Habari

Oman kujenga kituo cha kisasa cha kiislamu Z’bar

Hafsa Golo

SERIKALI ya Oman inatarajia kujenga kituo cha kisasa cha kiislamu Zanzibar ambapo ndani yake kitakuwa na msikiti mkubwa, madarasa sita, chumba cha kompyuta na maabara.

Balozi Mdogo wa Oman aliepo Zanzibar, Mansoor Nasser Mansoor Al-Busaidi alisema hayo wakati akizungumza na makampuni mbali mbali yaliojitokeza kuomba zabuni ya ujenzi wa kituo hicho, katika ukumbi wa Wizara ya Elimu Mazizini.

Alisema uamuzi wa kujenga kituo hicho ni kuendeleza misingi ya dini ya kiislamu nchini kwa kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya waislamu.

Aidha alisema uhusiano mzuri uliopo kati ya Oman na Zanzibar ndio ulioihamasisha nchi yake kujenga kituo hicho ambacho kitaleta matunda mazuri kwa pande zote mbili.
Hata hivyo, hakutaja thamani ya mradi huo mkubwa ambao utakuwa wa kwanza tokea Zanzibar ipate uhuru.

Alisema ujenzi wa kituo hicho utakuwa na mzunguko wa 14,000 huku msikiti ukiwa na ukubwa 4000 unaotarajiwa kuingia jumla ya waumini 3,500 kwa wakati mmoja na ambao utakuwa ni wa mwazo kwa ukubwa Zanzibar.

Naibu Katibu Mkuu wizara ya elimu na mafunzo ya amali,
Abdalla Mzee alisema ujenzi wa kituo hicho ni hatua moja ya mafanikio ya baadae ya kuanzisha chuo kikuu cha kiislamu Zanzibar.

“Lengo la baadae ni kutanua elimu na kuanzisha chuo kikuu cha kiislamu Mazizini kwa hiyo utakapomaliza ujenzi tunafikiria kufanya hivyo,”alisema.

Hata hivyo, alisema uamuzi uliofanywa na serikali ya Oman ni njia moja ya kukuza taaluma mbali mbali kwa Zanzibar ikiwemo masuala ya maabara, kompyuta na mafunzo ya dini ya kiislamu.

Naye Mkuu wa chuo cha Kiislamu Mazizini, Dk.Muhidini Ahmad alisema ujenzi huo utakipa hadhi zaidi chuo hicho na kuboresha sekta ya elimu.

Jumla ya kampuni 13 zimejitokeza kuomba zabuni ya ujenzi wa kituo hicho ikiwemo kampuni ya Shanks ya Oman, Salem Construction Ltd, Mazurui Bulding Contract.

Share: