Habari

Oman kugharamia matibabu wagonjwa wa moyo Zanzibar

SERIKALI ya Oman imekubali kugharamia matibabu ya watoto wa Zanzibar wanaosumbuliwa na maradhi ya mayo, watakaopelekwa India.

Hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, na ile ya Oman juu ya hoja ya kutanua wigo wa ushirikiano katika sekta ya Afya kati ya nchi hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mnazimmoja Waziri wa Afya Juma Duni  Haji, alisema  Fubuari 18, mwaka huu, madaktari bingwa wa maradhi ya moyo kutoka Hospitali ya Narayana Hurdayala iliyoko mjini Bangalor India ambayo ni maalum kwa maradhi hayo walifika nchini na kuwafanyia uchunguzi watoto 73 kwa Unguja.

Alifahamisha kuwa, watoto hao wenye umri wa chini ya mwaka mmoja hadi miaka 16 ni miongoni mwa watoto 100 wenye matatizo ya moyo ambao wamewahi kufikishwa hospitali kuu ya Mnazimmoja na wamo kwenye orodha ya wizara yake.

Waziri Duni alisema katika wiki ya kwanza ya mwezi wa machi, kati ya watoto 10 mpaka 20 watasafiri kwenda matibabuni katika hospitali na Narayana Hurdayala, na kwamba gharama zote za matibabu hayo zitalipwa na Serikali ya Oman.

“Tumekubaliana Serikali ya Oman, itagharamia matibabu hayo, nasi tutawajibika kufanya maandalizi ya hapa ikiwemo kupata pasi za kusafiria za watoto hao”, alieleza Waziri huyo.

Katika hatua nyengine alieleza kuwa, wataalamu hao waliondoka kwenda kuwafanyia uchunguzi kama huo watoto wa kisiwani Pemba na huko kuanisha watakaohitaji kutibiwa nchini India.

Alisema hatu hiyo itasaidia sana serikali ya Zanzibar ambayo imekuwa ikikabiliwa na idadi kubwa ya wananchi wanaohitaji msaada wa kwenda kutibiwa nje ya nchi kutokana na maradhi mbali mbali.

“Imekuwa kawaida kwa wananchi baada ya kuonana na madaktari wetu na kuonekana haja ya kutibiwa nje, hufika ofisini kwangu kutaka msaada, ni dhamira yetu kuwasaidia wote lakini uwezo wetu ni mdogo, hivyo tunaishukuru oman kwa kuliona hili na kuamua kutusaidia”, alifafanua Duni.

Hata hivyo, hakuweza kusema ni kiasi gani kitahitajika kuwatibu watoto hao, zaidi ya kufahamisha kuwa gharama hizo zitajulikana baadae na uongozi wa Hospitali ya Bangalore utaziwasilisha Oman, kwani pia zitategemea na aina ya matibabu kwani yapo viwango tafauti.

Waziri Duni alichukua Fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Oman, ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika sekta afya hapa Zanzibar,ikiwemo ujenzi wa Chuo cha Afya mbweni, pamoja na Hospitali.

Mbali na India nchi nyengine ambazo wagonjwa wanasumbuliwa na Maradhi tofauti kutoka Zanzibar wamekuwa wakipelekwa kwa matibabu, ni pamoja na Ujeruman, Israel, Hispania, Uholanzi na nyenginezo kadhaa.

Share: