Habari

Nini khasa tatizo la Zanzibar?

Nini khasa tatizo la Zanzibar?

Na Harith Ghassany
July 9, 2018

Maridhiano ndio “Magna Carta”* ya Zanzibar. Maridhiano bado yamo ndani ya Katiba ya Zanzibar. Kinachokosekana ni viongozi WAPYA watakaoweza kulitatua tatizo la Zanzibar.

Lakini nini khasa tatizo (real diagnosis) la Zanzibar kwa sentensi moja? Ifikirie vizuri jawabu yako: ni ya kupakapaka (finyu) au yenye undani na mtazamo mpya?

Natamani Zanzibar ingelikuwa na viongozi wabunifu. Viongozi wabunifu ni wale ambao wana uwezo wa kuanzisha mchakato endelevu katika kuituliza Zanzibar na kuipa maendeleo ya haraka sana ya kielimu na kiuchumi. Wenye kuililia na kuitamania Zanzibar iwe Singapore au Dubai ya Afrika Mashariki na Kati ni wengi. Lakini wangapi wanaotwambia ukweli iwe pembeni au hadharani nini khasa tatizo la Zanzibar? Maana kulijua tatizo ni nusu ya utatuzi.

Rwanda wameweka kando roho mbaya na siasa za mivutano ili wajenge nchi yao. Zanzibar bado tunachechemea kwa kutoaminiana na kudanganyana.

Wananchi wa Zanzibar kwa asilimia kubwa wameshaliona hili, tuombe tupate viongozi wakweli ambao wataweza kulifanyia upasuaji wa kina na dawa ya kudumu gonjwa hili sugu lenye sifa ya donda ndugu, siasa mbovu na chafu zilizowazoelesha Wazanzibari kushindwa kutia nguvu zao zote katika kuijenga Zanzibar badala ya kutupiana maneno na kubaguana kusikokwisha.

Lakini kwanza: nini khasa tatizo la Zanzibar? Kweli ni visingiziyo vya Utumwa, Mapinduzi, Muungano (Tanganyika), vyama vingi, chaguzi, Katiba, vyama va siasa lazima kuwa vya Kitaifa, kutoaminiana kwa viongozi wa vyama vya kisiasa, suala la vyama kujiona wao wana haki na Zanzibar zaidi ya wengine, suala la vyama kutosikiliza sauti za wafuasi, hoja za dini, mivutano baina ya Wazanzibari walioko Zanzibar, au baina ya Zanzibar na Tanganyika, au baina ya CCM Zanzibar na wahajirina, kukosekana kwa umoja wa kijamii au umoja wa kitaifa, au kushindwa katika yote kwa kushindwa kuifahamu, kujifunza, halafu kuisahau historia na kuzielekeza nguvu zote za kijamii na kuziweka kwenye kulijenga Taifa la Zanzibar na la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?

Au tatizo la Zanzibar lina mizizi mirefu zaidi na kuongezewa kasi Zama za Siasa (kabla ya 1964), mizizi ambayo bado haijatambuliwa na kungolewa na wasomi, vijana, na watawala wa 2018?

Fikiria vizuri kabla hujajibu kwa kuyarudia majibu ambayo tayari yanajulikana na ambayo yamekuwa wakielezwa Wazanzibari na wanasiasa wa pande ZOTE.

Tanzania Bara, Rwanda, Kenya, Eritrea, Ethiopia, wote wanabadilika na wanategemea kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi. Wazanzibari hawakunasa. Viongozi ni wale wenye kufata uongozi na uongozi wa Zanzibar ni Maridhiano ambayo yametikiswa lakini hayajaanguka.

Nini khasa tatizo la Zanzibar? Usikurupuke na usikubali kukurupushwa. Na zaidi kama kweli tuna uchungu na tunaipenda Zanzibar basi tusikubali kudanganyana.

*Magna Carta (Great Charter) ni mkataba/ msingi wa ustaarabu wa nchi za Magharibi ambao ulitiwa saini Uiengereza na Mfalme John mwaka 1215. Ni Mkataba ambao ulisimamisha uwajibikaji mbele ya sheria akiwemo Mfalme…

Share: