Habari

Ni Chadema si CUF wanositisha kutangazwa Mgombea

Dar es Salaam. Wakati wa hali ya sintofahamu ikiwa imetawala uteuzi wa mgombea atakayeungwa mkono na vyama vinne vya upinzani, imebainika kuwa mzozo unaochelewesha suala hilo ni mgombea ambaye Chadema haijamuweka bayana.

Katibu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa ndiye ambaye anapewa nafasi kubwa ya kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa mbele ya mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na kada wa NCCR-Mageuzi, Dk George Kahangwa, lakini hadi sasa vyama hivyo bado vinasita kumtangaza mteule wake.

Profesa Lipumba alikuwa amewaahidi waandishi wa habari wiki iliyopita kuwa mgombea ambaye ataungwa mkono na vyama hivyo vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na NLD angetangazwa Julai 14, lakini siku hiyo hakuna aliyetangazwa.

Badala yake viongozi wa Chadema, NLD na NCCR ndio waliofika Hoteli ya Coloseum jijini Dar es Salaam ambako Profesa Lipumba aliahidi kuwa ndiko jina la mgombea huyo lingetajwa, wakati viongozi wa CUF hawakuonekana na baadaye jioni wakasema kuwa walikuwa na kikao cha ndani ya chama cha kutafuta ufumbuzi wa mambo ambayo walikuwa hawajakubaliana.

Vyama hivyo vitatu vikaeleza baadaye kuwa jina hilo litatangazwa ndani ya siku saba kuanzia Julai 14, lakini siku iliyofuata CUF ilisema suala la kuachia chama kingine jukumu la kusimamisha mgombea urais litawasilishwa kwenye kikao cha Baraza Kuu la chama hicho ambacho kitafanyika Julai 25, jambo ambalo lilikubaliwa na vyama hivyo vitatu.

Matamko hayo yamefanya suala la mgombea urais wa Ukawa kugubikwa na giza nene, lakini kwa siku tatu Mwananchi imefuatilia na kubaini kuwa mgombea ambaye yuko na hajatajwa rasmi kwa vyama hivyo vinne ndiye anayechelewesha mchakato huo na amesababisha kuwapo na hatari ya umoja huo kuparaganyika.

Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka ndani ya vikao vya Ukawa vilivyoanza kufanyika takribani wiki mbili jijini Dar es Salaam, zinaeleza kuwa licha ya viongozi wa vyama hivyo kumpata mgombea wao wa urais katika kikao cha Julai 14 mwaka huu, walikwama kumtangaza kutokana na CUF kutokuwapo kikaoni ikielezwa kuwa wanapinga maendeleo ya mchakato huo.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa msimamo huo wa CUF umetokana na utata ulioibuka katika kikao cha Ukawa cha Julai 11 na 14, baada ya wagombea wawili kati ya watatu, kukubali mmoja wao agombee urais, lakini chama chake kikasema kuwa kinachotakiwa ni Ukawa kutangaza jina la chama kitakachotoa mgombea na si jina la mgombea.

Tayari Profesa Lipumba ameshachukua fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CUF, wakati Dk Kahangwa amechukua fomu kuwania urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, huku mchakato wa Chadema ukiwa haujaanza.

Habari hizo zinaeleza kuwa awali kulikuwa na mvutano mkali kati ya Profesa Lipumba na Dk Slaa na kwamba katika kikao cha Julai 11, Lipumba ambaye ni mwenyekiti wa CUF alikubali kumuachia Dk Slaa agombee urais kupitia Ukawa, lakini inaonekana hata ndani ya Chadema bado hawajaafikiana kuhusu jina la mgombea.

Hata hivyo, chama hicho kimeeleza kuwa jina la mgombea urais limeshapatikana na linasubiri muda muafaka.

“Tutamtangaza mgombea urais wa Ukawa ndani ya wiki moja kama tulivyosema awali,” alisema Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika jana.

“Wananchi wanatakiwa kutulia tu, siku ikifika tutatangaza.”

Mnyika alitoa ufafanuzi huo muda mfupi baada ya kulieleza gazeti hili jana kwamba wanaopaswa kuzungumzia suala hilo ni Dk Slaa na Profesa Lipumba.

Jibu kama hilo la Mnyika lilitolewa pia na mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alipoulizwa kuhusu habari kwamba kuna jina la mgombea urais linalosumbua Ukawa.

“Sijui chochote kuhusu hilo. Ila watu hawa wawili, Mbowe na Dk Slaa watakusaidia kujua kuhusu jambo hilo.”

Alipobanwa zaidi, alisema: “Unajua hata mimi nazisikia sana habari kama hizo pamoja na nyingine nyingi. Katika Ukawa watu wanazungumza ndani ya vikao na nje ya vikao, ila wa kulithibitisha hilo ni hao watu wawili niliokutajia.”

Lakini mpashaji habari wetu alisema ugumu wa kumpata mgombea urais wa Ukawa kutoka Chadema unasababishwa na chama hicho kutotaka kuweka bayana jina la mtu atakayebeba jukumu hilo wakati wameshakubaliana kuwa Dk Slaa ndiye asimamishwe.

“Inaonekana kama kuna mtu mwingine hivi. Wote tumekubali mgombea awe Dk Slaa, lakini Chadema wenyewe wanazuia asitangazwe,” alisema mpashaji huyo kutoka ndani ya vikao vya Ukawa.

Habari zaidi zinaeleza kuwa ndani ya Chadema kuna mvutano, kwani wapo wanaotaka Dk Slaa atangazwe kuwa ndiye mgombea na wanaotaka asitangazwe lakini hawaweki bayana kuwa hawamtaki au wanataka mtu mwingine.

Hata hivyo, habari hizo zinasema kuwa sababu nyingine inayochelewesha suala hilo ni Chadema kutotaka kumtangaza mgombea wake kutokana na mchakato wake wa uteuzi wa mgombea urais kutoanza. Mchakato huo utaanza Julai 20 na kumalizika Julai 25, siku ambayo CUF itakuwa na kikao chake cha Baraza Kuu kuamua mgombea urais.

Habari zinasema kuwa Chadema imekuwa ikisisitiza kuwa Ukawa itaje jina la chama kitakachotoa mgombea urais na si jina la mwanachama atakayegombea nafasi hiyo.

Habari hizo zinaeleza kuwa chama hicho kinachoongoza kambi ya upinzani, kinadai kuwa Ukawa kutangaza jina la mwanachama atakayegombea urais ni kuingilia mchakato wa Chadema ambao humalizika kwa kikao cha juu kupitisha mgombea urais wa chama.

Awali baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais kwa tiketi ya CUF, Profesa Lipumba alikuwa akisema kwenye mikutano ya hadhara kuwa vyama hivyo vinne vimekubaliana kuwa kila kimoja kifanye mchakato wake wa kupata mgombea. Alisema kila chama kitalazimika kupeleka Tume ya Uchaguzi (NEC) jina la mgombea wake ili kiwe na uhakika kuwa amepitishwa halafu ndipo vikutane na kuamua mmoja atakayeungwa mkono na vyama vyote.

Lakini hali hiyo ilibadilika mwishoni mwa mchakato wa CCM wa kumpata mteule wake wa mbio za urais baada ya Ukawa kuitisha mkutano wa pamoja na wabunge wa vyama vinavyounda umoja huo ambao habari zinasema walishinikiza kuwa mgombea wa Ukawa atangazwe mapema na si kusubiri mchakato wa kila chama.

Mvutano ndani ya Ukawa ulianza wakati CUF ilipotaka iachiwe nafasi ya kusimamisha mgombea urais kwa madai kuwa Chadema imeshaunda mtandao mzuri na hivyo itakuwa na nafasi ya kuingiza wabunge wengi, lakini chama hicho kinachoongoza kambi ya upinzani bungeni kikaeleza kuwa CUF ilishaachiwa nafasi ya kusimamisha mgombea urais wa Zanzibar.

matukio hayo yanatokea wakati aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa akiombwa asiondoke CCM baada ya kuenguliwa kwenye mchakato wa urais wa chama hicho tawala.

Makada kadhaa wamejitokeza hadharani na kumsihi mbunge huyo wa Monduli kukubali matokeo na kutofanya uamuzi wa kuondoka, huku watu wanaosema kuwa wanachama wa CCM wakitangaza kujivua uanachama na kujiunga na Chadema kwa maelezo kuwa hawakubaliani na uamuzi wa chama hicho tawala kumuengua Lowassa.

Lowassa hajatoa kauli baada ya kuenguliwa CCM na mapema wiki hii kulikuwa na habari kuwa angeongea na waandishi wa habari, lakini mkutano huo ukafutwa saa chache kabla ya kuanza.

(Mwananchi)

Share: