Habari

Naibu waziri Habari: ‘ubinaadamu upewe nafasi yake sehemu za kazi’

IMEANDIKWA NA HAJI NASSOR, PEMBA

NAIBU Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Chumu Kombo Khamis alisema, pamoja na sheria za kazi zinavyotakiwa kufuatwa kikamilifu, lakini hakuna budi kwa wakuu wa taasisi, wasiuweke pembeni ubinaadamu unaowakumba wafanyakazi wao.

Naibu waziri huyo alieleza hayo, jana ukumbi wa mikutano Shirika la Utangaazaaji Zanzibar ZBC- Pemba, wakati alipokuwa akizungumza na wafanayakazi wa ZBC, kuelekea mwaka mpya wa fedha wa 2019/2020.

Alisema sheria na kanuni za utumishi wa umma, zinafaa kuzingatiwa ipasavyo na kufuatwa kikamilifu, lakini ni vyema kwa wakuu wa maidara na mashirika, wasisite kuukumbuka ubinadamu kwa watendaji wao.

Alieleza kuwa, kila mtumishi wa umma, anatakiwa kuzielewa sheria na kanuni za utumishi na hizo ndio muongozo wa watumishi wote, ingawa wakati inapotokezea ubinaadamu kwa mfanyakazi, hakuna budi utizamwie mara mbili.

“Nadhani tunaelewa kuwa, suala la kutimiza wajukumu yetu ya kazi ndio msingi wa utumishi wa umma na hili, ili kulifikia hakuna budi kwa wakuu wa maidara, kuzisimamia sheria kikamilifu, lakini penye ubinaadamu uangaliwe,”alieleza.

Aidha Naibu waziri huyo wa Habari, alikemea majungu, fitina na rushwa ya ngono sehemu za kazi, akisema hayo hayana tija wala matunda kwenye sekta ya utumishi wa umma.

“Kama kuna mkuu wa taasisi, anayatumia madaraka yake vibaya, na kisha kukosana na mfanyakazi kwa sababu hakutimiziwa matakwa yake, kinachofuata baada ya hayo ni migogoro kazini,”alisisitiza.

Katika hatua nyengine, alisisitiza umuhimu wakuwepo vikao vya mara kwa mara kwa Shirika la Utangaazaji Zanzibar ZBC -Pemba, akisema ndio mwarubaini wa kuondoa changamoto zinazowakabili wafanayakazi.

Kwa upande wake Mtaribu wa ZBC Pemba, Abdalla Abeid, alisema, pamoja na changamoto za uchakavu wa vyombo vyao vya usafiri, wamekuwa wakipamba na hali ngumu, ili kuhakikisha wanatimiza wajibu wa kuwahabarisha wananchi.

“Gari zetu zimeshachoka sana, bajeti yetu bado ni finyu, lakini si haba tunajitahidi kuhakikisha, wananchi wa Pemba, wanaelewa matukio yote yanayotokezea, tana kwa wakati,”alieleza.

Juma Mussa Juma ambae ni mtangaazaji na mtengeneza vipindi wa ZBC, alisema wakati umefika sasa kufikiriwa suala la kupandishwa madaraja, kwa wafanyakazi waliokwisha hudumu kwa muda mrefu.

Nae fundi Omar Juma, alisema suala la maslahi yao limekuwa ni nyimbo ya muda mrefu, ambayo bado haijapatiwa ufumbuzi, hali inayowarejesha nyumba kiutendaji.

Hata hivyo afisa utumishi wa wizara ya Habari Pemba, Mohamed Juma Rashid, aliutaka uongozi wa ZBC Pemba, kuzidisha kasi ya ushirikiano baina yao na makao makuu ya wizara ya habari kisiwani humo.

“Hata kwa mfano mnataka kuandaa bajeti, basi sio vibaya kama tutakaa pamoja, na kushauriana ili kuona mnakuwa na bajeti yenu na kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi na kwa wakati.

Naibu waziri wa huyo, wa Habari, Utalii na Mambo ya kale, amekuwa na utaratibu wa kukutana na wafanyakazi na wakuu wa maidara wa wizara hiyo, kila muda ili kuona changamoto na mafanikio yao.

Mwisho

PembaToday

Share: