Habari

MWANI KUPATIWA SOKO LA UHAKIKA

Mwani

Na Khatib Suleiman – Zanzibar

Posted Jumanne, Juni 23, 2015

SERIKALI ya Zanzibar imesema ipo katika mchakato wa kutafuta soko la zao la mwani ambalo limebainika kuleta tija kubwa kwa wakulima zaidi akinamama Unguja na Pemba.

Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui aliliambia Baraza la Wawakilishi jana wakati akijibu hoja zilizotolewa na wajumbe wa baraza hilo waliochangia bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2015/16.

Mazrui alisema Wizara ya Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wapo katika mchakato wa pamoja wa kulipatia ufumbuzi tatizo la soko la mwani ambalo limeleta usumbufu mkubwa kwa wakulima.

Alisema zao la mwani linashughulikiwa na wafanyabiashara binafsi ambao ndiyo wanaotafuta soko la bidhaa hiyo kwa ajili ya wakulima wa Unguja na Pemba.

Hata hivyo, alikiri kwamba soko la bidhaa hiyo limekuwa likiyumba ambapo serikali imeahidi kulipatia ufumbuzi kwa kushirikiana na taasisi zinazoshughulikia kilimo hicho.

Aidha, Mazrui aliwapongeza wakulima wa zao la mwani Unguja na Pemba, kwa juhudi zao ambazo zimesaidia na kuitangaza Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi tatu katika bara la Afrika inayoongoza kwa uzalishaji wa mwani kwa wingi.

Alisema Kilimo cha mwani kimeleta faraja kubwa kwa wakulima Unguja na Pemba zaidi wanawake ambao wamepiga hatua kubwa na kuondokana na utegemezi wa moja kwa moja kutoka kwa waume zao.

Alisema inachokifanya SMZ ni kutoa faida kwa wakulima wa zao la karafuu kwa asilimia 80 huku ikitoa mikopo kwa ajili ya kuimarisha mashamba yao ikiwemo kutoa miche ya mikarafuu bure.

Chanzo: HabariLeo

Share: