Habari

MZUNGUKO WA MATENDO YA KINYAMA UNAO DHIHIRISHA USHAMBA WA MADARAKA

MZUNGUKO WA MATENDO YA KINYAMA UNAO DHIHIRISHA USHAMBA WA MADARAKA

Anaandika Dr, Farrell Jnr.

Mawaziri wa Emperor wana mambo makubwa. Kingwagala akiwa waziri wa utalii na mali asili anatoa amri ya kuuliwa kwa watuhumiwa wa uhalifu na sababu kubwa ni kuwa nao wanatuhumiwa kuuwa wa kwetu. Jiulize angekuwa Waziri wa Ulinzi si angelishapeleka jeshi kupigana na majirani? Tuna shida gani ya kuwa na mahakama? Tukishazamisha vitumbwi ya warundi tutapambana na visasi kwa nguvu ya mabomu na roketi? Mpe jukumu la ulinzi itakuwaje? Mpe mambo ya ndani tutakuwa tumemtawadha Duterte wa kwetu wenyewe.

Mbarawa yeye alilalamikiwa kuwa katika masuala ya msingi hakukuwa na sehemu ya Zanzibar katika Wizara iliobeba mambo ya Muungano. Akajibu maelezo hayo ni sawa na ya vijijini Pemba na vijiweni Darajani Unguja. Kwa ufupi maneno ovyo, hayakutakuwa kusemwa kwa Emperor. Nae huyu ni mpemba fyoko aliegombea huko vijiweni akashindwa na ndio malipo ya fadhila kwa Emperor. Tatizo nafasi yake ameshaambiwa kuwa sawa na Rais wa Zanzibar kwa tafsiri ya Profesa Waziri asie na Wizara Maalum. Wa kwetu huyu wenyewe, subiri atoke nae aulize kulikoni kijiweni kimnya!

Mwigulu yeye ndio katia fora hasa, anasema hata mukiandama chumbani na mmoja akaumia basi atawashika wahusika. Yaani kilele cha akili za mwendo wa kasi ndio hizo. Inabidi umkimbie hata mkeo siku hio usije ukamkwaa chumbani Mwigulu na jeshi lake watakubeba juu kwa juu. Ni PhD holder huyu, tena mbichi hasa akiwa na dhamana ya ulinzi wa ndani katika nchi inayookota maiti kwenye mifuko ya sandarusi, upigwaji wa risasi wa wabunge na kupotea kwa wananchi. Kumbuka Katiba yetu inaruhusu Maandamano, mikutano ya vyama na kuhimiza uhuru wa demokrasia. Hizi ndizo rangi zao halisi, nguvu, nguvu na maguvu zaidi. Zamani giningi ilikuwa mafichoni, sasa kila mchawi na makarama yake hadharani.

Kuna mwengine anasema fundi cherehani nae ni kiwanda. Na hio inatosheleza kuambiwa Tanzania nchi ya viwanda. Kwa tafsiri hio sisi tunaviwanda kumbe miaka na dahri maana hupiti mtaa mmoja ukamkosa fundi cherahani. Bibi yangu Mungu amrehem nae kumbe alikuwa mmiliki wa kiwanda kwa tafsiri ya maamuna wa Emperor asiekosea. Makamba yeye majuzi katumia neno la ajabu brain masturbation, ashaakum matusi. Naam, mimi naomba radhi, Waziri hana habari na heshima yake anayobeba. Kawaroga nani hawa? Au “Flustlation”! Huyu alau alisema hadharani anatamani kuongozwa na dikteta, Mungu kakisikia kilio chake, mtoto akililia wembe mpe.

Kuna Kabudi nae kabla ya uteuzi alisema katiba ya Muungano haivuki zaidi ya chumbe na mamlaka ya Emperor madogo visiwani kwa sababu ya uwepo wa Katiba yetu na Rais wetu. Majuzi na kwa nguvu zote anasema Rais ni mmoja tu na Waziri asie na Wizara Maalum. Mbobezi wa Sheria huyu na gwiji wa mabadiliko ya serikali Tatu kabla ya maji ya dhahabu ya ulwa na kilemba cha uongozi. Madaraka yanamfanya mtu mwema asiejielewa kuwa muovu. Kauli nilioiona dhaifu lakini ina ushahidi wa matukio tunayopitia. Usimuamini mwanaadam mbele ya madaraka, ulevi wake ni naqama kwa asiejitambua.

Yote tisa lakini Emperor yeye katoa mpya hasa, anasema hakuna Rais kama yeye, naam na akifa atakwenda kuongoza malaika akiwa mteule wa Mungu hasa. Yaani Jibril kwa waumin wa Kiislam tuamini atabadilishwa na kupewa yeye Emperor nafasi hio. Hujafahamu bado? Yaani haya anayoyafanya hapa duniani akiwa Emperor yatazidi mara mia huko akhera akiwa tena ndie kiongozi wa malaika. Nafikiri Kakobe kaona mbali sana kuhimiza watu watubu, tena watubu kwa kauli zao za kumdhihaki Mungu hakim wa haki asiedhulumu na watubu kwa matendo mabaya yanayofanyika dhidi ya wengine wasio na nguvu. Kawaida nafsi ya mtu mwema humsuta na akarudi nyuma dhidi ya maovu yake ila wale ambao Mwenyezi Mungu ameshapiga mihuri kwenye nafsi zao, thumun buqmun, naam hakukosea mwenye milki ya nafsi na roho za viumbe wote duniani.

Huko kwenye Wilaya na Mikoa ndio usiseme, kama watu wametiwa upupu kwa kushindana kujikuna katika matendo yasio na utu. Wengine ni wadogo kwa umri na unakaa unafikiri hivi huko mbele na kudra ya Mungu inavyokwenda watakuja kusema nini kwa matendo yao? Mara Mkuu wa Wilaya kafukuza wabunge ofisini kwa sababu dhaifu, wa Mkoa kajimilikisha Umungu alipo yeye ndipo alipo muumba ardhi na mbigu, Astaghfirullah. Mwengine kataka kuvunja msikiti, mwengine kafunga wabunge, raia, wazee na wanafunzi. Yaani utu haupo na mbadala wake ni amri na nguvu. Na bado kuna watu wanapiga makofi mpaka yawakute? “Evolution” ya ufisadi si mapesa tu kama zamani ya vijisenti na mboga mboga bali kwa sasa ni ufisadi wa haki, insaf, utu na ubinaadam. Kwa mara ya kwanza kabisa ufisadi umezaa biashara ya kisiasa ya mwanaadam kumnunua mwanaadam mwengine. Kama ulisimuliwa tu biashara ya utu kwa sasa ipo machoni mwetu kwa mwenye kuona.

Sasa tuliza akili na fikiri ningekwambia hii ni hadithi ya kitabuni ungelikiitaje kitabu hicho? Kusadikika? Alf Lela wa Lela? Abunuwas au Wasiojulikana? Naam, si ya kucheka, tunapoelekea kubaya sana. Tupo katika kina cha giza lililobeba ushamba wa madaraka, hasad ya matumizi ya nguvu, na ushindani katika ubabe, unyama na udhalili. Bahati mbaya wako wasioona zaidi ya miguu yao na kufikiri madhara ya haya hayatawagusa wenyewe binafsi. Hakika hakukosea alietwambia tuko katika hasara ilioje.

FB

Share: