Habari

Ndege mpya Boeing 787-8 Dreamliner ya Serikali ya Tanzania imewasili

Dar es Salaam Airport
Jumapili, Julai 8, 2018

SERIKALI ya Tanzania leo jioni (Jumapili Julai 8) imepokea ndege yake mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu.

Ndege hiyo ni ya nne kati ya ndege saba zilizonunuliwa na serikali kwa lengo la kuimarisha shirika lake la ndege la ATCL ambalo lilikwisha filisika.

Viongozi wakuu wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa Rais John Magufuli, walikuwepo kiwanjani wakati ndege hiyo ilipowasili.

Ndege hiyo imetua katika uwanja wa ndege wa Dar es Salaam ikitokea mjini Seattle nchini Marekani. Ndege hiyo ina uwezo kuchukua abiria 262.

Ndege nyingine ambazo serikali hiyo ilizinunu na tayari zinatoa huduma ni ndege moja aina ya Bombardier Q400 Dash-8 NextGen. Na ndege mbili aina ya Bombardier CS300 zenye uwezo wa kuchukua kati ya abiria 137 na 150 .

Mwaka 2016 Tanzania ilipokea ndege yake moja mpya aina ya Bombadier Q400 NextGen kwa ajili ya shirika lake la ndege la ATCL katika kuimarisha safari za ndani na kupunguza ukosefu wa muda mrefu wa safari za anga.

Rais Magufuli muda mfupi baada ya kuingia madarakani mwaka 2015 aliweka ahadi ya kulifufua shirika hilo kwa kununua ndege mpya ambazo zitasafiri ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya maeneo ambayo ATCL inatarajia kuongeza ufanisi wa safari zake ni miji ya Dodoma, Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar, Pemba, Bukoba na visiwa vya Comoro.

Kulingana na sifa zinazoelezwa kuhusu Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege zenye teknolojia ya kisasa. Ndege zenye utendaji mzuri na vifaa vipya vya kupendeza.

Mbali na sifa hizo lakini sifa nyingi kwa ndege kubwa na ndege za wastani aina ya Boing 787-8 Dreamliner italinusuru shirika la ndege la Tanzania na matumizi ya mafuta mengi.

Aidha, mazingira ya utendaji kwa kutumia chini ya asilimia 20 hadi 25 ya mafuta na asilimia 20 hadi 25 kwa uchafuzi wa mazingira ikilinganishwa na ndege nyengine zilizowahi kutumika.

Ndege ya Boeing 787-8 Dreamliner ni ya ukubwa wa wastani, yenye injini mbili inayotengenezwa na kampuni ya Boeing ya Marekani.

Matumizi yake ya mafuta ni wastani wa asilimia 20 chini kiwango cha ndege ya ukubwa sawa na huo na ndiyo ndege ya Boeing inayotumia kiwango cha chini zaidi cha mafuta.

Injini zake zimetengenezwa kwa njia maalumu ili kupunguza sauti ndani na pia nje ya ndege kwa hadi asilimia 60. Madirisha yake ni makubwa kuliko ya ndege nyingine za ukubwa kama huo kwa asilimia 30.

Kinyume na mfumo wa kawaida unaotumiwa wa kufungua na kufunga madirisha kuongeza au kupunguza mwangaza kupitia dirisha la ndege, kwa ndege hii ni kubonyeza kwa kutumia teknolojia ya kubadilisha rangi ya kioo kukiwezesha kudhibiti mwangaza unaopenya..

Share: