Habari

Oman kuendelea kuisaidia Z’bar – Dk. Hamed

Oman kuendelea kuisaidia Z’bar – Dk. Hamed
September 6, 2018

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

OMAN imesema itaendelea kuziunga mkono jitihada zinazochukuliwa na Zanzibar katika kuinua uchumi na maendeleo ya kijamii, hasa ikizingatiwa kuwa nchi hizo zinaunganishwa na historia ya muda ndefu.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman, Dk. Hamed Mohammed Al- Dhawiyan alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi.

Dk. Hamed alisema miradi ya kijamii ikiwemo ile ya kihistoria pamoja na majengo ya kale yanayojengwa na yaliyopata baraka ya kutaka kujengwa na Zanzibar chini ya msaada na ufadhili wa serikali ya Oman ni dalili ya kuendeleza udugu wa pande hizo mbili.

Alisema Oman katika juhudi za kuendelea kuitanga Zanzibar kimataifa hasa katika masuala ya kihistoria, imeandaa mkutano wa kimataifa wa masuala ya historia baina ya Oman na Zanzibar nchini Ujerumani, kwa lengo kuutangaza uhusiano ulipo kati ya nchi hiyo mbili.

Mwenyekiti huyo wa Mamlaka ya Uhifadhi Nyaraka na Makumbusho wa Serikali ya Oman alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba, taifa hilo halitasita kutumia utaalamu na ufadhili iliyonao katika kuendelea kusaidia mambo ambayo Zanzibar itahisi inayahitaji.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif alisema ziara za mara kwa mara zinazowajumuisha viongozi wa ngazi za juu wa pande zote mbili zinachangia kuimarisha afya ya uhusiano huo.

Alimueleza Mwenyekiti huyo kwamba kitendo cha Serikali ya Oman chini ya Sultan Qaboos cha kuwapa nafasi za juu za uongozi watu wenye asili ya Zanzibar ni thamani kubwa waliyonayo waoman kwa ndugu zao wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alielezea faraja yake kubwa aliyonayo kutokana na Oman kusaidia ujenzi wa msikiti wa Ijumaa uliopo Kiembesamaki na matengenezo ya jumba la Bait al Ajaib liliopo Forodhani, majengo yatakayoweka alama kubwa ya uhusiano wa pande hizo mbili.

Zanzibarleo

Share: