Habari

PEMBA- SAYARI ILIYO PWEKE”

“PEMBA- SAYARI ILIYO PWEKE”

Na Seif Al~jahury.

Nikisema Pemba nakusudia kile kisiwa kilicholala juu ya mgongo wa bahari yenye kina kirefu cha maji yaani bahari ya Hindi,na sikusudii ule mji uitwao Pemba ulioko katika nchi ya Msumbiji.

Pemba ni sayari yenye rutba na rangi ya kijani kibichi ambayo Mungu kaitunukia, mvua za kutosha na mazao ya mashambani ni fakhari ya Mpemba, bahari yenye samaki watamu ni tunu wanayoikosa wasiokuwa Wapemba, harufu nzuuri sana ya marashi ya karafuu inashinda ile ya Misk inayopendwa na Waarabu na hii ndio kama nembo ya Wapemba.

Naizungumzia Pemba yenye ustaarabu wa kipekee wa mila, tamaduni, desturi, heshima, na upendo tangu enzi na enzi hadi sasa. Ni ile Pemba wa Wapemba wajuanao kwa vilemba swadakta! Ukipotea njia kama ni mgeni Pemba basi utasitiriwa kwa kula na kulala bila bugudha.

Lugha yao ni Kiswahili tu ambacho hutofautiana lahaja za kipwani, ila wenyewe hufahamiana kiustadi.
Ni Pemba iliotajwa kwenye kitabu cha “Periplus of the Erithrean Sea” kama chimbuko la Ustaarabu Afrika Mashariki hususan ukanda wa Pwani ya bahari ya Hindi. Ndio ileee Achipelago na Zenjibar ikimaanisha bara la watu weusi.

Wapemba wenye mchanganyiko wa kidamu na Waarabu, Waajemi , Washirazi na wengineo ndio hawa ambao wana msimamo mmoja kwa kila maamuzi yao. Dini yao iliobeba 100% ya watu wote ndio muhimili wao wa maisha, Ukiwakera wao basi kauli yao ni Hewallah! Mungu yupo, huruma na mapenzi yao yanawafanya wawe karibu na Mungu wao.

Mazungumzo yao ni Jamvini wakati wa jioni,michezo ya karata,bao la soo huwakutanisha wao pamoja, kahawa na majibizano ya matani hufanya maisha yao kuwa ya furaha na kusahau dhiki walizonazo. Kanga na baibui kama mavazi yao huwasitiri wanawake na vigori, kanzu, vikoi na baraghashia za kufuma ndio haswaa kwa wanaume. Hata mtawala wa Kisultan wa Omani alifikia kusema wakati anakuja kuitawala Zanzibar basi Ustaarabu huu na Utamaduni ulikuwepo zamani.

Maisha ya mlo mmoja kwa siku imezoeleka kwa baadhi ya familia, wao huridhika kuchuma cha halali japo hakitoshi na hulala kwa furaha na matumaini ya kesho watapata kizuri.

Wanasema Wapemba wachawi! Lahaula uchawi upo kila sehemu Duniani ila Wapemba wana utamaduni wa kipekee ndomana wakawa tofauti na wasiowapenda wakawaita wachawi.

Naisemea Pemba kwa sababu ni Sayari iliyotengwa na kama si kusahaulika, ndio hii Pemba yenye karafuu bora zaidi Duniani ila tunzo na sifa za ubora wanapewa wengine wasio na hata shina la mkarafuu, Naizungumzia Pemba kwakua siku zote maisha kwao ni magumu, ni Pemba yenye utajiri mkubwa wa rasilimali za kimaumbile ila Mpemba hafaidiki nazo.

Siasa kwa Mpemba ni kama itikadi ya maisha yao kwakua imejenga historia kubwa sana ya mapambano dhidi ya Udhalimu na Udhalilishaji na hata umwagikaji damu wa ndugu zao, wacha tu iitwe itikadi kwao na wasilaumiwe kwa misimamo yao kwani wana sababu za kufanya hivyo.

Nje ya Pemba Mpemba hana thamani na anaonekana kama vile jiwe la teo lililolengwa na kutorejea tena lilikotoka! Kwani huyu Mpemba akienda kusikokua Pemba kutafuta maisha na maendeleo kafanya kosa? kipi kinamtofautisha Mpemba na asiekuwa Mpemba ukiacha lafudhi zao? je ni rangi, dini, makabila au mwonekano wao? wote ni wamoja.

Wao kukosa imekuwa kawaida na huridhika,lakini dhiki haizoeleki. Mpemba na yeye anataka maendeleo, anataka uhuru, asinyanyaswe kwani hakuzoea maisha hayo.

Mpemba naye anataka viwanda aajiriwe, anataka barabara asafirishe.
Ni wakati sasa, wanahitaji mabadiliko, Wasitengwe, wapewe fursa kwani wanaweza…
Mungu ibariki Pemba, Mungu ibariki Zanzibar.

Share: