Habari

Namshauri Dk Shein ageuke ‘muamba ngoma’ muda anao

Elbattawi
Jumanne, Desemba 26, 2017

JUMAMOSI usiku, Desemba 23, 2017 Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliwakabidhi wachezaji wa timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), zawadi kufuatia timu hiyo kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kombe la ‘Cecafa Senior Challenge’, yaliyomalizi katikati ya mwezi huu, nchini Kenya.

Siku ya Ijumaa mchana, Desemba 22, 2017 Dk Shein, aliwaandalia wachezaji, viongozi wa timu hiyo pamoja na baadhi ya viongozi wa SMZ, dhifa kwenye viwanja vya Ikulu ya Zanzibar.

Rais huyo wa Zanzibar, aliwakabidhi wachezaji 22 kila mmoja akipewa hundi (cheque) ya shilingi 3milioni na ahadi ya kupatiwa kiwanja cha kujenga nyumba. Hatua ambayo aliachiwa waziri anayehusika na ardhi kuitekeleza.

Hatua ya Rais wa Zanzibar, ya kuwazawadia vijana hao imepongezwa na watu wengi, kutoka makundi mbalimbali hususan vijana na wanamichezo wa fani mbalimbali. Kwa ufupi ni hatua inayostahiki kusifiwa na kuungwa mkono.

‘Zanzibar Heroes’ katika mechi yake ya fainali dhidi ya timu ya taifa ya Kenya, ‘Harambee Stars’ iliyochezwa kwenye uwanja wa Kenyatta, mjini Machakosi ilipambana kiume kwa dakika 120.

Kenya, ilifanikiwa kunyakua kombe la ubingwa wa ‘Cecafa Senior Challenge’ kwa mikwaju ya penalti. Dakika 90 za kawaida timu hizo walifungana bao 1-1.

Walipomaliza dakika 30 za nyongeza matokeo yakawa 2-2. Vijana wa ‘Zanzibar Heroes’, walijituma kiume kisawasawa na kwamba walidhihirisha msemo: “washindanapo wawili, mmoja hushindwa.” Baada ya kupigiana penalti.

Binafsi naipongeza sana ‘Zanzibar Heroes’ kwa jinsi walivyotandaza soko la kitaalamu kwa kiwango cha juu, chini ya Kocha Hemed Moroko. Kusema wazi, haikuwa shuguhuli ndogo au rahisi.

Kuna mambo mengi kupitia ‘Zanzibar Heroes’, wadau wa soka wamejifunza, viongozi wa serikali ya Zanzibar, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi wa Zanzibar, kwa ujumla wote wamejifunza kupitia mashindano yale.

Labda niseme, kuna watu wasioona mbali ‘kiakili na kifikra’ kwao lile la ‘Zanzibar Heroes’ ndiyo limekwisha. Ni kweli mashindano ya Cecafa ndiyo yamekwisha, sherehe za serikali za kuwapongeza ‘Zanzibar Heroes’, nazo zimeisha.

Lakini, kuna watu wanaoangalia mbali wanaoangalia mustakabaliwa wa Zanzibar, ndani ya Muungano na Tanganyika, wamepata muwamko na ari mpya, juu ya umuhimu wa nchi yao, faida ya kujitawala na karaha za kutawaliwa.

Narudia: Mashindano ya Cecafa, ndiyo yameshaisha. Je, Wazanzibari wamejifunza kitu au jambo lolote kuhusu mustakabali wa nchi yao dhidi ya muungano wake na Tanganyika. Hili ndilo swali kubwa swali nyeti la kuuliza?.

Tunafahamu kwamba michezo ni sehemu ya mazingira yanayomzunguuka binadamu kila siku na hasa kwa vijana, lakini kabisa, haiingii akilini kupenda na kuthamini michezo, bila kuwa na nchi na utaifa. Ni ujinga wa mwisho, kupenda michezo na kuipa umuhimu huku, kusahau maslahi ya nchi na utaifa.

Tuwape moyo, tuwatunze na kuwapongeza wanamichezo wetu kwa kuwazawaidi zawadi kem-kem za mali na na raslimali. Lakini, bila kuangalia kwanza umuhimu wa kuwa na nchi yetu kuwa na utaifa wetu, bila ya kuingiliwa na nchi nyingine ya kigeni. Tusikubali kuingiliwa na hata Tanganyika, abadan tusikubali.

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ni muungano kandamizi, unaowasalitisha Wazanzibari wenye kwa wenyewe, ili kuendelea kuitawala kifisadi, kihusda, na kihuni. ‘Zanzibar Heroes’ wametoa picha kwamba Wazanzibari wanaweza kuwa wamoja kama watakubali hilo kwa ridhaa yao na kuepukana na ushawishi wa kidudu mtu, Tanganyika.

Watanganyika, hasa viongozi wa serikali na CCM na wengine wanaotamani kuiona Zanzibar, haifurukuti, haisongimbele, hawakufurahishwa na hatua waliyofikia ‘Zanzibar Heroes’ ambayo iliibua ghafla umoja na mshikamano wa Wazanzibari.

Magazeti UCHWARA ya Tanganyika, yalishindwa kuandika kwa uzuri na mara kwa mara habari za ‘Zanzibar Heroes’ ni kwa sababu za ubinafsi/choyo na uadui wao dhidi ya Zanzibar. Azam TV pekee, inastahili pongeze na kwa sababu mmiliki wake ni Mzanzibari.

Lakini, pia lakushangaza na lakusikitisha ni kwamba hata TV ya serikali ya Zanzibar, ilishindwa kuonesha machi za ‘Zanzibar Heroes’ moja kwa moja (live coverage) kutoka nchini Kenya. Hadi pale wananchi wa Zanzibar (Unguja na Pemba), walipoonesha mwamko na msisimko juu ya timu yao.

Napasua anga: Nageuza hoja wazi wazi, tabu wanayoipata Wazanzibari chini ya viongozi wa SMZ na ndani ya Muungano wa Tanganyika, kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), madhila matupu, hata kuhadithia ni vigumu, haisemeki.

Othman Masoud, aliyekuwa ‘Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar’ (AG) alipojaribu kuipapatua Zanzibar katika makucha ya Muungano kharamu, ndani ya Bunge la Katiba, takriban miaka minne iliyopita. Nilimchukuwa Dk Ali Mohamed Shein, nikamtumbukiza ndani ya kapu ya maadui wa Wazanzibari, baada ya hatua alizochukuwa dhidi ya mwanasheria huyo.

Tuliona ujinga wa Dk Shein aliyoufanya dhidi ya Othman Masoud, mtetezi wa Wazanzibari. Aliona bora aondoe ‘asset’ aweke ZOMBI, kuwaridhisha mabwana zake, Tanganyika.

Othman Masoud, alifanyawajibu wake kama Mwanasheri Mkuu wa nchi, kulinda nchi isipoteze maslahi yake na haki zake za msingi. Dk Shein na madhalimu wenzake, hawakuridhika, wakamuondoa.

Eti, sasa anawapongeza ‘Zanzibari Heroea’ kwa kuirudishia Zanzibar, heshima yake, unafiki mtupu. Dk Shein, Wazanzibari wengemuona shujaa sana kama engesimama pamoja na Othman Masoud katika kulinda maslahi ya Zanzibar, yasimezwe na Tanganyika. Ukiuliza: Hivyo, Zanzibar ikiwa nchi huru Dk Shein, anakosa nini?.

Dk Shein, ‘sorry…very sorry’ Wazanzibari wenye akili zao timamu, hawezi kumuelewa kuwa kweli anahaja ya kuona heshima ya Zanzibar, ikirejea. Tatizo la Zanzibar ni akina Dk Shein na CCM yao. Pongezi zake zimejaa unafiki.

Ijumaa mchana, tarehe 22/12/2017 kwenye viwanja vya Ikulu katika karamu aliyowaandalia ‘Zanzibar Hehoes’ anakuja na kauli kwamba: ‘Zanzibar Heroes’ wameirejeshea Zanzibar heshima yake. Dk Shein, amejaa unafiki kwenye uso wake na ndani ya moyo wake.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31, 2010 Dk Karume (Amani Abeid), alikabidhi nchi kwa Dk Ali Mohamed Shein ikiwa imetulia kama maji ndani ya mtungi. Zanzibar, ikiwa katika amani na utulivu mkubwa miongoni mwa wa wananchi wake.

Lakini, muda mfupi labda tuseme ndani ya miezi sita au tisa baada ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Dk Shein (mwenyewe binafsi) aliaza uharamia wa kutokufurahishwa na serikali hiyo, akaanza kuibomoa, hatua baada ya hatua.

Kauli za ovyo na kebehi za Dk Shein dhidi ya SUK, zilitoa mwanya kwa maadui wasiyopenda umoja na mshikamano wa Wazanzibari, kuwaona Wazanzibari wameshikamana, wako kitu kimoja kujenga nchi yao, zilianza kufanyakazi kuibomoa SUK, na zilifanikiwa.

Likaibuka kundi la wanaCCM, lililoongozwa na nduli, Balaozi Seif Ali Iddi (adui namba moja wa Wazanzibari), kufanya juhudi usiku na mchana za kuiuwa SUK. Allah, ameanza kumuhukumu hapa hapa duniani, kidogo kidogo.

WanaCCM, akina Salmin Awadh na Asha Bakari Makame na wenzao wengine walishindwa kuficha ukorofi na ubinafsi wao kila walipokuwa wanapanda majukwani kauli zao zilikuwa ni dhidi ya SUK.

Salmin Awadh, alidiriki hata kuandaa mswaada, ili Baraza la Wawakilishi libadilishe sheria kuindoa SUK, ndani ya katiba ya Zanzibar. Kila wakati, Asha Bakari na Salmin Awadh, kauli zao zilikuwa ni za kuipiga vijembe, kuisimanga SUK.

Nakumbuka, mkutano mmoja wa hadhara wa CCM uliyofanyika Kibandamaiti, Nape Nnauye aliwahi kusema wataifuta Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Anatoka mshenzi Tanganyika, anakuja kuwafitinisha Wazanzibari kwao. Jinsi Wazanzibari walivyorogwa na Watanganyika.

Kwa ufupi, ukorofi wa viongozi wa Serikali ya Zanzibar chini ya CCM, hakuna Mzanzibari hata mmoja anayeweza kuueleza akaumaliza.

Kwa hivyo, hamasi waliyoionesha Wazanzibari kwa vijana wa ‘Zanzibar Heroes’ ni ujumbe kwamba Wazanzibari wanataka ‘mamlaka kamili’ ya nchi yao. Muhimu kwanza, ni kusimamisha nguzo ya UTAIFA. Michezo ni issue ndogo sana katika kupambana kusimamia maslahi ya nchi.

Kuna msemo: ‘mficha uchi hazai’. Binafsi sijaridhika kabisa na zawaidi ya Sh 3milioni na kiwanja. Kama kweli Dk Shein, alikuwa na moyo safi na mkunjufu wa kuwazaidia vijana wale, engewanunulia kule Fumba, zile ‘apartment flats’ za Bakhresa, kila mchezaji flat yake. Sio kuwapa viwanja.

Mchezaji mpira wa Zanzibar, hana kipato cha kumudu kujenga hasa timu zenyewe za Jang’ombe. Kumwambia ajenge nyumba ni kumchanganya mawazo. Dk Shein, kasikia wapi kuwa zawadi Sh 3milioni na kiwanja, kuwa mtu anaweza kujenga nyumba. ‘anawapaka mafuta kwa nje ya chupa’.

Sasa narejea kidogo kwa ‘Zanzibar Heroes’. Nawapongeza sana. Ni kweli kwamba watu wengi hawakuipa Zanzibar nafasi ya kushinda tangu awali. Hakuna ambaye aliwaza kuwa Zanzibar, ingefika fainali.

Mungu si Athamani, wamefika, tena kwa uwezo wao, kwa juhudi zao kupitia mafunzo waliyozingatia kutoka kwa kocha wao, Hemed Moroko.

Nasikitika sana kwamba, sikuwahi kuwaangalia katika mechi zao za nyuma kabla ya fainali, hasa walipocheza na maadui zao Tanganyika. Lakini niliiangalia vizuri, mechi ya fainali dhidi ya ‘Harambee Stars’, kupitia Azam TV.

Kwa ufupi ‘Zanzibar Heroes’ walicheza vizuri muda wote walipokuwa uwanjani walijituma, walicheza kwa kujiamini kabisa. Kikosi chake chote kilijituma ipasavyo. Walicheza kwa umahiri na walisakata soka inavyotakiwa.

Najikumbusha tu. Walianza kwa kuwafunga Watanganyika (wenyewe wanajiita Tanzania Bara) mabao 2-1 wakawafunga Wanyarwanda 3-1, kwa Walibya kidogo 1-0 na kutoka 0-0 na ‘Harambee Stars’.

Mechi ya nusu fainali waliwabamiza Waganda 2-1 matokeo yaliyoshangaza dunia. Kama ni kupiga kura ya timu bora, turufu yangu moja kwa moja nawapa ‘Zanzibar Heroes’.

Na hapa ndipo akina Dk Shein walipoibuka, huko nyuma walikuwa hata habari hawana. Alikuwa Dodoma, anapanga mikakati ya kupambana na Maalim Seif na kuingamiza Zanzibar na watu wake.

CUF upande wa Zanzibar, ndiyo walionekana zaidi kuwashajiisha wananchi Unguja na Pemba, kuwapa moyo na kusherehekea timu yao pamoja na kuandika ndani ya mitandao ya kijamii, tangu hatua ya awali.

Bora niseme kwa Zanzibar, wapinzani wa kisiasa hususan CUF, walilifanya hili kuwa ‘Political Issues in Zanzibar.’ Nakusudi kuwa ilikuwa ni hoja ya kuwaunganisha Wazanzibari katika masuala ya nchi.

Hata hivyo, Zanzibar ndiyo kilikuwa kikosi bora cha mashindano ya Cecafa kwa jinsi walivyocheza kwa ari, kujituma na kutokata tamaa. Walijiamini, hata walipotanguliwa kufungwa na ‘Harambee Stars’, hawakubabaika. Walituliza ball na kusawazisha tena kwa wakati mwafaka.

Zanzibar walicheza kwa kuonana, walipeana pasi kwa uhakika, waliweza kumiliki ‘ball, all the time’ bila kuyumba. Ni timu iliyojiamini na mchezaji wake, Feisal Abdalla atabaki katika kumbukumbu zangu kuwa ndiye aliyenikosha zaidi katika michuuano ile.

Narudia tena, pongezi mahsusi kwa kocha, Hemed Moroko. Pamoja na kuwa Kenya ndiyo wamechukua kombe, lakini ball ambalo vijana wa Zazanzibar walicheza Machakos, litabakia katika kumbukumbu za Wakenya na Dunia.

Derrick Nsibambi wa Uganda, aliibuka kuwa mfungaji bora katika michuuno ya Cecafa Senior Challenge 2017. Waganda walishika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Burundi kwa mabao 2-1.

Kwa mara nyingine, hongera ‘Harambee Stars’ kwa ushindi na hongera za dhati kutoka ndani ya moyo wangu kwa timu ‘Zanzibar Heroes’ kwa uwezo na viwango..

 

 

 

 

 

Tagsslider
Share: