Habari

Oman Yaikabidhi Serikali Hundi ya T.shilingi Bilioni 12.3

Tuesday, May 26, 2015

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 26.5.2015

SERIKALI ya Oman imeikabidhi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hundi ya T.Shilingi Bilioni 12.3 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Kiwanda cha Upigaji chapa zikiwemo mashine za kuchapishia magazeti na vitabu.

Wakati huo huo, Serikali ya Oman imeikabidhi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nyaraka za gari 10 zilizotolewa msaada na nchi hiyo zikiwemo za viongozi wakuu.

Balozi wa Oman katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Saoud Ali Mohamed Al Ruqaishi alimkabidhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein hundi hiyo pamoja na nyaraka hizo za gari, makabidhiano yaliofanyika leo Ikulu Mjini Zanzibar.

Mara baada ya kupokea hundi kwa ajili ya vifaa vya kiwanda hicho cha Upigaji chapa pamoja na nyaraka za gari hizo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alitoa pongezi kwa Serikali ya Oman chini ya uongozi wa Sultan Qabous Bin Said Al Said kwa msaada wake huo kwa Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa msaada huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuiwezesha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukamilisha nia na malengo yake ya kuhakikisha inakuwa na kiwanda chake cha kisasa cha Upigaji Chapa ambacho kitachapisha magazeti na vitabu.

Katika mazungumzo hayo, ambapo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd alihudhuria, Dk. Shein alisema kuwa msaada huo unaonesha wazi mahusiano na mashirikiano mazuri na ya muda mrefu pamoja na mapenzi yaliopo kati ya Serikali ya Oman na ndugu zao wa Zanzibar.

Alisema kuwa msaada huo ni muendelezo wa misaada kadhaa iliyotolewa na Serikali ya Oman kwa Zanzibar ikiwemo ujenzi wa Chuo cha Afya kilichopo Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar pamoja na misaada mengineyo ambayo tayari nchi hiyo imeshaitoa.

Aidha, Dk. Shein alimuhakikishia Balozi huyo kuwa misaada hiyo itatumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa na kusisitiza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati yake na Oman.

Dk. Shein, alisema kuwa kwa niaba ya wananchi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ametoa shukurani kwa Serikali ya Oman kwa misaada hiyo ukiwemo msaada huo wa mkubwa wa fedha.

Pamoja na hayo, Dk. Shein, kwa mara nyengine tena alimtumia salamu kiongozi wa nchi hiyo na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kuwa na afya njema yeye pamoja na wananchi wa nchi hiyo.

Mapema Balozi wa Oman Katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Saoud Ali Mohamed Al Ruqaishi ambaye alifuatana na Balozi Mdogo wa Oman anayefanyia kazi zake hapa Zanzibar Mhe.Ali Abdulla Al Rashdi alieleza kuwa Oman itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake kati yake na Zanzibar.

Balozi huyo wa Oman nchini Tanzania alisema kuwa ni matumaini makubwa ya Oman kuwa msaada huo wa fedha taslim kwa ajili ya ununuzi wa vifaa zikiwemo mashine kwa ajili ya Kiwanda cha Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali utasaidia kwa kiasi kikubwa katika utengenezaji wa magazeti na vitabu hapa Zanzibar.

Alisema kuwa kiwanda hicho kitawawezesha wananchi wa Zanzibar kuweza kuwa na kiwanda maalum cha kuchapisha magazeti pamoja na vitabu.

Pamoja na hayo, Balozi huyo alieleza kuwa gari hizo kumi zikiwemo za viongozi nazo zitasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuendeleza shughuli za maendeleo hapa nchini.

Balozi huyo vile vile, alieleza kuwa Kiongozi wa Oman Sultan Qaboos Bin Said Al Said anathamini uhusiano na mashirikiano yaliopo kati ya Oman na Zanzibar na kuahidi kuwa hatua hizo zitaendelezwa kwa upande wa wananchi pamoja na Serikali za pande zote mbili.

Upatikanaji wa vifaa hivyo kwa ajili ya Kiwanda hicho cha Upigaji chapa kutakiwezesha kiwanda hicho kuchapisha magazeti pamoja na vitabu mbali mbali hapa Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Zanzinews

Share: