Habari

Muungano na uvunjike haraka.

Uzalendo katika nchi yoyote siku zote huwa una’ambatanishwa na misukumo fulani fulani,ni lazima uwe unaiabudu misukumo hiyo ili ubarikiwe rasmi kuwa wewe ni muungwana na mzalendo halisi katika nchi yako/husika,Tanzania au Zanzibar na Tanganyika sisi tunatakiwa ku’upenda,ku’uabudu au ku’uenzi Muungano kwa wananchi wote wa taifa hili, na Mapinduzi kwa wale wakaazi wa visiwani peke yake, hapa navihusisha visiwa vyetu vya zanzibar tu, sio vile vya Tanganyika kama Ukerewe na Mafia.

Tumejisalimisha katika misukumo hii miwili kwa zaidi ya nusu karne,udugu,urafiki,damu yetu,wenzetu,ujirani mwema na kila aila ya kauli maridadi zimetumiwa ili tusifikiri au tusihoji yale muhimu kuhusu uhalali au muelekeo wa haya tunayo ya kariri miaka yote hii, kwa kuwa hayo ndio chimbuko la umoja,utaifa na maendeleo yetu,wakati sasa umebadilika na umefika wa sisi Wazanzibari kukubali kuwa kazi ya kujinasua na makucha haya, hasa hili la Muungano sio kazi ya CUF peke yake, au UAMSHO peke yao, hii ni kazi ya kila Mzanzibari mwenye akili timamu, kwa sababu kwa wale wenye matatizo ya akili kwa sasa ni wajibu kuwasamehe, kwa kuwa Mola kazi yake haina kasoro Inshaalah atawaruzuku na wao wapate afueni upesi kwani tunawahitaji mara tu wakipata nafuu katika kupigana vita hii.

Uamsho wamefanya kazi kubwa kutuelemisha sisi wenye visiwa hivi kiasi gani tunatawaliwa na Tanganyika na kwa nini,kufungwa kwao na kukaa gerezani kwa zaidi ya miaka minne sasa, ni ushahidi tosha kuwa hawa ni wafungwa wa kisiasa na sio magaidi kama inavyodaiwa,viongozi au watawala waliowekwa kwa nguvu za kivita na Magufuli/Kikwete hapa visiwani hawakuona tabu wala aibu kuwapeleka waungwana na waisalmu wenzao hawa kwenda kunyea ndooni kama alivyotamka balozi Seif Ali Iddi katika mkutano wa hadhara,udhaifu wao wa kupenda madaraka umewafanya wakose imani na dini yao,Mungu pamoja na viumbe wake, muhimu kwao ni kumfurahisha Mkoloni wetu Tanganyika, ambae kwa sasa ni Magufuli aendeleze utumwa katika visiwa hivi.

Rais wa Tanganyika na Tanzania ya kulazimishana, tangu aingie madarakani hajawahi kutoa kauli ya hekima wala ustaarabu,yeye amebobea katika kauli za kijeuri,hapa kwetu huziita za kifedhuli kwa lugha rasmi ya visiwani,hajui tetemeko la ardhi,njaa inayotukabili,maradhi anayo kataa kuwa Tanzania hakuna juu ya utafiti na maamuzi ya madaktari mabingwa,ukosefu wa fedha za kuwakopesha wanafunzi au matatizo mengine yoyote yanayo wakabili wananchi, yeye amekuwa mjuwaji wa kila kitu ghafla,la kushangaza kabla yeye hajawa rais anadhani sote tulikuwa wapumbavu?mtawala wa aina hii hawezi kuongoza nchi kama hii au nyingine yoyote yenye watu wenye akili timamu,ni lazima sote tuuguwe kwanza ndio tumkubali kwa moyo mkunjufu kiongozi kama huyu, kwa bahati nzuri wengi bado wazima vichwani,mapenzi ya vyama iwe cuf,chadema au ccm haviwezi kututia umajununi wa makusudi na kumkubali/ kukaa kimya huku tukitukanwa tukifungwa na kunyonywa bila huruma na ndugu zetu wa Tanganyika.

Jambo la kusikitisha hivi sasa tayari kuna wanzanzibari ndani ya CCM hapa kwetu,wamesha anza kujipanga na kuanza kampeni za chini kwa chini kwa ajili ya kuja kumrithi Mtawala/kibaraka Sheni kama atamaliza muda wake salama, basi nao wako tayari kuja kuendelea kumtumikia Bwana magunia au huyu huyu Magufuli kwa miaka mingine kumi ijayo, na kuhakikisha hakuna upungufu wa watumwa wake na wataendelea kulalamika tu miaka yote, badala ya kuungana na kumn’goa Sultani huyu mweusi, anae tukumbusha ubaya wa Sultani mweupe siku zote, kwa kuwa anajua hazitutoshi, mmoja wa watu hao ni huyu waziri mdogo wa Tanganyika wa mambo ya ndani, mheshimiwa Hamad Masauni ambae pakifanyika marekebisho ya baraza la mawaziri, huyu muungwana anapandishwa cheo na kupewa uwaziri kamili, huu ni muelekeo na muendelezo wa kutengenezwa kibaraka mpya, na mwingine ni yule yule asie jua anacho kitaka siku zote, si duniani wala si akhera zaidi ya cheo, aliye kuwa waziri kiongozi Ndugu Shamsi Vuai Nahodha, pamoja na mtoto wa mfalme bwana Hussein Mwinyi ambae ni waziri wa ulinzi wa Tanganyika, pamoja na akina mburu matari wenzangu wengine wengi, ambao watakuwa washika veli{wasindikizaji bi harusi}

Ndugu zangu Wazanzibari,hali ya kiuchumi na kimaisha kwa ujumla hapa kwetu Unguja na Pemba ni mbaya sana/ mno,wananchi wetu kwa sasa hali zao ni dhaifu kwa umasikini ulio kithiri au kuvuka mipaka,kama tunavyojua umasikini ndio chanzo cha maradhi yote ulimwenguni,serekali imekoma kutoa ajira miaka mingi, hawana wala hawachukui tena takwimu sahihi za ukosefu wa ajira”unemployment”kinachofanyika ni kubadilisha nambari tu na kumpa mheshimiwa akawasomee wananchi huko mikutanoni,biashara zimeanguka kwa kodi zilizopita viwango, pesa zimeadimika mifukoni kwa kuwa hazina vyanzo zaidi ya ujambazi na rushwa,sisi sio wa kuhangaika namna hii kama tungelikuwa tuna jiendesha wenyewe,Tanganyika zaidi ya kutukopesha mishahara ya wakubwa na wale walioko serekalini hawana wanacho tusaidia,wao wana jenga nchi yao kwa kasi na misaada yote inaingia katika mfuko wao kwa jina tukufu la Tanzania sisi tunaambulia Muungano.

Sio wananchi wote wana uwezo au watoto/ndugu walioko nje kama mimi ambae kila kukicha namshukuru Mola wangu kwa kuwajaalia watoto wangu na wajukuu zangu, wengi wao wako nje,wengine arabuni na wengine canada na scandinavia ambao kidesturi huniangalia mzee wao siku zote kwa kila shida yangu,hicho hicho nipatacho na mimi nagawana na wenzangu ili sote tujaaliwe kuliona jua siku ya pili,sisi wazanzibari tumegeuzwa omba omba bure bila sababu ya msingi zaidi ya siasa.

Siasa imekuwa ndio ugonjwa wetu wa kudumu kuliko donda ndugu,hatuzikani tena sasa,hatusali pamoja upya, tumeyerudia yale yale ya kila uchaguzi sisi tuna laana gani Ya Rabbi?kuna kitu tumekosea au tunakosea kila kukicha hii sio bure,moja ni hili la Masheikh wa uamsho kwa sasa kuwekwa ndani na sisi kukaa kimya, hata hao wari siku hizi wana kauli tele,kwani wamegundua kwa kukaa kimya tu hatoolewa mtu.

Lazima tuamke na kudai waachiwe huru na kulipwa fidia,ni lazima tuandamane siku ya ijumaa itakayokubaliwa iwe mfululizo, hawawezi kutuuwa sote baadhi tutatangangulia akhera hilo halina ubani,kuna mwana falsafa mmoja wa kiafrika kutoka Senegal ambae pia alikuwa mchezeshaji senema, {director}aliyesoma Urusi na kuishi ufaransa kwa muda marehemu Ousmane Sembene aliwahi kusema”kama hamko tayari kumwaga damu basi msidai uhuru”

Zanzibar ya namna gani tunatarajia kuwaachia wajukuu zetu kwa tamaa zetu?woga wetu?dini,mila na tamaduni zetu zote haziko salama?watu wetu na utaifa wetu unafutwa kila kukicha kwa visingizio vya kisiasa,tumepandikizwa chuki kiasi sasa tunagawana vyeo kwa kuukataa Upemba na kuukumbatia Usukuma,tunapeleka wabunge bungeni wengine wanarudi makwao kama yule mbunge wa dole wa zamani, anaitwa Selvester Mabunda, ambae juzi Magufuli kwa kujua yule ni mnyamwezi mwenziwe amaemchagua kuwa balozi,tumepeleka mbunge mwingine wa chwaka huyu Mheshimiwa Bwana Bhagwanji Meisuria,kashughulika na habari za Moshi na Mwanza, huku akijifunza kiswahili dodoma,hana taarifa wala hajui kama kuna Masheikh wana OZA JELA, na kutendewa unyama kila kukicha, pia shida za wananchi wa visiwa hivi sio kipa umbele chake, yeye anataka airport ya Moshi iwekwe Lami wakati sisi tunapita barabara za vumbi huyu ndie ccm kindakindaki.

Nilisema zamani mimi sitaki chama cha siasa kiwe ndio dira ya Uzanzibari wangu,kwa wale wanao nijua nahakika hawakuwa wakinijua, kwa sababu walitarijia mimi niwe kibaraka kama walivyo Wengine au wao, kwa kuwa maslahi ndio msingi wa maamuzi yetu tangu enzi sasa kumezidi nini?kilichozidi sisi ni WATUMWA WA TANGANYIKA, hili sasa halisitiriki kwa tamaa ya cheo wala kuoneana haya,sisi ni binadamu wenye uwezo wa kufikiri upya, hatuna kilema katika kufikiri, ni lazima tujinusuru na nakama za makusudi au kujitakia,tuwe na huruma kwa raia wenzetu,tuchukie ubaguzi kama ukoma na tusifurahie kufungwa kwa MASHEIKH wetu,kama hatukuwaonea uchungu sisi, tunatarajia Mugufuli ndio aanguwe kilio? Mtawala Sheni una jukumu na dhambi kubwa kwa aliye kuumba, wewe pamoja na balozi Iddi, nyie ndio mlio chukua jukumu la mateso yao,Mola wetu hatokubali kusikia kisingizio cha ugaidi wala Muungano kama mnavyotulaghai sisi kuwa ndio sababu zilizo kufanyeni Muwafungulie kesi za uzushi,yeye anazijua nafsi zenu na roho zenu kwa kuwa yeye ndie aliye ziumba sasa tumieni vichwa vyenu kama kweli nyie wasomi wa dini au dunia na mchague akhera yenu kabla milango haijafungwa na pumzi kusita.

Tundu Lissu nae ni wajibu wetu Wazanzibari kumtakia kila la kheri kiumbe huyu,nilijua baada ya ule mkutano wa Dimani kuwa huyu Mungwana atakwenda kujiunga na Masheikh JELA segerea/ukonga upesi, kwa sababu aliyo yahutubia siku ile katika kampeni ile,ilikuwa aibu kwa watawala wetu na vibaraka wao wote,aliwasomesha wengi wasio juwa, kuwa wao Watanganyika ndio wanaomiliki ardhi hii, NA SISI NI WATUMWA WAO,alimtaja Sheni kwa jina kuwa ni kibaraka wa Magufuli na hawezi kukataa kwa sababu hana wazimu, anakijua cheo chake kwa bwana fyokofyoko,sasa kosa la Lissu lipi?leo Tanzania tumerudi pahali ukisema kweli unaitwa mchochezi? na unawekwa ndani,tunatakiwa tukae kimya, tuwe watoto wazuri,HAPANA, tutasema na tutaaandika bora kuwa wachochezi kuliko kuwa WATUMWA/VIBARAKA.

Hotuba aliyoitoa siku ile, ndio itakayo tumiwa kama kielelezo cha uchochezi mahakamani,lakini hakuna la uongo katika kauli zile,hakuna Mzanzibari ambae kwa sasa angeweza kupanga na kuuelewesha umati madhara ya kutawaliwa kwa ufanisi kama vile, hasa hotuba yenyewe ikiwa inatolewa na mwananchi au raia ambae ni sehemu ya mkoloni wetu, kama vile anavyopenda kutujulisha Tundu Lissu siku zote, kuwa wao ndio wakoloni wetu,huyu ni muungwana anaelewa dhambi na maovu yanayo fanywa kwa jina lake na Watanganyika wenzake, na anachukia na kukemea unyonyaji huu,alijua kuwa atafunguliwa mashitaka na kuwekwa rumande au kufungwa na alisema pale mkutanoni,tusihofie sana nini au nani atafanyiwa nini katika kujinasua na minyororo hii,ccm ndio tatizo la afya yetu na visiwa hivi.ikiwa mtu anatoka Singida anakuja kutujulia hali na kutushika sikio….

Sasa sisi Wazanzibari wenyewe tunaogopa nini? au tuna muogopa nani?

Mkianza kuona maandishi yanasomeka kihindi kama yule mbunge wa chwaka, mjue mashine sio mimi,naomba tahfif kwa hilo mimi kiswahili sina ugeni nacho.

NAOMBA NIISHIE HAPA NA ASANTENI.

Share: