Habari

ZANZIBAR HEROES NI ISHARA YA UMOJA WETU

Mapenzi kwa nchi yake

ZANZIBAR!

Ndani ya damu zao kuna msisimko wa mapenzi kwa nchi yao. Hujisikia raha na furaha pale nchi yao inapovuma midomoni kwa uwakilishi mzuri wa jambo linalowahusu wao hasa nje ya nchi yao. Wote huungana kwa lao na kufurahi pamoja. Kumbe tunaweza. Tunaweza tukaungana katika kila jambo linaloyahusu maslahi ya Zanzibar na wazanzibari. Tunaweza tukafanya makubwa zaidi kwa sababu, hatujisifu tu, bali MwenyeziMungu ametujaalia wingi wa vipaji na vipawa.

Ameturuzuku ari ya kusimama katika kila nafasi ya maisha. Kama ulivyo mchanganyiko kwenye asili yetu ndivyo pia ulivyo mchanganyiko wa vipaji. Ari ya kufika kule tunakokutaka. Kukisimamia kile tunachokiamini.

Licha ya udogo wa Zanzibar yetu, nenda nchi yoyote duniani uwatazame Wazanzibari walivyotawanyika na shughuli zao. Hawajajikalia kitako tu, wanahangaika huku na kule kupambana. Wanatumia akili, nguvu na taaluma mradi tu yastawi maisha yao. Na Alhamdulillah, katika miji ya watu wanafanya vizuri, wakati mwengine kuliko hao wenyeji – Ni kwa sababu ya asili yao iliyowapika kuwa kuishi ni kutafuta. Au husema kwa msemo uliozoeleka kuwa ” Tumetumwa na kijiji”.

Ni jukumu la kila mmoja, hasa wenye nafasi za juu watuunganishe tuzidi kuwa kitu kimoja. Inaonekana kuwa huku chini ni kazi rahisi kuungana pindi tukiunganishwa. Ni wazi kuwa kwenye peto la umoja wetu kuna raha na furaha isiyomithilika kuliko kwenye gereza la mfarakano wetu. Furaha ya maadui ni kutuona tunagombana wenyewe kwa wenyewe. Na chuki zao ni kuungana kwetu. Siasa zetu ni mapito ya mabadiliko ya uongozi awamu hadi awamu. Si chuki. Si visasi. Si vita na uadui. Natamani kuiona Zanzibar ikitukutanisha pamoja kwa mapenzi kama ilivyotokea kwa Zanzibar heroes. Tuliuweka mbele Uzanzibari. Tukafurahi pamoja. Imenisisimua sana. Ikanifurahisha kisha ikanihuzunisha. Machozi yangu niliyaona yanasogea karibu zaidi na kutaka kudondoka. Kumbe inawezekana.

Naipenda Zanzibar. Zanzibar ni moja. Nawapenda wazanzibari. Nawapenda Watanzania.

Ally Hilal
P.O BOX 247,
ahbenylal7@gmail.com
Mwandishi( Ushairi na Riwaya)
Wete – Pemba.
Zanzibar.

Tagsslider
Share: