Habari

Naiona safari ya CCM nje ya Ikulu

Posted on October 24, 2015

Na Enzi T. Aboud

KISHINDO cha mabadiliko kimekuwa kama wingu kubwa na pana linalowasogeza pamoja wataka mabadiliko na kuvifanya vyama viwili vikubwa Zanzibar vya CCM na CUF vyenye ushindani kutikisa siasa za mazoweya.

Uongozi uliojaa kiburi na kujiona waliopo madarakani hawawezi kuguswa na chochote hauna nafasi tena. Kwa kuwa wamejaa pumzi, watawala wanaodhani wamehulukiwa utawala peke yao, sasa wajiandae kusukumwa nje kwani wamekataa kubadilika. Ule upepo mwanana wa nyadhifa unawapeperusha nje.

Wakati umewadia mabadiliko yapo tu, hata kama matokeo ya kura yatakuwa ya kukibakisha madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) au ya kuiondoa. Mabadiliko ya kuleta utawala mpya wenye matumaini ya uhakika hayaepukiki tena.

Hatua hiyo itamaliza kiburi na ukandamizaji wa watawala msonge wanaojikweza kwa sifa wasizostahiki, kumbe ni watukutu, waongo na wababaishaji wenye usongo wa kujilimbikizia mali na kuwaacha wengine kwenye dimbwi la umaskini.

Hakuna tena subira kwa watakao haki ya kweli. Wanataka usawa, heshima na maadili ya uwajibikaji katika nyanja zote za uchumi: kilimo, uvuvi, biashara ambazo kukua kwake kutachochea kuongezeka kwa ufanisi katika utoaji wa huduma za jamii.

Wananchi wanahitaji uongozi unaozingatia utawala wa sheria na demokrasia pana yenye kumpa kila mwananchi haki ya uhuru wa maoni, mawazo na fikra mbadala ya kuleta maendeleo na kuondokana na uadui wa kubinya maoni na kupata habari.

Mwamko mpya wa mabadiliko umewezesha wananchi kuhoji sababu za watawala kushindwa kutekeleza ahadi zao na kubakia kuzirudia hizo kwa hizo wakishaona uchaguzi mwingine umewadia.

Je, ni kuwafanya wananchi mazuzu na malofa wasiojua nyuma wala mbele? Watawala wanajidanganya kudhani wataendelea kunyonya jasho la wafanyakazi, wakulima, wakwezi na waburura marikwama ya mizigo wakijitafutia riziki ya halali, lakini wakiporwa na watawala wa CCM pasina aibu.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Mapinduzi Zanzibar, wananchi wameondoa woga na kuonekana waziwazi wakipinga utawala wa mabavu, wakipambana na Jeshi la Polisi na vikosi vya Janjaweed vilivyovishwa madaraka ya kupiga na kuwatesa.

Hawa ni katika makundi maovu waliojivisha joho la Mapinduzi kwa kisingizio cha kulinda utawala wa wanyonge kwa imani kuwa wao na viongozi wao ndio wanaoyatetea Mapinduzi.

Msingi wa Mapinduzi ni kuleta haki palipokuwa na ukandamizaji na kubadilisha maisha ya wananchi kwa usawa; kuwawezesha kuishi vizuri wakiwa na uhakika wa usalama wao na nafasi pana ya kufanya shughuli zao za kila siku bila vitisho.

Kaulimbiu ya muasisi wa Mapinduzi, marehemu mzee Abeid Amani Karume, aliyeongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya mapinduzi, ilikuwa ni kila mwananchi kujiletea maendeleo kwa kujitahidi kubadilisha mazingira yanayomzunguka au aliyoyazoea.

Na ndiyo iliyokuwa sifa yake kubwa Karume. Katika miaka minane ya utawala wake, alisimamia miradi mikubwa kadhaa, ukiwemo wa kujenga nyumba za maendeleo na kuwagawia bure wananchi. Hakuwa na majumba ya fahari.

Uthubutu wa kufanya mabadiliko ulianzia kule, chini ya siasa ya ujamaa na kujitegemea ambako watawala wa sasa wa CCM wameifuta na kuamua kuvaa suti na tai hata wakati wa jua kali wakienda vijijini kwa wananchi maskini.

Wanaserebuka na kukata nyonga kwa ngoma zinazopigwa na wasanii wachovu wanaoigiza mila za Wazungu na miziki yao eti ndio ngoma za CCM kuhamasisha wapigakura wanamchague Dk. John Magufuli anayeonesha vituko majukwaani.

Anajilaza na kujiinua kwa pushapu akijionesha kuwa ndie pekee mwenye afya nzuri kuliko wagombea wengine. Ishara ya kiongozi atakayeongozwa na ubabe atakapokuwa Ikulu. Hajui kibarua kilichoko mbele yake cha kubadilisha mfumo wa utawala uliochomekwa na CCM.

Mfumo wa ghilba, uonevu na kuchomozesha makucha ya kupora mali za nchi na kujigawia, hutekelezwa kimtandao kwa kushirikisha matajiri wanaodhamini michongo ya ulaji raslimali za nchi. Ni hawa wanaofanya biashara haramu pasina kuguswa na mkono wa sheria.

Kukithiri kwa maovu hayo, kumeongeza kasi ya mabadiliko. Mfumo wa udanganyifu kwa umma haujishiki tena sasa. Vijana wanaoumia kwa ukosefu wa ajira wanachemka na hawasikii lugha ya kujali historia wala uzalendo.

Ni sheria ya kimaumbile inayoendana na uwezo wa Mwenyezi Mungu kupambana na tawala dhalimu na kuzitimua madarakani hata wakijijengea milima ya majicho, walinzi wa ajabu makatili na wauaji. Sheria hii huwapiga dafrau na kuwatokomeza.

Watanzania wamechoka kushuhudia sera kandamizi kwa kisingizio cha kuimarisha Muungano wa Aprili 1964. Kila upande wa walioungana unataka mabadiliko ya mfumo wa kuuendesha Muungano.

Kukaa kimya kwa mgombea urais Dk. Magufuli, na mgombea mwenza wake, Mzanzibari Samia Suluhu Hassan kuhusu mabadiliko ya kweli ya mfumo wa Muungano kutawafedhehesha. Vile CCM ilivyohujumu Rasimu ya Katiba mpya, wameongeza ufa katika kuzishinda nyoyo za Watanzania, pande zote mbili za Muungano.

Ni jeuri kushikilia kuaminisha watu Muungano ni imara, na kero zimetatuliwa ipasavyo. Mengi ya waliyoyatia dosari wasomi wabobezi wa sheria na haki za binadamu Tanzania kama Profesa Issa Shivji na merehemu Prof. Haroub Othman, hayajatatuliwa.

CCM wanajidanganya kudhani wako sawa kutolijadili kwa ufasaha, bali wabaki tu kuelekeza umma usafi wa Katiba Inayopendekezwa ambayo eti imeipa Zanzibar mamlaka ya kuchimba mafuta na kukopa kuliko ilivyo siku zote.

Kama Dk. Magufuli halimkeri chembe suala hili, mwenza wake linamchefua na kumnyima nafasi ya kujiamini na uhuru kufanya kampeni awapo kwao Zanzibar. Hawezi kusema wazi serikali tatu hazifai, ingawa alishiriki kushawishi Wazanzibari washikilie serikali mbili.

Masikini mwanamama huyu anapigania kujenga viwanda, kuimarisha afya ya mama na mtoto na kuondoa migogoro ya ardhi akiwa Tanzania Bara. Yote hayo hayawahusu Wazanzibari.

Ni tofauti na Juma Duni Haji, mgombea mwenza wa Edward Lowassa wakiwakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Yeye anajiamini, muwazi anayesema bayana kuwa wakichaguliwa wataondoa mfumo wa serikali mbili kwa kuamini umeididimiza nchi.

Umedumisha uongozi kiritimba unaozuia fikra mpya katika ujenzi wa nchi kwa kutunga sheria kandamizi. UKAWA wanapanda chati kwa sababu wanaimba nyimbo zinazoeleweka; wanaahidi kupunguza makali ya uongozi unaotumia uchumi kujenga siasa.

Unapoona nguvu ya Maalim Seif Shariff Hamad anayeongoza Chama cha Wananchi (CUF) imezidi na amejizatiti kuirudishia Zanzibar mamlaka yake kamili, huku akizindua mpango wa kuigeuza Zanzibar Singapore ya Afrika kiuchumi na kijamii; lazima uone akili kubwa.

Sasa geukia upande wa Bara uone jinsi wimbi la mabadiliko lilivyogubika kona, likianzia na kupenya mifupani mwa CCM. Hapo usishangae kukuta Frederick Sumaye, Kingunge Ngombale-Mwiru na wengineo wamegutuka na kuchomoka kumfuata Lowassa. Wote wanasema, “mabadiliko hayazuiliki tena.” Ndivyo safari ya CCM nje ya dola inavyosawiri.

Chanzo: Mawio

Share: