Habari

Mwongozo wa Zanzibar kuanza kushiriki yenyewe kwenye masuala ya Kikanda na Kimataifa wapatikana

Mwongozo wa Zanzibar kuanza kushiriki yenyewe kwenye masuala ya Kikanda na Kimataifa wapatikana

Today at 11:49 AM

Kamati inayoshughulikia masuala ya Muungano imepitisha mwongozo kuhusu Zanzibar ambao utaviwezesha visiwa hivyo kushiriki kikamilifu katika masuala ya kikanda na kimataifa.

Suala hilo lilipitishwa Februari 6 na Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ya kushughulikia masuala ya Muungano.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba aliliambia Bunge jana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020.

Habari hiyo inaweza kuwa njema kwa Zanzibar kutokana na mwongozo huo kumezingatia maeneo ya mikutano ya kimataifa na kikanda, nafasi za masomo ya elimu ya juu na mafunzo mengine nje ya nchi na utafutaji wa fedha za misaada na mikopo ya kufadhili miradi mbalimbali.

Kwa muda mrefu, Zanzibar, ambayo iliungana na Tanganyika mwaka 1964 na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa ikitaka ushiriki katika masuala kimataifa na kikanda, huku ikitaka iwe inatafuta misaada na mikopo nje ya nchi badala ya utaratibu uliopo sasa wa Serikali ya Muungano kufanya kazi hiyo.

Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN), Zanzibar hushiriki chini ya Serikali ya Muungano.

Hivi karibuni, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid alitaka Ibara ya 50 ya Mkataba wa EAC ipitiwe upya ili kuruhusu wawakilishi wa Zanzibar katika jumuiya hiyo kuchaguliwa moja kwa moja kutoka visiwani humo.

Katiba hotuba yake ya bajeti, Makamba pia alizungumzia changamoto za biashara na umeme.

“Changamoto ya ongezeko la gharama za umeme kutoka Tanesco kwenda Zeco (Shirika la Umeme Zanzibar) nalo pia lilipatiwa ufumbuzi na imekubalika kuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) itatozwa kwa kiwango cha asilimia sifuri kwenye umeme unaouzwa na Tanesco,” alisema Makamba.

Pia, alisema malimbikizo ya deni la VAT lililokuwa limefikia Sh22.9 bilioni kwa Zeco kwenye umeme uliouzwa na Tanesco limefutwa.

Alisema pia walizipatia ufumbuzi hoja za biashara ambazo ni gharama za kushusha mizigo.

Nyingine ni viwanda vya Zanzibar kupata leseni za biashara kutoka Wakala wa Usajili na Utoaji wa Leseni za Biashara (Brela).

Jamii Forums mobile app

Share: