Habari

Othman Masoud: Masauni amelewa pombe gani?

Masheikh wa Uamsho wakipandishwa gari la polisi kutoka mahakamani Zanzibar

Na Othman Masoud Othman
Sources: Jamii Forums – Jumatano tarehe 1 Mei 2019
part ll

Msimamo wa Kisheria

Katika mfumo wa kikatiba wa Jamhuri ya Muungano, masuala ya mahkama na usimamizi wa sheria si suala la Muungano. Kilichokuwa cha Muungano ni Mahkama ya Rufaa pekee.

Kwa hivyo, hadi katika ngazi ya Mahkama Kuu, hakuna Mahkama ya Jamhuri ya Muungano bali Mahkama ya Tanzania Bara au Mahkama ya Zanzibar. Na katika hilo, ndio maana Mahkama Kuu ya Zanzibar na Mahkama Kuu ya Tanzania Bara zina mamlaka sawa [concurrent jurisdiction].

Katika Sheria ya Jinai, jambo moja lililowekewa ufafanuzi mzuri ni juu ya upeo wa mashtaka na mamlaka ya kushtaki.

Tulizoea kukariri kwa moyo kutokana na umuhimu wake kifungu kinachoeleza ni wapi mtu atashtakiwa kwa kosa alilotenda.

Kwa upande wa Zanzibar, kwa mfano, mtu atashtakiwa katika Mahkama za Zanzibar endapo viini vyote vya kosa [elements of the offence] vimefanyika Zanzibar au katika bahari kuu ambayo Zanzibar ina mamlaka nayo chini ya sheria za kimataifa.

Aidha, anaweza kushtakiwa Zanzibar endapo baadhi ya viini vya kosa vimetokea nje ya Zanzibar lakini baadhi ya viini vya kosa vimetokea ndani ya Zanzibar.

Kwa ufupi, ili mtu ashtakiwe Zanzibar ni lazima kuwe na uhusiano wa kosa hilo na Zanzibar. Hali ni hivyo hivyo kwa sheria za jinai za Tanzania Bara.

Hata hivyo, suala ambalo muda mrefu lilikuwa na utatanishi ni: jee, Mahkama Kuu ya Zanzibar inao uwezo wa kusimamia sheria zilizotungwa na Bunge la Muungano?

Mahkama Kuu ya Zanzibar katika kesi kadhaa imewahi kutowa ufafanuzi wa suala hilo. Katika kesi ya Himid Mbaye v. The Brigade Commander of Nyuki Brigade ya 1982, Mahkama Kuu ilieleza kwamba pamoja na kwamba Kamanda huyo ni ofisa wa Muungano, lakini kwa vile amefunguliwa madai Zanzibar lazima ashtakiwe Zanzibar kwa kufuata sheria ya Nyendo za Madai Zanzibar na hivyo haihitajiki kupata ridhaa ya Waziri wa Sheria wa Serikali ya Muungano bali waziri huyo apewe taarifa ya siku 60 kama inavyoeleza sheria ya Zanzibar ya nyendo za madai.

Mahakama Kuu pia iliwahi kutoa msimamo unaofanana na huo katika kesi ya Shaaban Khamis v. Samson Goa and the Commissioner of Police ya 1983.

Mbali ya maamuzi hayo ya Mahkama Kuu ya Zanzibar, Mahkama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya Seif Sharif Hamad v. SMZ ya 1992 ilitoa ufafanuzi bayana zaidi hasa kuhusiana na kesi za jinai.

Katika kesi hiyo Bwana Seif Sharif Hamad alishtakiwa kwa tuhuma za kupatikana na nyaraka za siri za serikali kinyume na Sheria ya Usalama wa Taifa [National Security Act] ambayo ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Hati ya mashtaka [Information] ilitiwa saini na Mkurugenzi Wa Mashtaka wa Tanzania Bara kwa vile ndiye aliyetajwa chini ya Sheria hiyo ya Usalama wa Taifa kwamba ndiye mwenye mamlaka ya kufungua mashtaka.

Mahkama ya Rufaa ilieleza: “Since the High Court of Zanzibar is not a Union matter, then its procedures and officers too are not Union matters.

So if legislation of the Union Parliament which applies to both parts of the Union is silent as to the procedure to be followed in case of litigation or prosecution in the High Court of Zanzibar for purposes either of consent or instituting or conducting prosecution it is the Attorney General of Zanzibar or such officers appointed by him.

The DPP [of the Mainland Tanzania] is not such an officer and as such officer and therefore he could not give his consent nor file information in the High Court of Zanzibar. So the proceedings were and are hereby declared to be a nullity.”

Kwa ufupi, Mahkama ya Rufaa ilibatilisha mashtaka na mwenendo mzima wa kesi kwa sababu DPP wa Tanzania Bara hakuwa na mamlaka ya kufunguwa kesi Zanzibar na aliyepaswa kufungua kesi ni Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, ambaye kwa wakati huo ndiye aliyekuwa na mamlaka ya mashtaka kwa vile ofisi ya DPP Zanzibar ilikuwa bado haijaanzishwa.

Ukichanganya yale niliyoeleza hapo awali na msimamo huu wa Mahkama ya Rufaa, ndio mana hata vyombo husika vya Tanzania Bara walijuwa na bado wanaelewa kwamba kuwasafirisha masheikh na kwenda kuwashtaki Tanzania Bara ni kinyume na katiba zote mbili na ni kinyume na sheria za pande zote mbili za Muungano.

Kama Bwana Masauni alikuwa na nia ya dhati ya kutafuta ukweli na kujiridhisha uadilifu katika suala hili, asingeliacha kutafuta wataalamu wa sheria ambao wanalifahamu vizuri suala hili wakampa ufafanuzi.

Kiini cha Masheikh Kusafirishwa Kupelekwa Dar es Salaam

Inahitaji weledi na kumbukumbu kidogo tu kufahamu kiini cha njama hiyo.

Baada ya vyama kuanzishwa Tume ya Muafaka ya Zanzibar chini ya Sheria Namba 10 ya mwaka 2001, miongoni mwa mambo waliyoyafanya ni kutafuta wataalamu kufanya mapitio ya mfumo wa kisheria wa Zanzibar.

Moja ya jopo la wataalamu hao alilokuwemo Profesa Issa Shivji lilibaini kwamba mashtaka yanatumika vibaya sana kwa malengo ya kisiasa. Na hivyo, wakapendekeza ianzishwe Ofisi huru ya Mkurugenzi wa Mashtaka badala ya mashtaka kuendeshwa na Mwanasheria Mkuu ambaye ana nasaba ya karibu na siasa.

Ilipoanzishwa Ofisi hiyo mwaka 2002 chini ya Katiba ya Zanzibar kupitia Marekebisho ya Nane ya Katiba, nilipata heshima ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka mwanzilishi wa Ofisi hiyo, ambapo niliitumikia kwa miaka 9 kabla ya kuteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu.

Miongoni mwa mambo ambayo yalifanyika ni kuondoa Polisi katika uendeshaji wa mashtaka ili wabaki na kazi ya upelelezi na badala yake mashtaka yaendeshwe na wanasheria wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka [civilianization of prosecution service].

Aidha, sheria za jinai, ile ya Jinai, Sura ya 13 [Penal Decree] na ile ya Nyendo za Jinai, Sura ya 14 [Criminal Procedure Decree] zilifanyiwa mapitio makubwa na kutungwa sheria mpya ya Jinai Namba 6 ya 2004 na ya Nyendo za Jinai, Namba 7 ya 2004.

Miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa katika sheria hizo mpya ni pamoja na kuharakisha mashtaka kwa kuondoa utaratibu wa Uchunguzi wa Awali [Preliminary Inquiry], kuweka ukomo wa upelelezi ambapo muda maalum wa upelelezi uliwekwa kwa makosa mbalimbali na utaratibu wa kuomba kuongezwa muda wa upelelezi na Mahkama.

Aidha, suala la dhamana liliwekwa bayana zaidi. Tokea wakati wa Sheria ya Jinai ya zamani [Penal Decree], hakukuwa na kosa ambalo halina dhamana chini ya sheria za Zanzibar.

Isipokuwa tu kwa makosa makubwa kama vile mauaji, Mahkama Kuu pekee ndio yenye uwezo wa kutoa dhamana. Ilikuwa mazoea kwamba Mahkama Kuu nayo haikuwa ikitoa dhamana.

Hivyo, sheria mpya iliweka bayana zaidi tu utaratibu wa kuomba dhamana Mahkama Kuu hata kwa makosa makubwa endapo mtu amekaa mahabusu muda mrefu na hakuna dalili kwamba upande wa mashtaka unafanya juhudi za kuridhisha katika upelelezi.

Mfumo mpya wa mashtaka ulisisitiza sana upelelezi ufanyike kwanza kabla ya kufunguwa mashtaka. Hatua hizo zilipunguza sana mahabusu, kesi za kubambikiwa na kesi za kisiasa.

Rais Karume, kwa juhudi zake binafsi alihimiza kufanya kila aina ya mageuzi ambayo yataleta ustaarabu katika kusimamia mashtaka.

Mfumo huo wa uendeshaji wa sheria za jinai ulionekana kikwazo kwa baadhi ya maofisa wa polisi, hasa wale waliotoka Tanzania Bara.

Na kwa hakika kutokana na kauli mbalimbali za walioandaa mpango wa kuwasafirisha masheikh hao kwenda Dar es Salaam, hilo ndio ilikuwa kiini cha masheikh hao kufanyiwa dhulma waliyofanyiwa na wanayoendelea kufanyiwa sasa.

Ninachojiuliza tu ni kwamba hivi Bwana Masauni hata akipata ukweli juu ya hili, bado ataona masheikh wanafanyiwa uadilifu? Pengine ni vibaya kutangulia kumhukumu, lakini naamini kama angekuwa na dhamira ya kweli ya kutafuta ukweli asingeshindwa kulijua hili.

Tathmini ya Masauni

Katika maelezo yake, Masauni anasema kwamba alienda kuwaona masheikh hao na wakamuhakikishia kwamba hawana tatizo lolote isipokuwa la kesi yao kuchelewa.

Aidha, walimuahidi kwamba hawatokubali kutumika tena katika siasa. Alienda mbali zaidi kutuhumu kwamba inawezekana walihusika, kwa namna moja au nyengine, katika kadhia za watu kumwagiwa tindi kali na Padri mmoja kuuliwa Zanzibar.

Na huyu ni mtu anayejinasibu na kutafuta ukweli na anayeamini kwamba yanayofanywa ni ya uadilifu. Hili limenishangaza na kunikumbusha mmoja wa watu waadilifu sana naye ni Seyyidna Omar Ibnul Khattab.

Katika kitabu chake cha MAISHA NA NYAKATI ZA SEYYIDNA OMAR, Dr Ali Mohammad as-Sallabi, miongoni mwa visa vingi vinavyofafanuwa misingi ya uadilifu iliyosimamiwa na Seyyidna Omar, ameeleza kisa cha Gavana wa Misri, Amr ibn Al-As.

Siku mojawapo vijana walikunywa kinywaji ambacho hawakujua kama ni kilevi. Baada ya kinywaji hicho kuwalewesha walifikishwa mbele ya Gavana wa Misri ili wapewe adhabu kwa kulewa. Ingawa mwanzoni alisita, lakini alitekeleza adhabu [hadd] kwa kuwachapa bakora na kuwanyoa nywele zao hadharani.

Lakini aliitekeleza adhabu hiyo hiyo kwa mmoja wa vijana hao kwa faragha akiwa ndani ya nyumba yake. Alifanya hivyo kwa sababu kijana huyo alikuwa mtoto wa Seyyidna Omar, ambaye ndiye aliyekuwa Khalifa wa Dola ya Kiislamu wakati huo na ambaye ndiye aliyemteua Amr kuwa Gavana wa Misri.

Alipopata habari hiyo, Seyyidna Omar alimpelekea Amr barua kali ya kumuonya kwa kufanya upendeleo huo na akamtanabahisha kwamba yeye Omar kama kiongozi hampendelei yeyote katika kutimiza wajibu wake.

Kisa chengine chenye mafunzo makubwa ni pale mtoto wa Gavana huyo alipompiga kijana mmoja wa Kimisri lakini Amr hakuchukuwa hatua yoyote dhidi ya mtoto wake.

Seyyidna Omar alimuita yeye na mtoto wake na baada ya kumkanya akamtaka afanye suluhu na aliyefanyiwa kitendo hicho.

Mbali ya hayo, alimwambia maneno ambayo huwa yananukuliwa sana na wapenda uadilifu. Alimwambia: “Hivi wewe ni nani wa kuwafanya watumwa watu waliozaliwa na mama zao wakiwa huru!?

Masauni yeye hajakerwa na Masheikh hao kuwekwa ndani muda mrefu kwa kisingizio cha upelelezi kutokamilika. Na bado anajinasibisha na uadilifu na uumini.

Uadilifu unahitaji ukerwe na kila chenye harufu ya dhulma, harufu ya uonevu na harufu ya upendeleo. Ndio viongozi waadilifu wa kweli kama Seyyidna Omar walivyotufunza kwa vitendo.

Inawezekana Masauni hafahamu kwa sababu hakuwepo, kwamba masheikh hao hawajawahi kuhusishwa wala kutuhumiwa kisheria kwa makosa aliyoyataja ya kumwagiwa watu tindikali wala kuuawa kwa Padri. Majalada ya kesi hizo yapo na angeweza kujiridhisha.

Ni vyema kumtanabahisha kwamba kumsingizia mtu iwe moja kwa moja au vyenginevyo kwa madhumuni tu ya kuonyesha kwamba ni mbaya ni kiwango cha juu cha kukosa uadilifu ambao Masauni anapenda kujinasibisha nao.

Ndio maana Allah [SW] katika Surat Al-Furqan [Sura ya 25], alipotaja sifa za watu wema amesema kwamba watu wema ni pamoja na wale ambao sio mashuhuda wa uongo na wanapokutana na mambo ya kipuuzi huyapita huku wakibaki na heshima.

Allah ameliunganisha hili la ushuhuda wa uongo na mambo ya upuuzi [laghwa] kwa sababu mara nyingi ni katika mambo hayo ya laghwa ambapo shetani huipamba starehe ya kupita, dhulma na haramu mpaka watu wakafika kuwa shuhuda wa uongo. Ni wazi na shetani naye amempambia Masauni laghwa katika jukwaa la siasa.

Hivi Masauni hafahamu kwamba masheikh hao kukaa ndani kwa miaka sita sasa ni adhabu ya kudhiisha na kudhalilisha? Masheikh hao ni watu wenye familia, wenye ndugu, wenye watoto, wenye wanafunzi, wafuasi, majirani na wahisani.

Wapo ambao ndoa zao na familia zimeparaganyika kwa sababu tu ya wenyewe kuwa mahabusu. Wapo ambao familia zao zinaishi kwa dhiki kubwa kwa sababu ya wao kutokuwepo.

Wapo ambao wazee wao wanaumwa kwa sababu ya fikra juu ya watoto wao. Fikiria pia afya na siha za watu hao ambao wapo kizuizini huku wao wakiwa na yakini kwamba wapo kizuizini sio kwa tuhuma za jinai, bali kwa dhulma ya dhahiri.

Bado unapata sura, mdomo na maneno ya kujinasibisha na uadilifu katika kulishughulikia suala lao?

Please soma part lll

Share: