Habari

Nani anayekataa Mapinduzi ya 1964

Nchi ya Zanzibar inaadhimisha miaka 54 tokea kufanyika Mapinduzi yaliyouondoa utawa wa Kifalme (Sultan) hapo January 12, 1964. Kufanikiwa kwa mapinduzi haya kulipelekea nchi ya Zanzibar kuwa na mfumo mpya wa kiuongozi ambao Rais (Republic) ndio kiongozi mkuu wa nchi. Waasisi wa mapinduzi haya pasipo shaka walikuwa na sababu zao ambazo kwa wakati huo zilikuwa haziwezi kuzuilika ila kufanyike mapinduzi.

Mapinduzi ni mfumo uliokuwa na unaotumika hadi leo hii kufanya mabadiliko ya uongozi pale njia za busara (uchaguzi, kujiuzulu) zinaposhindikana. Ukisoma mapinduzi ya Ufaransa (France Revolution) 1789 – 1799 yaliyo ondosha utawala wa Kifalme na kuleta utawala wa Urais. Wafaransa walimpindua mfalme Louis XVI, baada ya uchumi na mavuno ya wakulima kushuka. Baada ya kufanikiwa mapinduzi, serikali ilitangaza kudhibiti bei, kutoza ushuru matajiri, kusaidia maskini, kutangaza elimu bure na lazima, pia iliamrisha kuzitaifisha mali na majumba ya Wafaransa wengine waliokimbia. Hapo kabla serikali ilichukuwa ardhi ya kanisa katoli na kuibinafsisha.

Huko Misri mwaka 1952, kulifanyika mapinduzi yajulikanayo July 23 revolution, yakiongozwa na kundi la maofisa wa kijeshi chini ya ukuu wa Muhammad Naguib and Gamal Abdel Nasser. Madhumuni makuu yalikuwa kuondoa Utawala wa Kifalme chini ya Mfalme Farouk. Mapinduzi haya yalikuwa na lengo kubwa zaidi kwani lilibadili katiba ya Misri na kuleta utawala wa Urais (Republican). halkadhalika kwa nchi nyengine zote zilizokuwa zikitumia njia ya mapinduzi tokea karne zilizopita na miaka ya hivi karibuni malengo yao yamekuwa yakifanana.

Mapinduzi ya Zanzibar hayana tofauti yoyote na mapinduzi ya nchi nyengine. Sababu za msingi zilikuwepo, wananchi walishiriki, utawala ulikuwa na mapungufu yake, nakadhalika.

Ipo haja kwa Wazanzibar wote kutambuwa na kukubali kuwa mwaka 1964 kulifanyika mapinduzi na utwala wa Kifalme uliondoshewa. Ukubali au ukatae hilo limeshafanyika wala huna uwezo wa kulirudisha tena, haiwezekani. Bila ya shaka misuguano kwa vile bado wapo wale waliopinduliwa na waliopindua, lakini sio kitu tena cha kukijadili. Ni wakati wa kutungwa vitabu vikawekwa kwenye shelfu kama ni historia iliyopita.

Hoja nyingi zinakuja kuonyesha kuwa mapinduzi ni halali au kharamu. Tukubali kuwa waliopindua walikuwa na sababu zao, halkadhalika waliopinduliwa walikuwa na udhaifu wao. Kwa wakati tulio nao hautusaidii lolote zaidi ya kutukhasiri. Tunachotakiwa ni kutumia kiukamilifu dhana ya Mapinduzi haya kujenga na kuinawirisha nchi yetu ipasavyo.

Ingawa kuna hizi kauli kuwa baadhi ya watu wanapinga mapinduzi, maneno haya yanaweza kuwa ni kichaka cha kujifichia au kupaka matope wengine, pia inaweza kuwa tunawarithisha watoto wachukie mapinduzi yetu. Kinachotakiwa ni kuwa more positive kuamini kuwa Wazanzibar wote wameyakubali mapinduzi. Namna itawafungua macho na kuona ipo haja ya kuendeleza Mapinduzi, kulingana na wakati uliopo.

Hatuwezi kulinganisha kabla ya mapinduzi kulikuwa na kitu flani na baada ya mapinduzi kuna kitu fulani. Hivi unaweza kusema kabla ya mapinduzi hakukuwa na internet, mobile phone, gari nk. Au kabla ya mapinduzi kulikuwa na watu 300,000 wakati baada ya mapinduzi kuna watu 1,400,000. Mahitaji ya mwanadamu ni kulingana na wakati. Mfano, hapo kabla hata uwe hukusoma unaweza kuwa rais, ila sasa hivi unaambiwa hadi uwe na degree.

Wazanzibar tutambue kuwa Mapinduzi ndio zana yetu nyengine ya kuendeleza nchi yetu na kuikwamuwa kwenye makucha ya kikoloni, wanaposikia Wazanzibar wanaadhimisha mapinduzi wanajiuliza. Hivyo tuchukuwe na tuikubali dhana nzima ya mapinduzi kama vile Wafaransa na Wamisri walivyoyachukuwa mapinduzi yao kujenga mataifa yao. Mapinduzi ni utambulisho wa zama, na nchi yetu inahitaji zama hii kuenziwa.

Share: