Habari

PEMBA, MUHANGA WA SIASA

PEMBA ni moja ya visiwa viwili ndugu vinavyounda nchi ya Zanzibar. Pamoja na kuwa na jamii inayofanana kwa mambo mengi ikiwemo lugha, dini, mila, desturi na silka, bado tofauti ndogo za kiasili, kikabila na kisiasa zimeweza kuigawa Zanzibar katika makundi yanayovutana na kuhasimiana. Zanzibar inaundwa na jamii zenye asili kuu mbili – wale wenye chimbuko lao kutokea ndani ya Bara la Afrika na wale wenye chimbuko lao kutokea nje ya bara hilo, hasa kutoka Bara Hindi, Ghuba ya Uajemi na Arabuni.

Pemba ni jamii iliyopata bahati ya kuwa na kizazi mseto cha asili na makabila yote yaliyopo Zanzibar. Wakati katika kisiwa cha Unguja, jamii za makabila tofauti ziliishi kwa kujitenga kimiji na kindoa huko nyuma, jamii hizo kwa upande wa Pemba zilichanganya damu kwa kuoana na kuzaliana na kufanya jamii moja ya Wapemba isiyogawika kwa misingi ya kabila na rangi ya ngozi.

Nafasi ya mwanajamii haiwezi kutenganishwa na hali halisi ya utamaduni, historia, siasa na uchumi ndani ya jamii husika. Mivutano mingi yenye sura ya kihistoria bado inaendelea kufanywa kuwa ni sehemu muhimu ya maisha ya sasa ya Zanzibar. Ubishi utokanao na tofauti za kikabila na kiasili, matabaka ya kiuchumi na itikadi za kisiasa ni mambo yenye mizizi ya kihistoria iliyoanzia mbali ambayo ni lazima iwekwe wazi ili kuweza kuitathmini na kuifahamu hali ya sasa. Historia ya Zanzibar katika mizania ya ukabila na unasaba, inao mchango wake muhimu katika jinamizi linalowatesa Wapemba kwa muda mrefu (Beverly 1999).

Pemba inayo nafasi kubwa katika historia ya mapambano ya kujitawala inayoanzia katika zama za kale na inayoenea nje ya mipaka ya visiwa vya Zanzibar. Pemba imekuwa mstari wa mbele katika zama zote na katika mapambano ya aina zote, yalitiwa msukumo mkubwa na Wapemba. W. H. Ingrams, mwandishi wa kitabu maarufu kiitwacho Zanzibar, Its History and Its People, anawataja Wapemba katika mapambano dhidi ya Wareno kama watu waliojizatiti na kuamua. Wakati baadhi ya jamii za kienyeji za Afrika Mashariki zikisalimu amri kwa maovu ya Mreno, Wapemba wao walipambana mpaka tone lao la mwisho la damu. Wareno nao waliihesabu Pemba kama eneo
korofi na kituo kikuu cha upinzani dhidi ya mikakati yao ya utawala.Pamoja na kushiriki kwa roho na damu katika safari ndefu ya mapambano dhidi ya ukoloni, ubeberu na ukandamizaji, Wapemba hawakutambulika na mchango wao haukuthaminiwa. Badala yake, Wapemba – katika zama zote – wamekuwa watu wanaoteseka katika kila eneo linalohusu maendeleo ya mwanaadamu.

Katika zama za Usultani na baadae Muingereza Pemba ilibaki ni eneo lenye vijiji vya kienyeji vilivyokuwa nyuma kimaendeleo ambapo watu wake walidhihakiwa kwa kuwachezea ngoma watawala wanapokwenda kuzuru kisiwa hicho. Katika muongo wa Mapinduzi ya 1964 na miaka kadhaa baadae, Pemba iligeuka eneo la kujengea nidhamu ya Kimapinduzi ambapo wakaazi wengi wa kisiwa hicho waliteseka kwa jina la Mapinduzi hayo. Katika zama za sasa za Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa ulioanzia mwaka 1992, Pemba ndio imekuwa muhanga wa siasa. Matokeo ya uovu wa siasa hizi za vyama vingi, ambayo ni ubaguzi wa rangi, asili na kabila; ubaguzi katika ajira, Elimu na uongozi wa nchi; unyanyasaji, utesaji na mauwaji, takwimu zinathibitisha kwamba Wapemba ndio wamekuwa shabaha na waathirika wakuu.

Matokeo yake, Wapemba wengi wamekikimbia kisiwa chao na kwenda kuishi nje ya kisiwa hicho, nje ya Zanzibar au hata nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na hilaki na ugumu wa maisha ndani ya ardhi yao. Kizazi hiki kikubwa kilichoko nje ya Pemba hakifurahii kuwa huko katika maisha ya ukimbizi na kuzitenga jamii na familia zao. Wanachotamani siku zote ni kuona siku moja wanarudi na kuifanya ardhi yao ya Pemba kuwa ndio makaazi yao ya kudumu yenye kutoa fursa na neema kwa maisha yao na vizazi vyao.

Jinamizi la Wapemba pia limepewa tafsiri ya malipizo ya visasi dhidi ya wazee wao. Katika maudhui haya, Wapemba wanaitwa Waarabu, wanaitwa waliowapenda Waarabu kuliko Waafrika, waliowasaliti Waafrika weusi na kuwatukuza Waarabu na Magoa, na waliopinga Mapinduzi ya 1964 na kuunga mkono utawala mkongwe uliopinduliwa. Kitabu hiki kinajaribu kuweka bayana kipi ni kipi katika mjengeko wa kijamii, kitamaduni na kisiasa kwa watu wa kisiwa cha Pemba, na kinakusudia kuyasuta yote haya na badala yake kuonesha mchango chanya wa Wapemba katika historia ya mapambano na pia kuonesha uzalendo wao wa jasho na damu kwa nchi yao wanayoiamini na kuipenda – Zanzibar!

……Usikose kufuatilia zaidi haya na mengine mengi katika maudhui ya kitabu “Pemba, Muhanga wa Siasa”.

Kimeandikwa na Ahmed Omar
Dibaji na Mohammed Ghassani
Kimehaririwa na Ally Saleh

Kwa Unguja kinapatikana Masomo bookshop, nyuma ya soko la Drajani na Alif bookshop, Mkunazini.

Kwa upande wa Dar es Salaam wasiliana na Monalisa Joseph Ndala – 0657299225

Kitabu pia kinapatikana online kupitia hapa: http://www.lulu.com/shop/ahmed-omar/pemba-muhanga-wa-siasa/paperback/product-24020342.html

 

 

Share: