Habari

MZEE KARUME NA MAPINDUZI TUNAWATUMIA TU, KUHALALISHA UTUMWA WA MUUNGANO.

Huu ni wakati muafaka sana wa sisi Wazanzibari kujitathmini kwa kina, kwa sababu hivi sasa ni miaka 55 imesha tukurubia tangu tupindue January 12, 1964 na kupinduliwa April 26,1964. Sisi wananchi wa visiwa hivi vya Zanzibar hatuna budi kukubali kuwa katika maisha au jamii, kufanya kosa au makosa ni jambo la kawaida kwa kuwa hakuna mkamilifu,lakini tunapo amua au kuamuliwa kuwa ni lazima tuendelee kufanya dhambi hii moja au kadhaa kila siku hapo ndipo jukumu linakuwa letu sote.

Kosa letu kuu ni la kihistoria na kwa sasa mimi binafsi sipendi nirudi nyuma kila siku kujuta au kujutia hilo,bali naona ni bora nijikite katika kutafuta suluhisho badala ya kutafuta wa kumlaumu saa zote,Mapinduzi yetu matukufu yaliyotukomboa kutoka katika utumwa mmoja na kututia katika utumwa mwingine haraka sana, mimi sioni sababu yoyote ya kusherehekea ukombozi huu, ambao hata marehemu Mzee Karume kama angelikuwa hai basi asingehudhuria sherehe hizi.

Hakuna wa kunishawishi kuwa sisi ni watu HURU, sisi tuna tawaliwa kwa mabavu na Tanganyika,wao wana kila sababu ya kusherehekea siku ya tarehe 26 April ikifika, kwa sababu hiyo siku kwao ndio siku waliyo jin’yakulia visiwa hivi kwa bei POA.

Ndugu zangu nyote Wazanzibari bila kujali vyama vyetu bandia vya siasa, ambavyo ni lazima vikahakikiwe Tanganyika kwanza kwa mkoloni kisha ndio tupate vibali vya kuhutubiana kasumba,sisi tulikuwa nchi au visiwa huru kabla Muungano,baada ya Muungano nani anathubutu kusema kuwa sisi tunajiamulia mambo yetu wenyewe?

Kujikomboa au kupata uhuru maana yake nini?unapopindua ukachukua nchi ukairudisha mikononi mwa walio wengi maana yake nini?unapokuwa na serekali halali ya wananchi walio huru maana yake na kazi yake nini?sasa haya yote ni maswali tena wala sio magumu ni mepesi sana lakini hatupati jawabu kwa sababu sisi tumezowea kuoneana haya/muhali na kudanganyana,tunatakiwa wala hatuombwi tena kuwa unaposikia Mapinduzi basi ujue kuwa hiyo ndio siku TULIYOJIKOMBOA.

Sikatai kuwa siku hiyo tulijikomboa, na sitoisahau milele, TATIZO kwa nini tumekubali kutawaliwa upya na huyu mkoloni mweusi? jaribu kujiuliza ingekuwa Tanganyika ni Waarabu watupu,Wachina watupu au Wazungu watupu, jee sisi Wazanzibari tungekubali mpaka leo kuwa chini ya himaya moja wapo kati ya hizo?nafikiri ingetulazimu kufanya Mapinduzi mengine mapya, tena ya dharura ya kuwaondoa watawala hao weupe kama vile tulivyowaondoa wale wa awali, yaani Waingereza na WaOman,sasa kumezidi nini tena hata ikawa thawabu kutawaliwa na Nyerere,Mwinyi,Mkapa,Kikwete na MAkufuli?

Kila ikifika January 12 tuna sherehekea faida ya Mapinduzi,huku tukijua kuwa hapa hakuna faida ni hasara tupu,kuwa na bendera,rais,mawaziri,wawakilishi,wabunge feki wanaoingia katika bunge kuu la mkoloni kuwakilisha mikoa yao,mahakama,vyombo vyote muhimu vya dola havina maana yoyote, ikiwa vyombo hivyo havina madaraka wala uwezo wa kuamua lolote lenye maslahi yetu na visiwa hivi, bila kibali cha Askofu au shehe mkuu anayeitawala Tangayika.

Marehemu mzee Karume Mola amlaze mahala pema peponi pamoja na wana Mapinduzi wenziwe wote,Tunalitumia jina lake ovyo wakti kama huu ukifika, kwa kuwa yeye ndie baba wa taifa letu,kinacho nishangaza mimi kwa nini hata hotuba zake muhimu kuhusu taifa letu hili hatuwekewi kwenye sherehe hizi, katika maredio au sasa Televisheni/Luninga ili tukapata kumsikia mzee wetu usia wake kuhusu nchi yetu?tunabaki kutumiana kwenye WhatsAPP tu kinaogopwa nini waheshimiwa mlio kalia viti vya utukufu juu yetu.

Mimi najua hotuba za mzee Karume hamuwezi kuziweka kwa sababu zitawaumbua,yeye alikuwa akituhutubia sisi wananchi kuwa ni watu HURU, na hiii ni nchi HURU, pia aliongea mengi sana kwa muda mfupi alio tuongoza visiwa hivi kuhusu Utumwa,Uafrika,Usawa,Umoja na faida za Mapinduzi na kwa nini waliamua Kupindua, kuondoa ubaguzi,ukabila na kukataa KUTAWALIWA tena sasa sisi Tunafanya nini sasa?

Hivi sasa tumetiwa kwenye mtego wa vyama vingi, ambao umetugawa kama samaki(kibua/changu) sisi tumeshughulika na vyama huku nchi au visiwa vinazama, tunachukiana wenyewe kwa wenyyewe kwa faida ya anae tutawala bila fimbo, kwani muda mwingi anatumia mdomo mtupu,fimbo wakati wa uchaguzi anapoona hatari ya kupokonywa koloni lake.

Zanzibar hakuna tena utamaduni,asili inapotea kila kukicha visiwa vimejaa hakuna hata pa kutia mguu,njaa na umasikini unazidi badala ya kupungua, omba omba haina mkubwa wala mdogo,hili ndio lengo la Mapinduzi?

Kujitawala sisi imegeuzwa ndoto,tayari kuna waheshimiwa wanasubiri baraka za mkoloni waje na wao watutawale kwa miaka kumi ijayo baada ya kuondoka Sheni, wanashindana kwa kujipendekeza kwa Sultani mweusi, Rais mstaafu Mwinyi ana  mbembeleza Sultani mweusi safari hii ampe Ufalme mwanawe, ili uhakika wa kututawala upatikane,wote hawa wanayatumia mapinduzi haya matukufu kutukufurisha na asili yetu, kwa kuwa sisi tuliwahi kuwa watu huru kwa miezi mitatu na siku 12 tu.

Zanzibar tunafisidiwa na tumefidisika, upole wetu umegeuzwa udhaifu mkubwa,tamaa za wenzetu ndio mauti yetu sote,sasa tuna kamatana kama kuku na kupelekwa  magereza ya Tanganyika kwa mfalme kwa kuwa sisi hatuamini tena,magaidi huwajui wala masheikh huwasikii wote wako JELA huko Mrima,visiwani hakuna magereza ya wafungwa wa kisiasa? sisi ndio watu Huru?alilaumiwa Mmarekani aliewasweka wafungwa/magaidi Cuba Guantamno Bay,  jee  Tangayika amekamata bata Unguja na Pemba na kuwasafirisha Mahotelini wakale raha bara?

Haya sio Mapinduzi huu ni Utumwa ni lazima tuseme,tunajua kutenganisha lini tulijitawala na lini tulitawaliwa, Mzee karume msimtumie na mapinduzi yake kuhalalisha haramu zenu,kama kweli tunampenda na kumtukuza basi vunjeni Muungano kwanza,kisha waulizeni wenye visiwa vyao kama wanataka tena RAHA HIZI.

Historia ni historia nimesema huu sio wakati tena wa kumlaumu Mzee Karume au Nyerere, kama unawajua walipo nionyeshe,wao yao yamesha waishia na kutangulia kwenye haki,mimi na wewe ni wajibu wetu kuchagua kuyadumisha haya au kuyarekebisha haya huo ndio mtihani wetu.

Kama kuna kosa au makosa yametendeka huko nyuma hiyo ndio historia ilivyo,sio lazima iwe safi siku zote,muda unasonga mbele haurudi nyuma,na mawazo yetu yawe hivyo,Historia ipo ili tujifunze wapi tulikosea na wapi tulikuwa sawa,sisi tuna watoto na wajukuu na vitukuu,unadhani wao wanajali au wanataka kupoteza muda wao kutaka kujua nani alituponza? wao muhimu kwao tuwakabidhi visiwa huru,ili waweze kujiamulia na kujipangia maisha yao kwa faida yao bila kupangiwa  Dodoma.

Wazanzibari wenzangu nyote bila kujali rangi zenu,sura zenu,kabila zenu,dini zenu na asili zenu mimi nawatakia mwaka mpya wenye maamuzi magumu kuhusu mustakbali wa visiwa vyetu,sisi ni damu moja tushirikiane kumuondoa mkoloni huyu mwenye sura na rangi muhimu iliyofanana na wengi wetu,tatizo sio rangi yake,tatizo huyu hana tofauti na wale waliotutawala awali huko nyuma,wote hawa ni maadui wa nafsi zetu,anae kuthamini au kukupenda hakutawali wala kukutia utumwani,tusihadaike na hivi vyeo sisi sio watoto wadogo,unamchapa kiboko ukimpa pipi sekunde chache baadae anasahau.

Zanzibar Kwanza,vyama iwe basi.

Share: