Habari

PBZ Itupiwe Jicho! Laa si hivyo inakwenda zake.

KATIKA kipindi cha takribani miezi mitatu iliyopita, tumeshuhudia benki tatu nchini Kenya zikianguka na kupelekea kushindwa kuendelea na utoaji huduma za kibenki. Zipo sababu lukuki zinazopelekea taasisi za kifedha kushindwa kumudu uendeshaji wa huduma zake.

Hili si jambo geni hata kidogo duniani kutokea na hata hapa Zanzibar kumbukumbu zinaonesha kuwa benki ya Greenland ilikumbwa na kadhia hii ya kifedha na pia tukumbuke benki mama ya serikali hapa Zanzibar, PBZ pia ilikumbwa na mkasa huu na kufikia hatua mbaya kabisa ya nakisi ya mtaji.

Taasisi za kifedha kama benki zimeshikana sana kwa vile taratibu nyingi na teknolojia za uendeshaji wake zinafanana na ule msemo wa “mwenzio akinyolewa basi wewe utie maji”.

Kilichosababisha Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) iinuke na kuwa hivi ilivyo sasa ni huruma za Dkt. Amani Karume (Rais mstaafu wa awamu ya sita Zanzibar) kwa kutupilia mbali taarifa zote za kifedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Benki ya Dunia (WB).

Ishara hii ya benki kubwa kama Chase Bank, Imperial, NBK na Dubai Bank za Kenya kuanguka inapaswa ipewe uzito unaostahili kwa vile ni suala linaloweza kutokea hapa kwetu wakati wowote.

Sababu kuu za kuanguka kwa benki hizo za Kenya zinasemwa kuwa ni upambaji wa taarifa zao au taaarifa za kupika, kutofuata utaratibu wa mikopo kwa wakurugenzi wake (compliance), pia kutofanyika ukaguzi halisi wa kibenki (Bank Audit) na hivyo kupelekea kutojua kiasi cha tatizo katika benki husika.

Benki zote hizo katika taarifa zake za mwaka 2014 zinashangaza sana kwa kutosema ukweli wote. Kwa mfano, Chase Bank ilidai kupata faida ya shilingi za Kenya bilioni 2.3 wakati huo lakini sasa inadai kupata hasara ya shilingi za Kenya (Ksh) milioni 742 mwaka 2015.

Pia NBK ilitangaza kupata faida ya Ksh. 817 milioni mwishoni mwa mwaka 2014 na sasa imetangaza kupata hasara ya Ksh. 1.2 bilioni mwaka 2015. Ni kwa haraka kiasi gani benki hizo zimepata hasara kwa muda mfupi?

Hakuna jawabu lingine la swali hili zaidi ya ukweli kwamba wanachofanya wenye mabenki hawa ni kupika taarifa zao kwa kuwatumia wakaguzi na wahasibu wao. PBZ pia ina mapungufu mengi kwenye maeneo hayo.

Kwa kuogopa yasiwatokee matatizo ya namna hii, Imperial Bank ya Kenya imemshtaki mkaguzi wake wa nje (External Auditor) ambayo ni kampuni ya KPF kwa kushindwa kutoa taarifa za kweli kuhusu hali ya benki yao na mwenendo wake na pia kutotoa hatua za kuchukuliwa.

Pia kampuni maarufu ya kimataifa ya ukaguzi ya KPMG nayo imekumbwa na kashfa kama hiyo ya kutowajibika katika ukaguzi kwenye benki ya Trust. Kumekuwa na utaratibu wa kufanya mambo kwa mazoea matokeo yake yanapoharibika tunaanza kumtafuta ‘mchawi’ bila kuangalia wapi tumejikwaa, tunainukaje na kusonga mbele.

Ujuaji na ubabe kwa viongozi wasiojali taarifa za kitaalamu, kutokuwa tayari kuelekezwa na kujifanya wajuaji wa kila kitu katika ulimwengu huu ndiyo kiini kikubwa cha haya matatizo yanayotokea Kenya sasa na yaliyowahi kutokea Zanzibar katika siku za nyuma.

Kwa PBZ inapaswa kuwa makini kwenye maeneo ya ukaguzi na kupewa taarifa sahihi kwenye mwenendo mzima wa benki na hata kama hali si nzuri ili kuepuka kadhia kama hii.

Kuna taarifa zinaenea kuwa PBZ inaingiliwa sana kisiasa taungu kuondolewa kwa Mkurugenzi Mkuu wake wa zamani na baadhi ya wajumbe wa bodi yake na ni wazi kuwa sasa kuna ukosefu wa utashi wa kuisimamia benki hii kwenye misingi yake.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pia ina jukumu hilo la kuisimamia benki hii na kujiridhisha na miamala yake yote ili kuweza kulinda amana za wateja wake.

Pia kitengo cha ukaguzi wa ndani cha PBZ (Internal Auditor) na kitengo cha usimamizi wa utaratibu vinaonekana kuwa na upungufu mkubwa wa utaalamu na uzoefu wa kujua benki katika kiwango hicho na kuweza kujua tatizo kwa kiasi kikubwa sana.

Uchache wa wafanyakazi kwenye vitengo husika pia ni tatizo ambalo linazungumzwa huku kukiwa na madai kuwa hata wafanyakazi hao waliopo wengi hawana uzoefu unaohitajika na weledi katika eneo hilo la ukaguzi.

Mfano kitengo cha PBZ kwenye uismamizi wa utaratibu (Compliance Department) kuna wafanyakazi wanne kwa ujumla-huku watatu wakiwa ni wafanyakazi ambao hawajawahi kufanya kazi benki nyengine yeyote isipokuwa PBZ.

Pili kunaelezwa kuwa na tatizo la wafanyakazi ambao hawana ubobezi wa benki na uzoefu wao ni miaka chini ya mitatu kwenye benki. Kwa upande wa PBZ, kinachoonekana si kuwa na upikwaji wa taarifa bali ni kuwa hizo taarifa zikawa si za kweli kwa aina ya watu na mwenendo mzima wa benki kwa sasa.

PBZ upande wa Benki ya Kiislamu mpaka leo wanatumia mfumo wa Excell kwnye ripoti zao za eneo nyeti kabisa la mikopo. Hili linafanya kuwepo na urahisi wa upotevu wa taarifa, uwezekano wa mteja kutokulipa uko wazi kabisa na pia mteja kuwekewa taarifa ambazo si sahihi liko wazi.

Hivi karibuni kuna mteja mmoja aliandikiwa barua ya kudaiwa awamu tatu (Instalments) hali ya kuwa hadaiwi kabisa. Pia kuna mteja amekaa miezi minne bila kukatwa marejesho ya mkopo kwenye akaunti yake huku pesa zikiwemo, pia malamiko ya kuingiziwa pesa zaidi ya mara moja kwenye mshahara ama malipo ama kutolewa pesa zaidi.

Hapa ndipo unapoona ukubwa wa hatari walionayo PBZ. Wanaweza wakawa wanatengeneza taarifa bila ya kuzipika lakini athari zake zikawa kama au zaidi ya zile zilizopikwa ambazo sasa zinaua benki za Kenya.

PBZ inakosa pia watu wenye uwezo wa aina ya benki zilizopo kwingineko hapa duniani ambao wamejaa uzoefu wa kujua benki kwa kiwango kikubwa cha kimataifa, sio kuwa tu na wafanyakazi bali kuwa na wafanyakazi bora, weledi na ambao wameendelezwa vizuri ndani na nje.

Kwa ushauri wa mtaalam wa mambo ya kibenki, Alex Brummer, kwenye kitabu chake Bad Banks “in this sector at least history had – and still has – a habit of repeating itself.”

Kwa hiyo PBZ hawakuugua ‘kipindupindu’ miaka ya 1990 kwamba wana kinga bali wanahitaji kukaa sawa kwelikweli na kuwa na watu makini ili kukimbizana na changamoto za kibenki leo badala ya kuendelea kufanya kazi kimazoea.

Itoshe kwa waliokabidhiwa dhamana kujua wajibu wao hususani kwenye sekta za umma na kuweka watendaji weledi ambao watafanya kazi kwa ufanisi na kuwa chachu ya kupiga hatua mbele badala ya kurudi nyuma.

Chanzo: Raia Mwema

Tagsslider
Share: