadamu, vitu ambavyo kwa sasa havionekani.”

Licha ya kuunga mkono wazo la kuunda DeFront, Profesa Baregu anawashauri wale wanaotaka kuunda huo muungano wafikirie kwa makini kama kweli kunahitajika muungano mwingine.

Alikuwa makini kutahadharisha kwamba si kwamba anapinga wazo lenyewe bali anajiuliza tu kama kweli kulikuwa na haja ya kuunda muungano mpya wakati UKAWA upo.

“Shida inazozipata UKAWA kwa sasa si kwa sababu ya mapungufu yake yenyewe, bali ni kwa sababu ya hali halisi ya kisiasa iliyopo nchini,” anatanabahisha mjumbe huyo wa zamani wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Anaongeza, “Kusema kwamba unahitaji jahazi jipya huku bahari ikiwa na matatizo yaleyale haitasaidia.”

Kama kutakuwa na sababu za msingi, basi Baregu analikaribisha wazo hilo kwa mikono miwili: “Kuna umuhimu wa kukaa chini na kutafakari. Ni tahadhari tu. Mimi ni mzee, nimejionea mengi katika maisha yangu.”

Hata hivyo, Zitto, ambaye chama chake siyo mwenza wa UKAWA, anasisitiza kwamba DeFront haikusudii kuiondosha UKAWA bali kuizidishia nguvu.

Ingawaje wazo la kuundwa kwa DeFront limeonekana kutokuwa maarufu miongoni mwa viongozi mbalimbali wa vyama waliotakiwa kulitolea maoni, wengi wao wanadhani ya kwamba ni wazo zuri.

Kwa mfano, John Mrema ambaye ni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, anasema:

“Makubaliano kati ya chama chake na ACT-Wazalendo yanahusu uchaguzi mdogo wa Agosti 12 tu na wala si kuhusiana na DeFront.”

Lakini analikaribisha wazo la kuunda muungano huo akisema kwamba, “Kama lengo ni kuiondoa CCM madarakani, tutashirikiana.”

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Mazrui anasema hakuwa akijua kuhusu wazo la kuunda DeFront kwani suala lenyewe halikuwahi kujadiliwa katika vikao vya chama lakini aliupongeza uamuzi wa Zitto kufikiria uundaji wa muungano huo.

“Ni wazo zuri ukizingatia hali iliyopo sasa ya kuzorota kwa demokrasia nchini,” anasema Mazrui.

Na vipi kuhusu UKAWA? Mazrui anasema kwamba “UKAWA upo hai lakini hauleti wadau wengine kama asasi zisizo za kiraia na vyama vya wafanyakazi.”

“(UKAWA) haina huo uwanda mpana. Na kwa sababu DeFront inaenda mbele zaidi ya chaguzi basi UKAWA unaangukia humohumo katika DeFront,” anasema Mazrui.

Tagsslider
Share: