Habari

Othman Masoud: Masauni amelewa pombe gani?

Masheikh wa Uamsho ambao wako mahabusu hii ni Ramadhani ya sita katika Gereza la Ukonga, Dar es Salaam.

Na Othman Masoud Othman
Sources: Jamii Forums – Jumatano tarehe 1 Mei 2019
part l

Kijijini kwetu alikuwepo mzee mmoja ambaye alikuwa maarufu sana. Miongoni mwa mambo yaliyompa umaarufu ni jinsi alivyokuwa mweledi katika elimu ya dini ya Kiislamu kiasi cha kuwafundisha baadhi ya walimu wakubwa katika kijiji hicho.

Pamoja na taaluma aliyokuwa nayo, alikuwa mpenzi mkubwa wa pombe. Kwa ufupi alikuwa mlevi, unaweza kusema mlevi wa kupindukia.

Katika sikukuu moja ya Eid-ul-Fitri majira ya laasiri akiwa ameshauchapa ulevi hajiwezi, akitembea kwa shida, alikutana na watu wakiwa wamebeba jeneza wakielekea makaburini kuzika. Aliwaangalia kama vile ni jambo geni kwake, kisha akasema:

“Jamani watu wengine nao hawachagui hata siku ya kufa? Inakuwaje leo siku ya sikukuu mtu unakwenda kujifia? Siku ya furaha unaigeuza ya msiba.” Maneno yake hayo yakawa gumzo kubwa kijijini.

Siku ya pili watu kadhaa walimfuata kumuwaidhi kwamba sasa pombe inampeleka kubaya mpaka anafanya utani na kudura za Allah. Miongoni wa waliomfuata ni sahibu yake wa karibu sana ambaye alimueleza:

“Sahibu yangu sasa pombe inakumaliza. Mimi ninajua miaka yote unalewa, lakini hivi vituko vyako vya jana naona ulevi unakumaliza!”

Na yeye mwenyewe akamjibu kwa upole: “Ni kweli unayosema. Hata mimi najiuliza sijui jana nililewa pombe gani. Lakini kila lenye mwanzo lina mwisho. Mimi kuanzia leo nnaweka nia ya kuacha ulevi!”

Na kweli, baada ya muda aliwacha kabisa pombe, akafanya kazi ya ualimu na mtu wa kushikamana na dini.

Maelezo aliyoyatoa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni wiki chache zilizopita katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusiana, pamoja na mambo mengine, Masheikh wa Zanzibar waliopo mahabusu katika Gereza la Ukonga Dar es Salaam yamenikumbusha kisa hicho nilichokieleza hapo juu.

Nimejiuliza peke yangu, nikaona haitoshi, niulize na wenzangu akiwemo na yeye mwenyewe (Hamad Masauni), hivi amelewa pombe gani iliyompelekea aeleze mambo ambayo hata mtoto mdogo anaweza kubaini kwamba ni ya kuhadisiwa?

Napenda nieleze kwa ufupi kwa nini nimejiuliza Masauni amelewa pombe gani. Ndani ya bunge kumekuwa kukitolewa maelezo kuhusiana na kadhia ya masheikh hao na baadhi ya mawaziri ambayo ni ya kusikitisha; mengine ya uongo wa wazi na mengine ya ubabaishaji wa kupindukia.

Nimewahi kuona Mwigulu Nchemba akitoa maelezo ya ubabaishaji bungeni kuhusiana na kadhia ya masheikh wakati akijibu suali la Mheshimiwa Dkt. Suleiman Ali Yussuf.

Aidha, nimewahi kushuhudia mwalimu wangu, Profesa Palamagamba Kabudi, akifanya siasa bungeni kwa kupitia haki za raia hao ambao hadi sasa hawana hatia.

Lakini, maelezo ya Masauni kwa hakika yaliniuma sana kiasi cha kunisukuma kuandika ukweli ninaoufahamu katika kadhia hiyo. Imeniuma kwa vile alitoa maelezo akiwa amejitanda kilemba cha uumini na kupenda uadilifu.

Kupenda uadilifu ni kitu chema sana, lakini kuna msemo wa wanafalsafa unaosema: “The principle of being principled is to be principled.” Kwa ufupi huwezi kuwa muadilifu nusu nusu. Ukiamua kujinasibisha na uadilifu, lazima uonekane au angalau ufanane na uadilifu.

Masheikh Kukamatwa na Kusafirishwa Tanzania Bara

Wakati masheikh hao walipokamatwa, Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein alikuwa katika safari ya kikazi katika visiwa vya Samoa. Dkt. John Pombe Magufuli, nadhani, wakati huo hakuwa ameanza hata mchakato wa kugombea urais au hata fikra ya kugombea nafasi hiyo.

Mhandisi Hamad Masauni yeye alikuwa mbunge wa kawaida, sidhani kama alishaanza kuwa na ndoto ya kuwa naibu waziri. Mimi wakati huo nilikua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar.

Siku ya pili tu tokea kukamatwa masheikh hao usiku mkubwa na asubuhi wakasafirishwa kupelekwa Dar es Salaam, baadhi ya wazazi na jamaa wa masheikh hao, wake kwa waume walinifuata ofisini.

Kilikuwa kikundi kikubwa kwa kweli. Mmoja kati ya hao alikuwa mke wa mmoja wa wahusika na mmoja ni mama mzazi wa mmoja wa wahusika. Maelezo yao jinsi ya walivyokamatwa yalikuwa ya kusikitisha sana.

Niliwaahidi kwamba nitafuatilia kwa haraka suala la kusafirishwa kwao kupelekwa Dar es Salaam, kwani ninahisi haikuwa sawa kisheria. Siku hiyo hiyo niliomba kuonana na Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, na nilipata miadi ya kuonana naye siku ya pili asubuhi.

Nilipokutana na Makamo wa Pili wa Rais nilimweleza kwamba, suala la watu kukamatwa ni jambo la kawaida na ndio kazi ya polisi kama wanatuhumu mtu ametenda kosa la jinai.

Hata hivyo, sababu ya kuonana naye ni kueleza maoni yangu ya kisheria juu ya uharamu wa kitendo cha kuwasafirisha kwenda Dar es Salaam chini ya Katiba ya Zanzibar na Sheria.

Nilimpa mfano wa kadhia ya watu waliokamatwa Zanzibar kwa tuhuma za uchochezi kwa kutangaza kutaka Pemba ijitenge.

Wahusika hao walipokamatwa, Rais Amani Karume alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Marekani, lakini aliporudi tu siku ya pili akamuita Mwanasheria Mkuu, Mheshimiwa Idi Pandu, na mimi binafisi nikiwa Mkurugenzi wa Mashtaka, na kutuhoji kwa nini tuliruhusu watu hao wasafirishwe kupelekwa Dar es Salaam kwa tuhuma za kosa lililotokea Zanzibar.

Nakumbuka alihoji: “Hivi hao watu kama wamesema, si wajibiwe tu? Na kama ni lazima wakamatwe na kuhojiwa, hivi Zanzibar hapana Serikali, hapana Mwendesha Mashtaka, hapana Mahkama?”

Baada ya kumjibu kwamba watu wamekamatwa na kusafirishwa bila ya sisi kushauriwa, alimwita Kamishna wa Polisi naye baada ya kumhoji akampa amri watu hao warejeshwe Zanzibar haraka na kama wana tuhuma zozote waje washtakiwe Zanzibar. Baada ya siku mbili watu hao wakarejeshwa Zanzibar.

Aidha, nilimweleza Makamo wa Pili wa Rais msimamo wa kisheria uliotolewa na Mahkama Kuu ya Zanzibar chini ya wakati huo Jaji Mkuu Augustino Ramadhani na pia Mahkama ya Rufaa ya Tanzania ambapo Mahkama hiyo ilielekeza wazi kuwa mtu anapotuhumiwa kwa kosa lolote lililotendeka Zanzibar, hata kama kosa hilo ni chini ya Sheria ya Muungano, basi lazima ashtakiwe na mamlaka ya mashtaka ya Zanzibar, katika Mahkama ya Zanzibar na kwa kutumia sheria za nyendo za jinai za Zanzibar. Baada ya kumueleza hivyo aliahidi atalifatilia kwa Kamishna wa Polisi Zanzibar.

Kilichonishangaza sana ni kwamba wakati Dkt. Shein aliporudi kutoka safari, alituita mimi nikiwa Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka, Bwana Ibrahim Mzee, tukiwa pamoja na Makamo wa Pili wa Rais.

Miongoni mwa mambo aliyotuarifu ni kwamba Jeshi la Polisi wanataka tutowe wanasheria wa Serikali kutoka ofisi zetu mbili waende Dar es Salaam wakashirikiane nao kuwahoji watuhumiwa kwa vile wanasheria wa Zanzibar wanazielewa vizuri zaidi sheria za Zanzibar.

Mimi nilitangulia kumueleza kwamba: “Kabla hujarudi safari, nilionana na Makamo wa Pili na kumpa ushauri wangu wa kisheria kuhusu kadhia hiyo na nilimueleza kwa kina msimamo wa kisheria na kwamba kusafirishwa watu hao na kwenda kuhojiwa na kushitakiwa Dar es Salaam ni haramu!”

Ilionesha dhahiri kwamba hakuwa amearifiwa kabla juu ya ushauri huo. Nilimalizia kwa kumwambia kwamba: “Kwa vile suala hilo si halali, nikitowa wanasheria kufanya kazi hiyo, nitakuwa ninabariki kitu batili!”

Naye Mkurugenzi wa Mashtaka akatoa maelezo nadhani fasaha zaidi ya kuunga mkono kwamba suala hilo lilikuwa batili na si vyema kwa wanasheria wa serikali kutumika kubariki batili hiyo.

Rai iliyotolewa ni kuwa Makamo wa Pili aitishe kikao cha vyombo vya ulinzi vinavyohusika na kadhia hiyo ili kupata muafaka.

Siku ya pili tukaonana na vyombo husika chini ya uenyekiti wa Makamo wa Pili wa Rais. Si vyema kueleza kwa urefu yaliyojiri katika kikao kile lakini inatosha kusema kwamba hatimaye angalau mmoja wa maofisa waandamizi wa Tanzania Bara, aliyepigiwa simu tukiwa katika kikao kile alikiri kwamba hata wao wanafahamu kwamba hilo jambo lina matatizo ya kisheria.

Lakini kwa sasa wanachotaka ni kupata ukweli wa tuhuma hizo na ndio maana wakaomba msaada wa wanasheria wa serikali kutoka Zanzibar.

Baada ya maelezo hayo, busara iliyotoka ni kuwa wanasheria wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka waende Dar es Salaam kama ilivyoombwa kwa vile ofisi hiyo ndiyo inayohusika na mashtaka na sio Ofisi ya Mwanasheria Mkuu.

Siwezi kuyasema yale wanasheria hao walioenda Dar es Salaam waliyoeleza baada ya kurudi safari hiyo, lakini naamini Bwana Masauni kama ana nia ya dhati ya kutafuta ukweli atawatafuta wanasheria hao kwa vile bado wapo.

Katika maelezo yake, Bwana Masauni anasema kwamba amejiridhisha kuwa serikali imesimamia suala hili kwa uadilifu na kama angelihisi haisimamii kwa uadilifu, angejiuzulu na akaungana na wale wanaohoji kadhia hiyo.

Suala langu ni kwamba hivi serikali inaposhauriwa na Mwanasheria Mkuu ambaye, chini ya kifungu cha 20(1) cha Sheria Namba 6 ya 2013, ushauri wake wa kisheria ndio msimamo rasmi wa kisheria wa serikali isipokuwa kama Rais atatoa maelekezo tofauti au utenguliwe na mahkama, na ikaenda kinyume na ushauri huo, huo ndio uadilifu?

Mbali ya ushauri wa Mwanasheria Mkuu, katika masuala ya kesi za jinai, Serikali inapokwenda kinyume na ushauri wa Mkurugenzi wa Mashtaka, nao huo ndio uadilifu anaouzungumzia Bwana Masauni?..

Please soma part ll

Share: