Habari

Othman Masoud: Masauni amelewa pombe gani?

Masheikh wa Uamsho wakipandishwa gari la polisi kutoka mahakamani Zanzibar

Na Othman Masoud Othman
Sources: Jamii Forums – Jumatano tarehe 1 Mei 2019
part lll

Nini Hasa Kosa la Masheikh?

Hakuna asiyejuwa, hata wale wanaojitowa fahamu, kwamba masheikh hao wapo ndani ikiwa sehemu ya uwekezaji unaofanywa kuwanyamazisha wote wanaodai haki zao kama wananchi wa Zanzibar ndani ya Muungano.

Na wanafanya hivyo kwa njia ya amani, kwa njia zinazokubaliwa kisheria, njia ya kusema na kutoa mawazo yao. Uwekezaji huo umeanza siku nyingi na bado unaendelea. Hilo ndio kosa walilolifanya na kukamatwa chambilecho Wazungu “red-handed”.

Lakini naomba nimtanabahishe Masauni maneno ya mwanasiasa mahiri wa Uingereza Bwana William Pitt [Earl of Catham] aliyoyasema katika Bunge la Uingereza tarehe 14 Januari 1766 wakati akiwatetea na kuwaunga mkono Wamarekani kwa kudai haki zao kutoka kwa Waingereza:

“Gentlemen have been charged with giving birth to sedition in America. They have spoken their sentiments with freedom against the unhappy act, and that freedom has become their crime. Sorry I am to hear the liberty of speech in this House imputed as a crime…I rejoice that America has resisted.”

Nadhani Bwana William Pitt anastahiki kujinasibisha na uadilifu kwa kuisema Serikali yake ndani ya Bunge akiwatetea wale ambao wanaoshtakiwa kwa makosa ya uchochezi kwa kudai haki zao huku akionesha wazi kuwa anawaunga mkono katika harakati zao.

Aidha, ni vyema Masauni akakumbuka kwamba historia ya dunia imethibitisha kuwa huwezi kutumia nguvu na vitisho kunyamazisha watu wanaodai haki zao.

Wenye busara kama vile mbunge mwengine maarufu wa Uingereza, Bwana Edmund Burke, naye katika hotuba yake katika Bunge la Uingereza aliyoitoa Machi 1775 aliitanabahisha serikali yake kwamba matumizi ya nguvu hayajawahi kusaidia katika kunyamazisha harakati za binadamu kudai haki yake. Yeye alisema:

“The use of force is but temporary, it may subdue for a moment, but it does not remove the necessity of subduing again; and a nation is not governed which is to be perpetually conquered.”

Hoja ya Masauni ya Siasa za Kuligawa Taifa

Miongoni mwa maneno mazuri sana aliyoyasema Bwana Masauni ni yale ya kukemea siasa za kuligawa taifa. Jinsi ya alivyosema yale maneno kwa hisia, binafsi natamani sana ingekuwa kauli yake ya dhati kabisa.

Kutokana na ushawishi wake wa kisiasa, angeisaidia sana Zanzibar kuondokana na maradhi ya ubaguzi na mifarakano inayopandikizwa kila uchao hata kwa kizazi cha kesho.

Lakini hivi Masauni hajui nani walioko mstari wa mbele kupandikiza fitna hiyo? Wanasema hata hofu ya Mungu hawana. Wanasema hadharani, kwa mabango na matangazo kauli za kupandikiza chuki na kukigawa hata chama chao kwa misingi ya rangi, asili na kabila.

Wapo waliokwenda mbali zaidi na kusema katika mikutano ya hadhara na vyombo vikuu vya nchi kwamba Serikali ya Zanzibar haiwezi kutolewa kwa njia ya kura kwa vile imepatikana kwa mapinduzi. Ndio tuseme Masauni anataka tuamini kwamba hajawahi kuyasikia au kuyaona hayo yote? Tumuulize ni lini ameyakemea hata kwa faragha?

Na yapo mengine mabaya zaidi ya hayo ambayo yanajenga mizizi ya chuki ya muda mrefu zaidi kwa vizazi vyetu na ambayo tunaamini kama Masauni hakushiriki kuyaandaa, basi angalau anayajuwa vizuri lakini hayajawahi hata kumuuma kwamba ni mabaya kwa mustakbali wa taifa.

Hitimisho

Inasikitisha sana kwamba katika karne hii ya maendeleo makubwa sana ya binaadamu, katika taifa letu bado wapo viongozi wanaotumia rasilimali na nguvu nyingi kushughulikia mambo ambayo hayaongezi tija wala sifa yoyote kwa taifa.

Kama angekuwa na dhamira ya dhati ,Masauni angeisaidia sana Serikali kupata ukweli na ufumbuzi wa suala la masheikh wale wanaoteseka kwa sababu tu ya hakuna aliyepo tayari kuwa mkweli.

Watu wote niliowataja na wengine ambao sikuwataja wanaolijuwa suala la masheikh kwa undani wapo na ni wazima wa afya.

Mimi naamini kwamba wanaweza kusaidia sana kuueleza ukweli. Baadhi yao wamestaafu na hiyo inawapa fursa ya kuwa wawazi zaidi.

Mimi naamini viongozi wetu wa sasa walibebeshwa tu suala la masheikh. Ukizingatia kwa makini kauli ya Mwigulu Nchemba, kauli ya Profesa Kabudi na kauli ya Masauni zinavyopishana ni dhahiri kwamba yapo mambo viongozi hawaelezwi ukweli.

Kama nilivyotangulia kueleza kwamba lilipotokea suala hili,Rais Magufuli hakuwa ameanza hata mchakato wa Urais na Dkt Shein naye hakuwepo hata nchini.

Ni busara wakachukuwa nafasi yao kama viongozi waliobebeshwa tu suala hili na kulipatia ufumbuzi wa haraka. Kwa Dkt Shein, itamsaidia sana kama atatanabahi ule msemo wa Kiswahili unaosema:

“Ukishapata Mlango wa Kuingia basi Tafuta na wa Kutokea”. Rais Dkt Amani Karume nadhani aliukumbuka msemo huu na leo kwa hakika anafaidika nao.

TANBIHI: Mwandishi wa makala hii aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Ofisi ya Mwendesha Mashitaka na kisha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Kutokana na ukubwa au urefu wa MAKALA, haikuwezekana kukaa ‘page’ moja wala mbili, nimeona bora kuigawa part 3 ili itie hamu isomeke vizuri, bila kumchosha msomaji.

Share: